The chat will start when you send the first message.
1JE! tunaanza tena kujisifu nafsi zetu? au tunahitaji, kama wengine, barua zenye sifa zetu kwenu, au zitokazo kwenu?
2Barua yetu ni ninyi iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu wote;
3mnadhihirishwa kuwa m barua ya Kristo iliyo kazi ya khuduma yetu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho ya Mungu aliye hayi; si katika vibao vya mawe, bali katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama.
4Na tumaini hiio tunalo mbele za Mungu kwa Kristo;
5si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu,
6aliyetutosheleza kuwa wakhudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha.
7Bassi, ikiwa khuduma ya mauti katika maandiko, iliyochorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hatta wana wa Israeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao utukufu uliokuwa ukibatilika;
8je! khuduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu?
9Kwa maana ikiwa khuduma ya hukumu ina utukufu, khuduma ya haki ina utukufu unaozidi sana.
10Maana hatta ile iliyotukuzwa haikuwa na utukufu kwa sababu hii, kwa ajili ya utukufu uzidio sana.
11Kwa maana, ikiwa ile inayobatilika ilikuwa na utukufu ukomao, zaidi sana ile ikaayo ina utukufu udumuo.
12Bassi, kwa kuwa tuna taraja la namna hii, twatumia ujasiri mwingi;
13nasi si kama Musa alivyotia utaji juu ya uso wake, illi wana wa Israeli wasitazame sana mwisho wa ile iliyokuwa ikibatilika;
14pamoja na hayo fikara zao zilitiwa ugumu; kwa maana hatta leo utaji huo huo, wakati lisomwapo Agano la Kale, wakaa, haukuondolewa; ambao buoudolewa katika Kristo;
15bali hatta leo, Musa asomwapo, utaji huikalia mioyo yao.
16Lakini wakati wo wote itakapomgeukia Bwana ule utaji huondolewa.
17Bassi Bwana ndiye Roho huyo; walakini alipo Roho ya Bwana, hapo ndipo panapo uhuru.
18Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiuangalia utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa na kufananishwa na mfano huo huo, toka utukufu hatta utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana aliye Roho.