Zekaria 6

Zekaria 6

Maono ya nane: Magari manne ya vita

1Nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, yanatokea magari ya vita manne, yanatoka kati ya milima miwili, na milima hiyo ilikuwa ni milima ya shaba.

2Katika gari la kwanza walikuwa farasi wekundu; na katika gari la pili walikuwa farasi weusi;[#Zek 1:8; Ufu 6:4,5]

3na katika gari la tatu walikuwa farasi weupe; na katika gari la nne walikuwa farasi wa rangi ya kijivujivu.[#Ufu 6:2]

4Nikajibu, nikamwuliza yule malaika aliyesema nami, Hawa ni nini, Bwana wangu?[#Zek 5:10]

5Malaika akajibu, akaniambia, Hawa ni pepo nne za mbinguni, zitokeazo baada ya kusimama mbele za Bwana wa dunia yote.[#Zab 68:17; Ebr 1:7,14; 1 Fal 22:19; Ayu 1:6; Dan 7:10; Lk 1:19; Ufu 7:1]

6Gari lile lenye farasi weusi latoka kwenda hata nchi ya kaskazini; nao farasi weupe wanatoka kwenda katika nchi ya magharibi; na wale wa rangi ya kijivujivu wakatoka kwenda hadi nchi ya kusini.[#Yer 1:14; #6:6 Katika Kiebrania ni ‘wakatoka kufuata nyuma yao’.]

7Farasi wale walipotoka, walitaka kwenda huku na huko katika dunia; naye akawaambia, Haya! Tokeni, mwende huku na huko katika dunia. Basi wakaenda huku na huko katika dunia.[#Mwa 13:17]

8Ndipo akaniita, akaniambia akisema, Tazama, wale waendao mpaka nchi ya kaskazini wameituliza roho yangu katika nchi ya kaskazini.[#Mhu 10:4]

Kutawazwa kwa chipukizi

9Neno la BWANA likanijia, kusema,

10Pokea vitu mikononi mwa baadhi ya watu waliohamishwa, yaani, Heldai, na Tobia, na Yedaya; na siku iyo hiyo nenda ukaingie katika nyumba ya Yosia, mwana wa Sefania, waliyoifikia kutoka Babeli;[#Ezr 2:1]

11naam, pokea fedha na dhahabu, ukatengeneze taji, ukamvike kichwani Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu;[#Kut 28:36]

12ukamwambie, ukisema, BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Tazama, mtu huyu ndiye ambaye jina lake ni Chipukizi; naye atakua katika mahali pake, naye atalijenga hekalu la BWANA.[#Isa 9:6; 4:2; Zek 3:8; Mik 5:5; Mal 3:1; Yer 23:5; 33:15; Zek 13:7; 3:8; Mk 15:39; Lk 1:78; Yn 1:45; Zab 80:15-17; Mt 16:18; Efe 2:20; Flp 2:9; Ebr 2:9]

13Naam, yeye atalijenga hekalu la BWANA; naye atakuwa na heshima ya kifalme; na ataketi na kutawala; na kutakuwa na kuhani katika kiti chake cha enzi; na maelewano yenye amani yatakuwa kati ya hao wawili.[#Zab 21:5; 110:4; Isa 22:24; Ebr 3:1]

14Na hayo mataji yatakuwa ya Heldai, na Tobia, na Yedaya; na kwa fadhili za mwana wa Sefania; yawe kumbukumbu katika hekalu la BWANA.[#Mk 14:9]

15Nao walio mbali watakuja na kusaidia kujenga hekalu la BWANA, nanyi mtajua ya kuwa BWANA wa majeshi amenituma kwenu. Na haya yatatokea, kama mkijitahidi kuitii sauti ya BWANA, Mungu wenu.[#Efe 2:13]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya