Zaburi 80

Zaburi 80

Sala ya kurejeshwa kwa Israeli

1Wewe uchungaye Israeli, usikie,[#Kut 25:22; Kum 33:2; 1 Sam 4:4; Zab 89:1]

Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi;

Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.

2Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na Manase,

Uziamshe nguvu zako,

Uje, utuokoe.

3Ee Mungu, uturudishe,[#1 Fal 18:37]

Uangaze uso wako nasi tutaokoka.

4Ee BWANA, Mungu wa majeshi, hadi lini

Utayaghadhibikia maombi ya watu wako?

5Umewalisha mkate wa machozi,

Umewanywesha machozi kwa kipimo kikuu.

6Unatufanya sababu ya ugomvi kwa jirani zetu,

Na adui zetu wanacheka wao kwa wao.

7Ee Mungu wa majeshi, uturudishe,

Uangaze uso wako nasi tutaokoka.

8Ulileta mzabibu kutoka Misri,[#Isa 5:1,7; Yer 2:21; Eze 15:6]

Ukawafukuza mataifa ukaupanda.

9Ulitengeneza nafasi mbele yake,

Nao ukatia mizizi sana ukaijaza nchi.

10Milima ilifunikwa kwa kivuli chake,

Matawi yake ni kama mierezi ya Mungu.

11Nao uliyaeneza matawi yake hadi baharini,[#Kut 23:31; Zab 72:8]

Na vichipukizi vyake hadi kunako Mto.

12Kwa nini umezibomoa kuta zake,[#Isa 5:5]

Wakauchuma wote wapitao njiani?

13Nguruwe wa msituni wanauharibu,

Na hayawani wa kondeni wanautafuna.

14Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,[#Zek 1:12,16,17; Isa 63:15]

Utazame toka juu uone, uujie mzabibu huu.

15Na mche ule ulioupanda[#Isa 49:5]

Kwa mkono wako wa kulia;

Na tawi lile ulilolifanya

Kuwa imara kwa nafsi yako.

16Umechomwa moto; umekatwa;

Kwa lawama ya uso wako wanapotea.

17Mkono wako na uwe juu yake[#Zab 89:21; Kut 4:22; Zab 110:1; Dan 7:13,14; Yn 5:21-27]

Mtu aliye katika mkono wako wa kulia;

Juu ya mwanadamu uliyeimarisha

Kwa nafsi yako;

18Kisha hatutakuacha kwa kurudi nyuma;

Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako.

19Ee BWANA, Mungu wa majeshi, uturudishe,[#Hes 6:25; Zab 27:4,9]

Uangaze uso wako nasi tutaokoka.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya