Zaburi 62

Zaburi 62

Wimbo wa kusifia imani kwa Mungu pekee

1Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa utulivu,

Wokovu wangu hutoka kwake.

2Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu,

Ngome yangu, sitatikisika.

3Hadi lini mtamshambulia mtu,[#Isa 30:13]

Mpate kumwua ninyi nyote pamoja?

Kama ukuta unaoinama,

Kama ua ulio tayari kuanguka,

4Mpango wao ni kumwangusha tu mtu mwenye cheo;[#Zab 28:3]

Huufurahia uongo.

Kwa kinywa chao hubariki;

Kwa moyo wao hulaani.

5Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa utulivu.[#Mik 7:7,10]

Maana tumaini langu hutoka kwake.

6Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu,

Ngome yangu, sitatikisika.

7Kwa Mungu wokovu wangu,[#Yer 3:23]

Na utukufu wangu;

Mwamba wa nguvu zangu,

Na kimbilio langu ni kwa Mungu.

8Enyi watu, mtumainini sikuzote,[#1 Sam 1:15; Zab 42:4]

Ifunueni mioyo yenu mbele zake;

Mungu ndiye kimbilio letu.

9Hakika binadamu ni ubatili,

Na wenye cheo ni uongo,

Katika mizani huinuka;

Wote pamoja ni hafifu kuliko ubatili.

10Msiitumainie dhuluma,[#Isa 26:4; Mk 10:23; Lk 12:15]

Wala msijivune kwa unyang'anyi;

Mali izidipo msiiangalie sana moyoni.

11Mara moja amenena Mungu;

Mara mbili nimeyasikia haya,

Ya kuwa nguvu zina Mungu,

12Na fadhili ziko kwako, Ee Bwana;[#Ayu 34:11; Yer 17:10; Mt 16:27; 1 Pet 1:17; Rum 2:6; Ufu 2:23]

Maana ndiwe umlipaye kila mtu

Kulingana na haki yake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya