The chat will start when you send the first message.
1Jinsi mji huu ukaavyo ukiwa,[#Isa 47:7; Omb 1:9; Ezr 4:20]
Huo uliokuwa umejaa watu!
Jinsi alivyokuwa kama mjane,
Yeye aliyekuwa mkuu kati ya mataifa!
Binti mfalme kati ya majimbo,
Jinsi alivyoshikwa shokoa!
2Hulia sana wakati wa usiku,[#Yer 13:17; Omb 1:16; Ayu 7:3; Zab 6:6; Yer 4:30]
Na machozi yake yapo mashavuni;
Miongoni mwa wote waliompenda
Hakuna hata mmoja amfarijiye;
Rafiki zake wote wamemtenda hila,
Wamekuwa adui zake.
3Yuda amehamishwa kwa sababu ya kuonewa,[#Law 26:14,32,33; Kum 28:64]
Na kwa sababu ya utumwa mkuu;
Anakaa kati ya mataifa,
Haoni raha yoyote;
Wote waliomfuata wamempata
Katika dhiki yake.
4Njia za Sayuni zaomboleza,
Kwa kuwa hakuna ajaye kwa sikukuu;
Malango yake yote yamekuwa ukiwa,
Makuhani wake hupiga kite;
Wanawali wake wanahuzunika;
Na yeye mwenyewe huona uchungu.
5Watesi wake wamekuwa kichwa,[#Yer 30:14; Omb 3:39]
Adui zake hufanikiwa;
Kwa kuwa BWANA amemtesa
Kwa sababu ya wingi wa makosa yake;
Watoto wake wadogo wamechukuliwa mateka
Mbele yake huyo mtesi.
6Naye huyo binti Sayuni
Enzi yake yote imemwacha;
Wakuu wake wamekuwa kama ayala
Wasioona malisho;
Nao wamekwenda zao hawana nguvu
Mbele yake anayewafuatia.
7Siku za mateso na misiba yake,[#Mik 4:11]
Yerusalemu huyakumbuka matamanio yake yote
Yaliyokuwa tangu siku za kale;
Hapo watu wake walipoanguka mikononi mwa mtesi,
Wala hakuna hata mmoja wa kumsaidia;
Hao watesi wake walimwona,
Wakafanya sabato zake kuwa mzaha.
8Yerusalemu amefanya dhambi sana;[#Yer 13:22]
Kwa hiyo amekuwa kama kitu kichafu;
Wote waliomheshimu wanamdharau,
Kwa sababu wameuona uchi wake;
Naam, yeye anaugua,
Na kujigeuza aende nyuma.
9Uchafu wake ulikuwa katika marinda yake;[#Kum 32:29]
Hakukumbuka mwisho wake;
Kwa hiyo ameshuka kwa ajabu;
Yeye hana mtu wa kumfariji;
Tazama, BWANA, mateso yangu;
Maana huyo adui amejitukuza.
10Huyo mtesi amenyosha mkono wake[#Kum 23:3; Neh 13:1]
Juu ya matamanio yake yote;
Maana ameona ya kuwa mataifa wameingia
Ndani ya patakatifu pake;
Ambao kwa habari zao wewe uliamuru
Wasiingie katika kusanyiko lako.
11Watu wake wote hupiga kite,[#Yer 38:9]
Wanatafuta chakula;
Wameyatoa matamanio yao wapate chakula
Cha kuihuisha nafsi;
Ee BWANA, tazama, uangalie;
Kwa maana mimi nimekuwa mnyonge.
12Je! Si kitu kwenu, enyi nyote mpitao njia,[#Dan 9:12; Mt 24:21; Lk 21:22]
Angalieni, mtazame
Kama kuna majonzi yoyote mfano wa majonzi yangu,
Niliyotendwa mimi,
Ambayo BWANA amenihuzunisha kwa hayo
Siku ya hasira yake iwakayo.
13Toka juu amepeleka moto mifupani mwangu,[#Ayu 18:8; Zab 66:11; Eze 12:13; Hos 7:12]
Nao umeishinda;
Ametandika wavu aninase miguu,
Amenirudisha nyuma;
Amenifanya kuwa mtu wa pekee,
Na mgonjwa mchana kutwa.
14Kongwa la makosa yangu limefungwa na mkono wake;[#Kum 28:48; Mit 5:22; Isa 14:25; Mt 11:29,30]
Hayo yameshikamana;
Yamepanda juu shingoni mwangu;
Amezikomesha nguvu zangu;
15Bwana amenitia mikononi mwao,[#Isa 63:3; Ufu 14:19]
Ambao siwezi kupingamana nao.
Bwana amewafanya mashujaa wangu wote
Kuwa si kitu kati yangu;
Ameita mkutano mkuu kinyume changu
Ili kuwaponda vijana wangu;
Bwana amemkanyaga kama shinikizoni
Huyo bikira binti Yuda.
16Mimi ninayalilia mambo hayo;
Jicho langu, jicho langu linachuruzika machozi;
Kwa kuwa mfariji yuko mbali nami,
Ambaye ilimpasa kunihuisha nafsi;
Watoto wangu wameachwa peke yao,
Kwa sababu huyo adui ameshinda.
17Sayuni huinyosha mikono yake;
Hakuna hata mmoja wa kumfariji;
BWANA ametoa amri juu ya Yakobo,
Kwamba wamzungukao wawe watesi wake;
Yerusalemu amekuwa kati yao
Kama kitu kichafu.
18BWANA ndiye mwenye haki;[#Neh 9:33; Dan 9:7; 1 Sam 12:14]
Maana nimeiasi amri yake;
Sikieni, nawasihi, enyi watu wote,
Mkayatazame majonzi yangu;
Wasichana wangu na wavulana wangu
Wamechukuliwa mateka.
19Niliwaita hao walionipenda
Lakini walinidanganya;
Makuhani wangu na wazee wangu
Walifariki mjini;
Hapo walipokuwa wakitafuta chakula
ili kuzihuisha nafsi zao.
20Angalia, Ee BWANA; maana mimi ni katika dhiki;[#Isa 16:11; Yer 4:19; Hos 11:8; Kum 32:25]
Mtima wangu umetaabika;
Moyo wangu umegeuka ndani yangu;
Maana nimeasi vibaya sana;
Huko nje upanga huua watu;
Nyumbani mna kama mauti.
21Wamesikia kwamba napiga kite;[#Yer 46:1]
Hakuna hata mmoja wa kunifariji;
Adui zangu wote wamesikia habari ya mashaka yaliyonipata;
Hufurahi kwa kuwa umeyafanya hayo;
Utaileta siku ile uliyoitangaza,
Nao watakuwa kama mimi.
22Huo uovu wao wote
Na uje mbele zako wewe;
Ukawatende wao kama ulivyonitenda mimi
Kwa dhambi zangu zote;
Kwa maana mauguzi yangu ni mengi sana,
Na moyo wangu umezimia.