Luka 1

Luka 1

1Kwa kuwa watu wengi wameweza kuandika kwa utaratibu habari za mambo yaliyotimizwa katikati yetu,

2kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo,[#Yn 15:27]

3nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu,[#Mdo 1:1]

4upate kujua hakika ya mambo yale uliyofundishwa.

Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji kwatabiriwa

5Zamani za Herode, mfalme wa Yudea, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa kikundi cha ukuhani cha Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti.[#1 Nya 24:10]

6Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiishi katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.

7Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana.

8Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani wakati wa zamu yake mbele za Mungu,

9kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba.[#Kut 30:7]

10Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba.

11Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia.

12Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.

13Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto wa kiume, na jina lake utamwita Yohana.

14Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake.

15Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye.[#Hes 6:3; Amu 13:4,5; 1 Sam 1:11]

16Na wengi katika Waisraeli atawarejesha kwa Bwana Mungu wao.

17Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotayarishwa.[#Mal 3:1; 4:5-6; Mt 17:11-13]

18Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi.[#Mwa 18:11]

19Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema.[#Dan 8:16; 9:21; Ebr 1:14]

20Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake.[#Lk 1:45]

21Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni.

22Alipotoka akiwa hawezi kusema nao, walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwaashiria akakaa bubu.

23Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake.

24Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema,

25Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.[#Mwa 30:23]

Kuzaliwa kwa Yesu kwatabiriwa

26Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka katika mji wa Galilaya, jina lake Nazareti,

27kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa ukoo wa Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu.[#Mt 1:16,18; Lk 2:5]

28Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe.[#Amu 5:24]

29Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?

30Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu.

31Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume; na jina lake utamwita Yesu.[#Mt 1:21-23; Amu 13:3; Isa 7:14]

32Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye Juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.[#2 Sam 7:12,13,16; Isa 9:7]

33Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.[#Mik 4:7; Dan 7:14]

34Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?

35Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujia juu yako, na nguvu zake Aliye Juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.[#Kut 13:12; Mt 1:18,20]

36Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto wa kiume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa;

37kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.[#Mwa 18:14]

38Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.

Mariamu Amtembelea Elisabeti

39Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hadi katika nchi yenye milima kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yudea,

40akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti.

41Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu;[#Lk 1:15; Mwa 25:22]

42akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa.[#Kum 28:9; Amu 5:24]

43Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijie mimi?

44Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu.

45Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.[#Lk 1:20; 11:28]

Wimbo wa Sifa wa Mariamu

46Mariamu akasema,[#1 Sam 2:1-10]

Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,

47Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu;

48Kwa kuwa ameutazama[#1 Sam 1:11; Lk 1:25; Zab 113:5,6; Lk 11:27]

Unyonge wa mjakazi wake.

Kwa maana, tazama, tokea sasa

Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;

49Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu,[#Zab 111:9]

Na jina lake ni takatifu.

50Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi[#Zab 103:13,17]

Kwa hao wanaomcha.

51Amefanya nguvu kwa mkono wake;[#Zab 89:10; 2 Sam 22:28]

Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

52Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi;[#Ayu 5:11; 12:19; Zab 147:6; 1 Sam 2:7]

Na wanyonge amewainua.

53Wenye njaa amewashibisha mema,[#1 Sam 2:5; Zab 34:10; 107:9]

Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu.

54Amemsaidia Israeli, mtumishi wake;[#Isa 41:8; Zab 98:3]

Ili kukumbuka rehema zake;

55Kama alivyowaambia baba zetu,[#Mwa 17:7; 18:18; 22:17; Mik 7:20]

Abrahamu na uzao wake hata milele.

56Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.

Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji

57Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume.

58Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye.

59Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria.[#Law 12:3; Mwa 17:12]

60Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana.[#Lk 1:13]

61Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo.

62Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita.

63Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote.

64Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu.

65Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya Yudea yenye milima.

66Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.

Unabii wa Zekaria

67Na Zakaria, baba yake, akajazwa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema,

68Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,[#Lk 7:16; Zab 41:13; 72:18]

Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa.

69Ametusimamishia pembe ya wokovu[#1 Sam 2:10; Zab 18:2; 132:17]

Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake.

70Kama alivyosema tangu mwanzo

Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu;

71Tuokolewe na adui zetu[#Zab 106:10]

Na mikononi mwao wote wanaotuchukia;

72Ili kuwatendea rehema baba zetu,[#Zab 105:8; 106:45; Mwa 17:7; Law 26:42]

Na kulikumbuka agano lake takatifu;

73Kiapo alichomwapia Abrahamu, baba yetu,[#Mwa 22:16,17; Mik 7:20]

74Ya kwamba atatujalia sisi,[#Tit 2:12,14]

Tuokoke mikononi mwa adui zetu,

Na kumwabudu pasipo hofu,

75Kwa utakatifu na kwa haki

Mbele zake siku zetu zote.

76Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye Juu,[#Mal 3:1; Mt 3:3]

Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake;

77Uwajulishe watu wake wokovu,[#Yer 31:34]

Kwa kusamehewa dhambi zao.

78Kwa njia ya rehema za Mungu wetu,[#Hes 24:17; Isa 60:1,2; Mal 4:2]

Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia,

79Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti,[#Isa 9:2; 58:8; Mt 4:16]

Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.

80Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hadi siku ile alipotokeza hadharani kwa Israeli.[#Mt 3:1]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya