Isaya 48

Isaya 48

Mungu muumbaji na mkombozi

1Sikieni haya, enyi watu wa nyumba ya Yakobo, mnaoitwa kwa jina la Israeli, mliotoka katika maji ya Yuda; mnaoapa kwa jina la BWANA, na kumtaja Mungu wa Israeli, lakini si kwa kweli, wala si kwa haki.[#Kum 6:13; Yer 7:9; Sef 1:5; #48:1 Katika Kiebrania ni ‘maji a Yuda’.]

2Maana hujiita wenyeji wa mji mtakatifu, hujitegemeza juu ya Mungu wa Israeli; BWANA wa majeshi ni jina lake.[#Mik 3:11; Rum 2:17]

3Mimi nimehubiri mambo ya kale tangu zamani; naam, yalitoka katika kinywa changu, nikayadhihirisha; niliyatenda kwa ghafla, yakatokea.[#Yos 21:45]

4Kwa sababu nilijua ya kuwa wewe u mkaidi, na shingo yako ni shingo ya chuma, na kipaji cha uso wako ni shaba;[#Kut 32:9; Kum 31:27]

5basi nimekuonesha tangu zamani; kabla hayajatukia nilikuonesha; usije ukasema, Sanamu yangu imetenda haya; sanamu yangu ya kuchonga, na sanamu yangu ya kuyeyusha, imeyaamuru.

6Umesikia haya; tazama haya yote; nanyi, je! Hamtayahubiri? Nimekuonesha mambo mapya tangu wakati huu, naam, mambo yaliyofichwa, usiyoyajua.

7Yameumbwa sasa, wala si tokea zamani; na kabla ya siku hii ya leo hukusikia habari yake; usije ukasema, Tazama, niliyajua.

8Naam, hukusikia; naam, hukujua; naam, tokea zamani sikio lako halikuzibuka; maana nilijua ya kuwa wewe watenda kwa hila nyingi, nawe umeitwa mkosaji tangu kuzaliwa kwako;[#Zab 58:3]

9kwa ajili ya jina langu nitaahirisha hasira yangu, na kwa ajili yako nitajizuia, ili nisifiwe, wala nisikukatilie mbali.[#Yos 7:9; Zab 106:8]

10Tazama, nimekusafisha, lakini si kama fedha; nimekuchagua katika tanuri ya mateso.[#Zab 66:10; Isa 1:25; Mal 3:3]

11Kwa ajili ya nafsi yangu, kwa ajili ya nafsi yangu, nitatenda haya; je! Litiwe unajisi jina langu? Wala sitampa mwingine utukufu wangu.[#Kum 32:26; Isa 42:8]

12Nisikilize mimi, Ee Yakobo; na Israeli, niliyekuita; mimi ndiye. Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho pia.[#Kum 32:39; Isa 44:6; Ufu 1:17; 22:13]

13Naam, mkono wangu umeuweka msingi wa dunia, na mkono wangu wa kulia umezitanda mbingu; niziitapo husimama pamoja.[#Zab 102:25]

14Kusanyikeni, ninyi nyote, mkasikie; ni nani miongoni mwao aliyehubiri haya? BWANA amempenda; atatimiza mapenzi yake juu ya Babeli, na mkono wake utakuwa juu ya Wakaldayo.

15Mimi, naam, mimi, nimenena; naam, nimemwita; nimemleta, naye ataifanikisha njia yake.

16Nikaribieni, sikieni haya; tokea mwanzo sikunena kwa siri; tangu yalipokuwapo, mimi nipo; na sasa Bwana MUNGU amenituma, na roho yake.[#Zek 2:8,9]

17BWANA, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.[#Zab 32:8]

18Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari;[#Kum 5:29; Zab 81:13]

19Tena wazao wako wangalikuwa kama mchanga, na hao waliotoka katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingalikatika, wala kufutwa mbele zangu.[#Mwa 22:17; Hos 1:10]

20Haya, tokeni katika Babeli,[#Zek 2:6,7; Kut 19:4; Ufu 18:4]

Kimbieni kutoka kwa Wakaldayo;

Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya,

Yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni,

BWANA amemkomboa mtumishi wake, Yakobo.

21Wala hawakuona kiu alipowaongoza jangwani;[#Hes 20:11; Neh 9:15; Zab 105:41; Isa 48:21; 1 Kor 10:4]

Alitoa maji katika mwamba kwa ajili yao;

Pia akaupasua mwamba, maji yakatoka kwa nguvu.

22Hapana amani kwa waovu, asema BWANA.[#Isa 57:21]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya