Yoshua Mwana wa Sira 45

Yoshua Mwana wa Sira 45

Musa

1Musa alipendwa na Mungu na wanadamu; ambaye kumbukumbu lake lina baraka.[#Kut 6:28—11:10; 20:1-21]

2Alimfananisha na watakatifu kwa utukufu, akamwadhimisha hata adui zake wakamwogopa;

3na kwa maneno yake akayahimiza maajabu. Akamtukuza mbele ya mfalme, akampa amri mbele ya watu wake, akamwonesha kwa sehemu utukufu wake.

4Akamtakasa katika uaminifu wake na upole wake, akamchagua katika wote wenye mwili.

5Akamsikiza sauti yake, na kumwingiza katika wingu la giza; na kumpa amri uso kwa uso, ndiyo sheria ya uzima na maarifa; ili amfundishe Yakobo maagizo yake, na Israeli hukumu zake.

Haruni

6Haruni naye alimfanya kuwa mtukufu; ambaye alikuwa mtakatifu kama yule ndugu yake wa kabila ya Lawi.[#Kut 4:14]

7Akamsimamisha kwa agizo la milele, kwamba apewe heshima ya ukuhani; akampamba mapambo mazuri, akamvika vazi la utukufu.[#Kut 28:1-43]

8Akamvika ukamilifu wa uzuri, akampamba utukufu na nguvu; suruali ya bafta, na kanzu ndefu, na joho.

9Akamzungushia kengele na makomamanga ya dhahabu, ili kutoa sauti tamu akienda; kutoa sauti ya kusikika hekaluni, na kuwa ukumbusho wa wana wa watu wake.

10Tena vazi takatifu lenye dhahabu na samawi na urujuani, kazi ya mtarizi; na mfuko wa hukumu wenye Urimu na Thumimu, mwekundu uliosukwa, kazi ya fundi;

11na vito vilivyochorwa mfano wa mhuri juu ya deraya katika kijalizo cha dhahabu, kazi ya msanii; kila kito kiwe ukumbusho uliochorwa maandiko, kwa kadiri ya hesabu ya kabila za Israeli.

12Tena taji la dhahabu juu ya kofia, imenakishwa kama mhuri neno hili UTAKATIFU, pambo la heshima, kazi maarufu, ya kutamanika kwa macho, njema na nzuri.

13Kabla yake havikuwako kama hiyo; hakuna mgeni aliyejivika navyo, ila watoto wake daima katika vizazi vyao.

14Matoleo yake yateketezwa pia, kila siku mara mbili daima.

15Musa alimweka wakfu, akimpaka mafuta matakatifu; ikawa kwake agano la milele, na kwa wazao wake kama siku za mbinguni; ili kumhudumia Mungu, na kufanya kazi ya ukuhani, na kuwabariki watu wake kwa jina lake.[#Law 8:1-36]

16Akamchagua katika wote wenye uhai, ili kutoa sadaka ya kuteketezwa, na mafuta, na sadaka ya manukato matamu, na kumbukumbu; na kufanya upatanisho kwa wana wa Israeli.

17Naam, kwa amri yake alimpa mamlaka katika maagizo na hukumu; naye akawafundisha watu wake maagizo, na wana wa Israeli hukumu.

18Wageni walimkusanyikia na kumwonea wivu jangwani, Dathani na Abiramu pamoja na kikosi chao, na kusanyiko la Kora, katika nguvu ya hasira yao.[#Hes 16:1-35]

19BWANA akaliona hilo, nalo likamkasirisha, na katika ghadhabu ya hasira yake akawaangamiza. Akaumba ishara juu yao, na kwa moto wake wa miali akawateketeza.

20Akazidi kumtukuza Haruni, akampa urithi.

Alimpa matoleo ya bega kwa chakula,

Wale dhabihu za kuteketezwa za BWANA;

21Malimbuko akamwekea kuwa sehemu yake,

Kuwa kipawa chake na cha wazao wake.

22Maana hana urithi katika nchi ya watu,

Wala sehemu yoyote katikati yao;

Mradi BWANA ni sehemu ya urithi wao,

Katikati ya wana wa Israeli.

Finehasi

23Finehasi mwana wa Eleazari ndiye wa tatu, mtukufu katika uhodari wake; yaani, yeye alifanya wivu kwa ajili ya Mungu, akasimama imara walipogeuka watu; katika wema wa juhudi ya roho yake akafanya upatanisho kwa Israeli.[#Hes 25:7-13]

24Kwa hiyo kwa ajili yake Mungu akaliimarisha agizo, ndilo agano la amani la kudumisha patakatifu; ya kwamba yeye na wazao wake wawe na heshima ya ukuhani hata milele.

25Kama vile lilivyo agano na Daudi mwana wa Yese wa kabila ya Yuda, ya kwamba urithi wa ufalme awe nao peke yake na toka mwana hata mwana; ndivyo ulivyo urithi wa Haruni, una yeye na wazao wake.

26Sasa mhimidini BWANA aliye mwema,

Awatiaye ninyi taji la utukufu;

Na akujalie wewe hekima moyoni mwako,

Ili uwahukumu watu wake kwa haki;

Mema yao yasipate kubatilika,

Wala enzi yako hata vizazi vyote.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya