The chat will start when you send the first message.
1Ee BWANA, baba na Mungu wa uzima wangu,
Usinitupe katika mashauri ya adui,
Wala usiniache nianguke kwayo.
2Nani ataweka mijeledi mawazoni,
Na mchapo wa hekima moyoni mwangu?
Nisikose adhabu ya ujinga wangu,
Moyo wangu usiachilie dhambi.
3Ujinga wangu usizidi kuwa mwingi,
Wala dhambi zangu zisiongezeke;
Nisije nikaanguka mbele ya watesi,
Adui yangu asitukuke juu yangu.
4Ee BWANA, baba na Mungu wa uzima wangu,
Usinipe macho ya kiburi,
5Uiondoe tamaa mbali nami;
6Choyo na uzinzi yasinipate,
Wala moyo wenye tamaa mbaya usinisibu.
7Wanangu, sikilizeni utawala wa kinywa; aushikaye hatakamatwa.
8Mwenye dhambi katika midomo yake atapatwa, na mshutumu na mwenye kiburi atajikwaa.
9Usikizoeze kinywa chako kuapa, wala usifuate desturi ya kulitaja jina lake Mtakatifu.[#Mt 5:34; Yak 5:12]
10Yaani, mtumishi akichapwa daima hakosi kuchubuka; hivyo aapaye na kutamja Mungu daima hawezi kusafika dhambi.
11Mtu mwenye viapo vingi atajaa uovu; wala adhabu haitaondoka nyumbani mwake; akikosa dhambi yake itakuwa juu yake; akikosa kuiangalia ametenda dhambi maradufu; akiwa ameapa bure hatahakikishwa; kwa maana nyumba yake itajaa misiba.
12Kuna desturi ya mazungumzo inayolingana na kuapa; walakini isionekane katika urithi wa Yakobo; maana hayo yote yawe mbali na wenye haki, wasije wakagaagaa matopeni mwa dhambi.
13Usikizoeze kinywa chako kunena matusi, kwa maana ndani yake mna maneno ya dhambi.
14Kumbuka baba yako na mama yako, uketipo katika mkutano wa wakuu; usije ukawa msahaulifu mbele yao, ukawa mpumbavu kwa sababu ya desturi yako; mradi utataka kama usingalizaliwa, na kuilaani siku ya kuzaliwa kwako.
15Wala yeye aliyezoea usemi uliofedheheka hapati adabu siku zote za maisha yake.
16Watu wa namna mbili huzidisha dhambi,
Naye wa namna ya tatu ataleta ghadhabu;
17Mwenye unyege,
Na mwasherati,
Naye atembeaye mbali na kitanda chake.
Moto uwakao hautazimika hata ukome; wala mwasherati haachi hata moto umteketeze mwili na nyama. Mkate wa kila namna ni mtamu kwake, haachi mpaka kufa.
18Husema moyoni mwake, Nani anionaye? Giza limenizunguka, na kuta zimenificha, wala hakuna anionaye; nimwogope nani? Yeye Aliye Juu hatazikumbuka dhambi zangu,
19Basi, macho ya watu ndiyo hofu yake; wala hajui ya kuwa macho ya BWANA yang'aa kuliko jua mara elfu, yanatazama njia zote za wanadamu, yanachunguza mahali pa siri.
20Mambo yote yalijulikana naye kabla hayajaumbwa, na kadhalika baada ya kukamilika.
21Hakika mtu huyo ataadhibiwa katika njia za mjini; hata na mahali asipodhani atafumaniwa.
22Vivyo hivyo naye mke amwachaye mume wake, akaingiza mrithi kwa mgeni.
23Kwa maana kwanza, ameivunja sheria yake Aliye Juu; pili amemkosa mume wake mwenyewe; tatu, amejifanya mzinzi kwa ukahaba, na kuingiza watoto kwa mgeni.
24Huyo ataletwa mbele ya kusanyiko, na juu ya watoto wake kutakuwa maulizo.
25Watoto wake hawatatia mizizi, wala matawi yake hayatazaa matunda.
26Ataacha ukumbusho wake kuwa laana, wala fedheha yake haifutiki.
27Na watu watakaosalia watajua ya kwamba hakuna jema kuliko kumcha BWANA, wala hakuna tamu kuliko kuzishika amri zake.