The chat will start when you send the first message.
1Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Sikukuu za BWANA, ambazo mtazipigia mbiu kuwa ni makusanyiko matakatifu; hizi ni sikukuu zangu.[#Kut 32:5; Hes 10:2,3,10; 2 Nya 30:5; Yoe 1:14; 2 Fal 10:20; Zab 81:3]
3Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yo yote; ni Sabato kwa BWANA katika makao yenu yote.[#Kut 20:8-10; 23:12; 31:15; 34:21; 35:2; Kum 5:12-14; Lk 13:14; Neh 13:22; Isa 56:2; 58:13; Eze 20:12]
4Sikukuu za BWANA ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo mtayapigia mbiu kwa nyakati zake.[#Kut 23:14]
5Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya BWANA.[#Kut 12:1-13; Kum 16:1-2; Hes 28:16; Yos 5:10]
6Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa BWANA ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba.[#Kut 12:14-20; 23:15; 34:18; Kum 16:3-8]
7Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yo yote ya utumishi.[#Kut 12:16; Hes 28:18; Kum 16:1]
8Lakini mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.
9Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
10Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapokuwa mmekwisha ingia hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu;[#Kut 23:16; Hes 15:2,18; Kum 16:9; Yos 3:15; Mit 3:9; Rum 11:16; 1 Kor 15:20; Yak 1:18; Ufu 14:4]
11naye atautikisa mganda mbele za BWANA ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya Sabato kuhani atautikisa.[#Kut 29:24; Law 9:21; 10:14]
12Na siku hiyo mtakayoutikisa mganda, mtamsongeza mwana-kondoo wa kiume mkamilifu wa mwaka wa kwanza awe sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA.
13Na sadaka yake ya unga itakuwa sehemu za kumi mbili za efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, ni kafara iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto kuwa harufu ya kupendeza; na sadaka yake ya kinywaji itakuwa ni divai, robo ya hini.
14Nanyi msile mkate, wala bisi, wala masuke machanga, hata siku iyo hiyo, hata mtakapokuwa mmekwisha kuleta sadaka ya Mungu wenu; hii ni amri ya milele katika vizazi vyenu katika makao yenu yote.
15Nanyi mtajihesabia tangu siku ya pili baada ya Sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia Sabato saba;[#Kut 23:16; 34:22; Kum 16:9-12; Law 25:8]
16hata siku ya pili ya hiyo Sabato ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsongezea BWANA sadaka ya unga mpya.[#Mdo 2:1]
17Mtatoa katika makao yenu mikate miwili ya kutikiswa, itakuwa ya sehemu za kumi mbili za efa; itakuwa ya unga mwembamba, itaokwa na chachu, iwe malimbuko kwa BWANA.[#Kut 23:16; 22:29; Hes 15:17-19; Kum 26:1,2]
18Nanyi, pamoja na hiyo mikate, mtasongeza wana-kondoo saba, walio wakamilifu, wa mwaka wa kwanza, na ng’ombe mume mmoja, na kondoo waume wawili; watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA, pamoja na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji, sadaka ya harufu ya kupendeza iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto.
19Nanyi mtasongeza mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili waume wa mwaka wa kwanza kuwa dhabihu ya sadaka za amani.[#Law 4:23,28; Hes 28:30]
20Kisha kuhani atawatikisa pamoja na hiyo mikate ya malimbuko kuwa sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA, pamoja na wale wana-kondoo wawili; watakuwa watakatifu kwa BWANA, wawe wa huyo kuhani.[#Hes 18:12; Law 7:31-34; Kum 18:4]
21Nanyi mtapiga mbiu siku iyo hiyo; kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; msifanye kazi yo yote ya utumishi; ni amri ya milele katika makao yenu yote, katika vizazi vyenu.
