Warumi 12

Warumi 12

1BASSI, nawasihi, ndugu, kwa huruma zake Mungu, mtoe miili yenu iwe dhabihu hayi, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ibada yenu yenye maana.

2Wala msifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufunya upya nia zenu, mpate kujua kwa hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.

3Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia killa mtu alioko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyoamgawi killa mtu kadiri ya imani.

4Kwa maana kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, navyo viungo vyote havitendi kazi moja;

5vivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na sisi sote tu viungo killa mmoja kwa wenzake.

6Bassi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani;

7ikiwa khuduma, tuwemo katika khuduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake;

8mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukarimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia, kwa bidii; mwenye kurehemu, kwa furaha.

9Pendo niwe nalo pasipo unafiki; mkichukia lililo ovu, mkiambatana na lililo jema.

10Kwa pendo la udugu, mwe na shauku ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu;

11kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;

12kwa tumaini, mkifurahi; katika shidda, mkivumilia; katika kusali, mkidumu;

13kwa mahitaji ya watakatifu, mkiwashirikisha; katika kukaribisha wageni, mkijitahidi.

14Wabarikini wanaowafukuzeni; barikini, wala msilaani.

15Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao.

16Mwe na nia moja ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge.

Msiwe watu wa kujivunia akili.

17Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Andaeni yaliyo mema machoni pa watu wote.

18Kama yumkini, kwa upande wenu, mwe na amani na watu wote.

19Msijilipize kisasi, wapenzi, bali ipisheni ghadhabu; maana imeandikwa, Kisasi juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.

20Bassi adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivi, utampalia makaa ya moto kichwani pake.

21Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Published by: Bible Society of Tanzania