Zaburi 69

Zaburi 69

Sala ya ukombozi katika mateso

1Ee Mungu, uniokoe,

Maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu.

2Ninazama katika matope mengi,

Pasipowezekana kusimama.

Nimefika penye maji ya vilindi,

Mkondo wa maji unanigharikisha.

3Nimechoka kwa kulia kwangu,

Koo yangu imekauka.

Macho yangu yamedhoofika

Kwa kumngoja Mungu wangu.

4Wanaonichukia bure ni wengi[#Zab 35:19; Yn 15:25]

Kuliko nywele za kichwa changu.

Watakao kunikatilia mbali ni wengi,

Adui zangu kwa sababu isiyo kweli.

Hata mimi nililipishwa kwa nguvu

Vitu nisivyovichukua.

5Ee Mungu, unajua upumbavu wangu,

Wala hukufichwa dhambi yangu.

6Wanaokungoja Wewe wasiaibishwe,

Kwa ajili yangu, Bwana, MUNGU wa majeshi.

Wanaokutafuta Wewe wasifedheheshwe,

Kwa ajili yangu, Ee Mungu wa Israeli.

7Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu,

Fedheha imenifunika uso wangu.

8Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,[#Isa 53:3; Yn 1:11]

Na asiyetambuliwa na wana wa mama yangu.

9Maana mvuto wa nyumba yako umenila,[#1 Fal 19:10; Zab 119:139; Yn 2:17; Rum 15:3]

Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata.

10Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga,

Nikalaumiwa kwa hayo.

11Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu,[#1 Fal 9:7; Yer 24:9; Zab 44:13,14]

Nikawa kifani cha dharau kwao.

12Waketio langoni hunisema,[#Ayu 17:6; Omb 3:14]

Na nyimbo za walevi hunidhihaki.

13Nami maombi yangu nakuomba Wewe, BWANA,[#Isa 49:8; 2 Kor 6:2]

Wakati ukupendezao; Ee Mungu,

Kwa wingi wa fadhili zako unijibu,

Katika kweli ya wokovu wako.

14Uniponye kwa kunitoa matopeni,

Wala usiniache nikazama.

Na niponywe kutoka kwa wanaonichukia,

Na kutoka katika vilindi vya maji.

15Mkondo usinigharikishe, wala vilindi visinimeze,

Wala Shimo lisifumbe kinywa chake juu yangu.

16Ee BWANA, unijibu, maana fadhili zako ni njema,

Kwa kadiri ya rehema zako unielekee.

17Wala usinifiche uso wako, mimi mtumishi wako,

Maana mimi nimo taabuni, unijibu upesi.

18Uikaribie nafsi yangu, uikomboe,

Kwa sababu ya adui zangu unifidie.

19Wewe umejua kulaumiwa kwangu,[#Zab 22:6; Isa 53:3; Ebr 12:2]

Na kuaibika na kufedheheka kwangu,

Mbele zako Wewe wako watesi wangu wote.

20Laumu imenivunja moyo,

Nami ninaugua sana.

Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna;

Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu.

21Wakanipa uchungu kuwa chakula changu;[#Mt 27:34; Mt 27:48; Mk 15:36; Lk 23:36; Yn 19:28-29]

Na nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki.

22Meza yao mbele yao na iwe mtego;[#Rum 11:9-10; 2 Kor 3:14]

Naam, sikukuu zao sadaka ziwanase.

23Macho yao yatiwe giza wasione,

Na viuno vyao uvitetemeshe daima.

24Uimwage ghadhabu yako juu yao,

Na ukali wa hasira yako uwapate.

25Makambi yao na yawe ukiwa,[#Mdo 1:20]

Pasiwe na mtu wa kukaa hemani mwao.

26Maana wanamwudhi mtu uliyempiga Wewe,[#Isa 53:4]

Wanazidisha maumivu ya hao uliowatia jeraha.

27Uwaongezee uovu juu ya uovu,[#Rum 9:31]

Wala wasipate msamaha kutoka kwako.

28Na wafutwe katika kitabu cha uhai,[#Kut 32:32; Eze 13:9; Lk 10:20; Flp 4:3; Ebr 12:23; Ufu 3:5; 13:8; 17:8]

Wala pamoja na wenye haki wasiandikwe.

29Nami niliye maskini na mtu wa huzuni,

Mungu, wokovu wako utaniinua.

30Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,

Nami nitamtukuza kwa shukrani.

31Nayo yatampendeza BWANA kuliko ng'ombe,

Au ndama mwenye pembe na kwato.

32Walioonewa watakapoona watafurahi;

Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.

33Kwa kuwa BWANA huwasikia wahitaji,

Wala hawadharau wafungwa wake.

34Mbingu na nchi zimsifu,

Bahari na vyote viendavyo ndani yake.

35Maana Mungu ataiokoa Sayuni, na kuijenga miji ya Yuda,[#Zab 57:1-3; 102:13,16; Isa 14:32; 44:26]

Na watu watakaa ndani yake na kuimiliki.

36Wazawa wa watumishi wake watairithi,

Nao walipendao jina lake watakaa humo.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya