The chat will start when you send the first message.
1Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta?[#1 Kor 1:18; Yn 12:38; Rum 10:16]
Na mkono wa BWANA amefunuliwa nani?
2Maana alikuwa mbele zake kama mche mwororo,[#Mk 9:12]
Na kama mzizi katika nchi kavu;
Yeye hana umbo wala uzuri;
Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.
3Alidharauliwa na kukataliwa na watu;[#Zab 22:6; Ebr 4:15; Yn 1:10]
Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko;
Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,
Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.
4Hakika ameyachukua masikitiko yetu,[#Mt 8:17; 26:66; 1 Pet 2:24]
Amejitwika huzuni zetu;
Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa,
Amepigwa na Mungu, na kuteswa.
5Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,[#1 Pet 2:24]
Alichubuliwa kwa maovu yetu;
Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake,
Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
6Sisi sote kama kondoo tumepotea;[#1 Pet 2:25]
Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe;
Na BWANA ameweka juu yake
Maovu yetu sisi sote.
7Alionewa, lakini alinyenyekea,[#Mdo 8:32; 1 Pet 1:19; Ufu 5:6]
Wala hakufunua kinywa chake;
Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni,
Na kama vile kondoo anyamazavyo
Mbele yao wakatao manyoya yake;
Naam, hakufunua kinywa chake.
8Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa;[#Dan 9:26]
Na maisha yake ni nani angeyajali?
Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai;
Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.
9Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya;[#Mt 27:57; 1 Pet 2:22]
Na pamoja na matajiri katika kufa kwake;
Ingawa hakutenda jeuri,
Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.
10Lakini BWANA aliridhika kumchubua;[#2 Kor 5:21; Gal 3:13; Rum 6:9; Efe 1:5]
Amemhuzunisha;
Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi,
Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi,
Na mapenzi ya BWANA yatafanikiwa mkononi mwake;
11Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika.[#Yn 17:3; 1 Yoh 2:1; Rum 5:18]
Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki
Atawafanya wengi kuwa wenye haki;
Naye atayachukua maovu yao.
12Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu,[#Flp 2:9; Kol 2:15; Mk 15:28; Lk 22:37; 23:34]
Naye atagawana nyara pamoja nao walio hodari;
Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa,
Akahesabiwa pamoja na hao wakosao.
Walakini alichukua dhambi za watu wengi,
Na kuwaombea wakosaji.