Sala ya Azaria 1

Sala ya Azaria 1

Sala ya Azaria tanurini

1Nao vijana walitembea katikati ya moto, wakimsifu Mungu na kumhimidi BWANA.[#Dan 3:23]

2Ndipo Azaria akasimama akasali hivi, akifumbua kinywa chake katikati ya moto na kusema:

3Umehimidiwa, Ee Bwana, MUNGU wa baba zetu, na jina lako lastahili kusifiwa na kutuzwa milele.

4Maana Wewe u mwenye haki katika mambo yote uliyoyafanya; naam, matendo yako ni kweli, na njia zako ni haki, na hukumu zako zote ni za adili.

5Katika mambo yote uliyoyaleta juu yetu, na juu ya Yerusalemu, mji mtakatifu wa baba zetu, umetekeleza hukumu za adili;

6maana kwa kweli na haki umeyaleta hayo yote juu yetu kwa sababu ya dhambi zetu, kwa kuwa sisi tumetenda dhambi na kufanya maovu kwa kukuacha Wewe.

7Katika yote tumekosa sana, wala hatukuzitii amri zako na kuzishika; wala hatukufanya kama ulivyotuamuru ili tupate kufanikiwa.

8Basi, yote uliyotuletea, na yote uliyotutendea, umeyatenda kwa haki.

9Ulitutia katika mikono ya adui zetu, wasio na sheria, makafiri wa kuchukiza; na katika mikono ya mfalme asiye haki, mwovu sana kupita wote wa ulimwengu.

10Sasa hatuwezi kuvifumbua vinywa vyetu aibu na mashutumu yametupata sisi watumishi wako na wote wakuabuduo.

11Usituache kabisa, kwa ajili ya jina lako, wala usilitangue agano lako na kutuondolea rehema zako,

12kwa ajili ya Abrahamu umpendaye, na kwa ajili ya Isaka mtumishi wako, na Israeli mtakatifu wako,

13ambao uliwaahidia ya kuwa utauzidisha uzao wao kama nyota za mbinguni na kama mchanga uliopo pwani.

14Maana sisi, Ee BWANA, tumekuwa duni kuliko mataifa mengine yote, na kudhulumiwa leo katika ulimwengu wote kwa sababu ya dhambi zetu.

15Sasa hakuna mfalme wala nabii wala kiongozi; hakuna dhabihu wala kafara wala sadaka wala uvumba; wala mahali pa kukutolea dhabihu na kuona rehema.

16Lakini kwa moyo uliovunjika na kwa roho nyenyekevu tukubaliwe nawe, na sadaka yetu iwe machoni pako leo kama dhabihu za kondoo dume na ng'ombe, na kama kondoo wanono elfu kumi.

17Nasi tukufuate kwa unyofu, maana wanaokutumaini Wewe hawataaibika.

18Na sasa tunakufuata kwa moyo wote; tunakucha, na kuutafuta uso wako.

19Usitufedheheshe, bali ututendee kwa kadiri ya fadhili zako, sawasawa na wingi wa huruma zako.

20Utuokoe kwa kadiri ya maajabu yako, na kulitukuza jina lako, Ee BWANA.

21Na waaibishwe wote wanaowaudhi watumishi wako; wafedheheke katika uwezo wao na ukuu wao.

22Nguvu zao zivunjike; nao wapate kujua ya kuwa Wewe ndiwe Bwana, MUNGU peke yako, mtukufu juu ya ulimwengu wote.

Wimbo wa Wayahudi Watatu

23Basi, watumishi wa mfalme waliowatupa ndani ya tanuri hawakulegea katika kuongeza moto kwa mafuta na lami na makumbi na kuni,

24hata mwako wa moto ukapanda juu ya tanuri kadiri ya dhiraa arubaini na tisa.

25Ukaenea, ukawateketeza wale Wakaldayo waliokuwa karibu na tanuri.

26Lakini malaika wa BWANA alishukia ndani ya tanuri pamoja na Azaria na wenzake, akaukumba mwako wa moto katika tanuri,[#Tob 5:4]

27akafanya katikati ya tanuri mfano wa upepo wa unyevu uvumao, hata moto haukuwagusa kamwe, wala kuwadhuru au kuwasumbua.

Wimbo wa vijana watatu

28Ndipo wale watatu, kama kwa kinywa kimoja, walimsifu Mungu na kumtukuza na kumhimidi, wakisema:

29Umehimidiwa. Ee Bwana, MUNGU wa baba zetu:

Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;

Lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

30Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

31Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako;

Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

32Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi;

Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

33Umehimidiwa katika anga la mbinguni

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

34Enyi viumbe vyote vya BWANA mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

35Malaika wa BWANA, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

36Enyi mbingu, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

37Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

38Nguvu zote za BWANA, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

39Jua na mwezi, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

40Nyota za mbinguni, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

41Manyunyu yote na ukungu, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

42Pepo zote, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

43Moto na hari, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele:

44Kipupwe na msimu, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

45Umande na sakitu, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

46Jaiidi na baridi, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

47Barafu na theluji, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

48Usiku na mchana, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

49Weupe na giza, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

50Umeme na mawingu, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

51Dunia na imhimidi BWANA;

Imsifu na kumwadhimisha milele.

52Milima na vilima, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

53Mimea yote ya nchi, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

54Chemchemi, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

55Bahari na mito, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele

56Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

57Ndege wote wa angani, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

58Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

59Wanadamu, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

60Mwana wa Israeli, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

61Makuhani wa BWANA, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

62Watumishi wa BWANA, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

63Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

64Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

65Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini BWANA;

Msifuni na kumwadhimisha milele.

Kwa maana anetuokoa katika ahera,

na kutuponya katika mikono ya mauti.

Ametuopoa katikati ya tanuri na moto uwakao,

naam, katikati ya moto ametuokoa.

66Mshukuruni BWANA, kwa kuwa yu mwema;

Kwa maana fadhili zake ni za milele.

67Enyi nyote mnaomwabudu BWANA, mhimidini Mungu wa miungu;

Msifuni na kumshukuru;

Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya