The chat will start when you send the first message.
1PAOLO, Silwano, na Timotheo kwa kanisa la Wathessaloniki lililo katika Mungu Baba yetu, na Bwana Yesu Kristo:
2Neema iwe kwenu na imani zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na Bwana Yesu Kristo.
3Imetupasa kumshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu, ndugu, kama ilivyo wajib, kwa kuwa imani yenu inazidi sana, na upendo wa killa mtu kwenu kwa wenzake umekuwa mwingi.
4Hatta sisi wenyewe twajisifu katika makanisa ya Mungu kwa ajili ya uvumilivu wenu, na imani mliyo nayo katika adha zenu zote na mateso mnayoyavumilia;
5ndio ishara ya hukumu ya haki ya Mungu illi mstabilishwe kuuingia ufalme wa Mungu, ambao kwa ajili yake mnateswa;
6kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi,
7na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake,
8katika mwako wa moto, akiwalipa kisasi wao wasiomjua Mungu, nao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo;
9watakaoadhibiwa kwa uharibifu wa milele, kutengwa na uso wa Bwana na na utukufu wa nguvu zake,
10atakapokuja illi kutukuzwa katika watakatifu wake, na kuajabiwa katika wote waaminio (kwa sababu ushuhuda wetu ulisadikiwa kwenu), katika siku ile.
11Kwa hiyo twawaombea ninyi siku zote, illi Mungu wetu awahesabu kuwa nimeustahili wito wenu, akatimize killa haja ya wema na killa kazi ya imani kwa nguvu:
12jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe kwenu, na ninyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.