22Nanyi hapo mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala msiyakusanye masazo ya mavuno yako; utayaacha kwa ajili ya huyo maskini, na mgeni; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.[#Law 19:9-10; Kum 24:19-22; Kut 23:11; Kum 15:1-18; Ayu 20:19; Zab 112:9; Mit 14:31; Isa 58:7,8; Yak 2:1; Rut 2:15,16]
23Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
24Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, kutakuwa na kustarehe kabisa kwenu, ni ukumbusho wa kuzipiga baragumu, ni kusanyiko takatifu.[#Hes 10:10; 29:1; Law 25:9]
25Msifanye kazi yo yote ya utumishi; nanyi mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto.
26Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,[#Law 16:29-34]
27Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtazitesa nafsi zenu; nanyi mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto.[#Kut 30:10; Law 16:30; Hes 29:7; Isa 58:3,5; Dan 10:3,12]
28Nanyi msifanye kazi yo yote siku hiyo; kwa kuwa ni siku ya upatanisho, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu mbele za BWANA, Mungu wenu.
29Kwa kuwa mtu awaye yote asiyejitesa mwenyewe siku iyo hiyo, atakatiliwa mbali na watu wake.[#Mwa 17:14; Law 13:46; Hes 5:2; 2 Nya 26:21; 2 The 3:6]
30Na mtu ye yote afanyaye kazi ya namna yo yote siku hiyo, mtu huyo nitamwangamiza atoke katika watu wake.
31Msifanye kazi ya namna yo yote; ni amri ya milele katika vizazi vyenu, katika makao yenu yote.
32Itakuwa kwenu sabato ya kustarehe kabisa, nanyi mtazitesa nafsi zenu; siku ya kenda ya mwezi wakati wa jioni, tangu jioni hata jioni, mtaishika hiyo Sabato yenu.
33Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,[#Kum 16:13-15]
34Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba ni sikukuu ya vibanda muda wa siku saba kwa BWANA.[#Kut 23:16; 34:22; Hes 29:12; Kum 16:13; Ezr 3:4; Neh 8:14; Zek 14:16; Yn 7:2; Ebr 11:9]
35Siku ya kwanza kutakuwa na kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.
36Mtamsongezea BWANA sadaka kwa moto siku saba; siku ya nane kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; nanyi mtamsongezea BWANA sadaka kwa moto; ni mkutano wa makini huu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.[#Hes 29:35; 2 Nya 7:8,9; Neh 8:18; Yn 7:37]
37Sikukuu za BWANA ni hizi, ambazo mtazipigia mbiu ya kuwa ni makusanyiko matakatifu, ili mmsongezee BWANA sadaka kwa moto, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na dhabihu, na sadaka za kinywaji, kila sadaka kwa siku yake;
38zaidi ya hizo Sabato za BWANA, na zaidi ya matoleo yenu, na zaidi ya hizo nadhiri zenu zote, na zaidi ya sadaka zenu za hiari, ambazo mwampa BWANA.
39Lakini siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, hapo mtakapokuwa mmekwisha kuyachuma mavuno ya nchi, mtaweka sikukuu ya BWANA muda wa siku saba; siku ya kwanza kutakuwa na kustarehe kabisa, na siku ya nane kutakuwa na kustarehe kabisa.[#Kut 23:16; Kum 16:13; Mt 21:8]
40Nanyi siku ya kwanza mtajipatia matunda ya miti mizuri, na makuti ya mitende, na matawi ya miti minene, na mierebi ya vijitoni; nanyi mtafurahi mbele za BWANA, Mungu wenu, muda wa siku saba.[#Neh 8:15; Kum 16:14; Isa 35:10; 66:10; Rum 5:11]
41Nanyi mtaishika kuwa sikukuu kwa BWANA muda wa siku saba katika mwaka; ni amri ya milele katika vizazi vyenu; mtaishika katika mwezi wa saba.
42Mtakaa katika vibanda muda wa siku saba; wazalia wote wa Israeli watakaa katika vibanda;
43ili vizazi vyenu vipate kujua ya kuwa niliwaketisha wana wa Israeli katika vibanda, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri; mimi ndimi BWANA Mungu wenu.[#Kum 31:13; Zab 78:5,6]
44Naye Musa akawaambia wana wa Israeli hizo sikukuu za BWANA.