The chat will start when you send the first message.
1BWANA akanena na Musa, akamwambia,
2Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wenu, ni mtakatifu.[#Law 11:44-45; 20:7,26; 1 Pet 1:16; Kut 19:6; Efe 1:4; 1 The 4:7]
3Kila mtu na amche mama yake, na baba yake, nanyi mtazitunza Sabato zangu; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.[#Kut 20:8,12; 31:13; Kum 5:12,16; Mwa 2:2; Neh 9:14; 13:15-21; Isa 56:2; 58:13; Mk 2:27; Ebr 4:9]
4Msigeuke kufuata sanamu, wala msijitengenezee miungu ya kusubu mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.[#Law 26:1; Kut 20:3-5,23; 34:17; Kum 27:15; 1 Kor 10:14]
5Nanyi hapo mtakapomchinjia BWANA sadaka ya amani mtaitoa kwa njia ipasayo ili mpate kukubaliwa.
6Italiwa siku iyo hiyo mliyoichinja, na siku ya pili yake; na kama kitu chochote katika sadaka hiyo kilisalia hata siku ya tatu kitachomwa moto.
7Ikiwa sadaka hiyo inaliwa hata kidogo siku ya tatu ni machukizo; haitakubaliwa;
8lakini kila mtu atakayekula atalipizwa uovu wake mwenyewe, kwa sababu amekinajisi kitu hicho kitakatifu cha BWANA; na mtu huyo atatengwa na watu wake.
9Na mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa katika pembe za shamba lako, wala usiyakusanye masazo ya mavuno yako;[#Law 23:22; Kum 15:1-18; 24:19-22; Kut 23:11; Rut 2:15]
10wala usiyakusanye masazo ya mizabibu yako, wala usiyaokote matunda ya mizabibu yako yaliyopukutika; uyaache kwa ajili ya maskini na mgeni; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.[#Zab 41:1; 140:12; Mit 14:31; 22:16; Mhu 5:8; Isa 3:12-15; Yak 2:1-9]
11Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane uongo.[#Kut 20:15,16; Kum 5:19,20; 1 Fal 13:18; Yer 9:3-5; Mdo 5:3,4; Efe 4:25]
12Msiape uongo kwa jina langu, na ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi BWANA.[#Kut 20:7; Kum 5:11; Mt 5:33]
13Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang'anya mali yake; ujira wake aliyeajiriwa usikae kwako usiku kucha hadi asubuhi.[#Kum 24:14-15; Mal 3:5; Yak 5:4]
14Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi BWANA.[#Kum 27:18; Rum 14:13; 1 Pet 2:17]
15Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki.[#Kut 23:6-8; Kum 16:19; Zab 82:2; Mit 24:23; Yak 2:9]
16Usiende huku na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usijifaidi kwa damu ya jirani yako; mimi ndimi BWANA.[#1 Fal 21:13; Mt 26:60; #19:16 Katika Kiebrania ni ‘kuwa kinyume cha damu’.]
17Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, au ulipizwe uovu kwa ajili yake[#Mt 18:15; Mwa 27:41; 1 Yoh 2:9,11; 3:15; Lk 17:3]
18Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA.[#Mt 5:43,44; 19:19; 22:39; Mk 12:31; Lk 10:27; Rum 13:9; 12:17; Gal 5:4; Yak 2:8]
19Mtazishika amri zangu. Usiwaache wanyama wako wa mfugo wakazaana kwa namna mbalimbali; usipande shamba lako mbegu za namna mbili pamoja; wala usivae mwilini mwako nguo ya namna mbili zilizochanganywa pamoja.[#Kum 22:9-11]
20Tena mtu yeyote alalaye na mwanamke aliye mjakazi, naye ameposwa na mwanamume mwingine, wala hakukombolewa kwa lolote, wala hakupewa uhuru wake; watachunguzwa; hawatauawa, kwa sababu huyo mwanamke hakuwa huru.
21Na huyo mwanamume ataleta sadaka yake ya hatia aitoe kwa BWANA, hata mlangoni pa hema ya kukutania; kondoo dume kwa hiyo sadaka ya hatia.
22Kisha huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa huyo kondoo dume wa sadaka ya hatia mbele za BWANA, kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya; naye atasamehewa hiyo dhambi yake aliyoifanya.
23Nanyi mtakapoingia katika nchi ile, na kupanda miti ya namna zote kwa ajili ya chakula, ndipo mtayahesabu matunda yake kama yaliyotakazwa; kwa muda wa miaka mitatu miti hiyo itakuwa kwenu kama katazo; matunda yake hayataliwa.[#19:23 Katika Kiebrania ni ‘kama kutotahiriwa kwao’.]
24Lakini mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa ni matakatifu, kwa ajili ya kumpa BWANA shukrani.[#Kum 12:17,18]
25Na katika mwaka wa tano mtakula matunda yake, ili ipate kuwapa mavuno yake; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.
26Msile kitu chochote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi.[#Mwa 9:4; Law 7:26-27; 17:10-14; Kum 12:16,23; 15:23; 18:10; 2 Fal 17:17]
27Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu.[#Law 21:5; Kum 14:1; Yer 9:26]
28Msichanje chale yoyote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA.[#Kum 14:1]
29Usimnajisi binti yako, ili kumfanya awe kahaba; isiwe hiyo nchi kuuandama ukahaba, na nchi kujawa na uovu mkuu.[#Kum 23:17]
30Zishikeni Sabato zangu, mpaheshimu patakatifu pangu; mimi ndimi BWANA.[#Law 26:2; Mhu 5:1]
31Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.[#Kum 18:11; 1 Sam 28:3; 2 Fal 23:4; Isa 8:19]
32Mwondokeeni mtu mwenye mvi; heshimuni uso wa mtu mzee; nawe mche Mungu wako, Mimi ndimi BWANA.[#1 Fal 2:19; Mit 20:29; 23:22; 1 Tim 5:1]
33Na mgeni akikaa pamoja nawe katika nchi yako, usimdhulumu.[#Kut 22:21; Kum 24:17-18; 27:19]
34Mgeni aishiye pamoja nawe atakuwa kama mzaliwa kwenu; mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.[#Kut 12:48; Kum 10:19]
35Msifanye yasiyo haki katika hukumu, wala katika kupima, wala katika mizani, wala katika cheo.[#Kum 25:13-16; Mit 20:10; Eze 45:10]
36Mizani ya haki, vipimo vya haki, efa ya haki, hini ya haki, ndivyo mtakavyokuwa navyo. Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri.[#Kum 25:13,15; Mit 20:10]
37Zishikeni sheria zangu, na hukumu zangu, na kuzitenda. Mimi ndimi BWANA.[#Kum 6:25; 5:1; Law 18:4,5]