Waamuzi 17

Waamuzi 17

Mika na Mlawi

1Wakati huo alikuwako mtu mmoja wa nchi ya vilima ya Efraimu, aliyeitwa Mika.

2Naye akamwambia mama yake, Hizo fedha elfu na mia moja ulizoibiwa, na kuweka laana kwa ajili yake na kusema masikioni mwangu, tazama, ninazo mimi hizo fedha; ni mimi niliyezitwaa. Mama yake akasema, Mwanangu na abarikiwe na BWANA.[#Mwa 14:19; Rut 2:20; 3:10; 2 Sam 2:5]

3Basi akamrudishia mama yake hizo fedha elfu na mia moja. Mama yake akasema, Mimi naziweka fedha hizi kabisa ziwe wakfu kwa BWANA, zitoke mkononi mwangu kwa ajili ya mwanangu, ili kufanya sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu; basi kwa hiyo nakurudishia wewe.[#Kut 20:4,23; Law 19:4; Kum 12:30; Zab 115:4-8]

4Basi hapo alipomrudishia mama yake hizo fedha, mama yake akatwaa fedha mia mbili, akampa fundi mwenye kusubu fedha, naye akafanya sanamu ya kuchonga kwazo, na sanamu ya kusubu; ambazo zilikuwa ndani ya nyumba ya Mika.[#Isa 46:6]

5Basi mtu huyo Mika alikuwa na nyumba ya miungu, naye akafanya naivera, na kinyago, akamweka wakfu mmoja miongoni mwa wanawe, akawa kuhani wake.[#Kut 28:4-15; Amu 8:27; 18:14; 1 Sam 23:6; Mwa 31:19; Hos 3:4]

6Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; kila mtu alifanya hayo aliyoyaona kuwa ni mema machoni pake mwenyewe.[#Amu 21:25; 18:1; 19:1; Kum 33:5; 12:8]

7Alikuwako mtu kijana mmoja mwanamume aliyetoka Bethlehemu-yuda, wa jamaa ya Yuda, aliyekuwa Mlawi, naye akakaa huko kama mgeni.[#Yos 19:15; Amu 19:1; Rut 1:1,2; Mik 5:2; Mt 2:1,5,6]

8Mtu huyo akatoka katika huo mji, Bethlehemu-yuda, ili aende kukaa kama mgeni hapo atakapoona mahali; akafikia nchi ya vilima vilima ya Efraimu katika safari yake, hadi nyumba ya huyo Mika.

9Mika akamuuliza, “Umetoka wapi?” Akamwambia, Mimi ni Mlawi wa Bethlehemu-yuda, nami naenda kukaa popote nitakapoona mahali.

10Mika akamwambia, kaa pamoja nami, uwe kwangu baba, tena kuhani, nami nitakupa fedha kumi kila mwaka, na nguo ya kuvaa, na vyakula. Basi huyo Mlawi akaingia ndani.[#Mwa 45:8; Amu 18:19; Ayu 29:16; Isa 22:21; Mwa 45:8]

11Huyo Mlawi aliridhika kukaa na mtu huyo; kisha huyo kijana akawa kwake kama wanawe mmojawapo.

12Basi Mika akamweka wakfu huyo Mlawi, huyo kijana, naye akawa kuhani wake, akakaa nyumbani mwa Mika.

13Ndipo Mika akasema, Sasa ninajua ya kwamba BWANA atanitendea mema, kwa kuwa nina Mlawi kama kuhani wangu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya