The chat will start when you send the first message.
1Mlifufuka pamoja na Kristo kutoka kwa wafu. Hivyo ishini maisha mapya, mkiyatazamia yaliyo mbinguni, ambako Kristo ameketi mkono wa kulia wa Mungu.
2Msiyafikirie yaliyo hapa duniani bali yaliyo mbinguni.
3Utu wenu wa kwanza umekufa, na utu wenu mpya umetunzwa na Kristo katika Mungu.
4Kristo ndiye utu wenu mpya sasa, na atakaporudi mtashiriki katika utukufu wake.
5Kwa hiyo kiueni chochote kilicho cha kidunia kilichomo ndani yenu: uasherati, matendo machafu, mawazo na tamaa mbaya. Msijitakie na kujikusanyia vitu vingi, kwani ni sawa na kuabudu mungu wa uongo.
6Mungu ataionyesha hasira yake kwa wale wasiomtii, kwa sababu ya maovu wanayotenda.[#3:6 Baadhi ya nakala za Kiyunani hazina maneno haya.]
7Ninyi pia mlifanya maovu haya huko nyuma, mlipoishi kama wao.
8Lakini sasa, jitengeni mbali na mambo haya katika maisha yenu: hasira, ukorofi, chuki, na mazungumzo yenye matusi.
9Msiambiane uongo ninyi kwa ninyi. Ninyi mmeyavua mavazi ya kale; utu wa kale mliokuwa nao na matendo mabaya mliyotenda hapo awali.
10Na sasa mmevaa utu mpya unaofanywa upya kila siku hata kuufikia ufahamu kamili wa Kristo. Mfano wenu wa maisha mapya ni Kristo, aliye mfano na sura ya Mungu aliyewaumba ninyi.
11Katika utu huu mpya haijalishi ikiwa wewe ni Myunani au Myahudi, umetahiriwa au hujatahiriwa. Haijalishi pia ikiwa unazungumza lugha tofauti au hata kama wewe ni mtu asiyestaarabika, ikiwa ni mtumwa ama mtu huru. Kristo ndiye wa muhimu zaidi, naye yumo ndani yenu ninyi nyote.[#3:11 Au Msithiani. Wasithiani ni watu waliojulikana kuwa watu waishio porini na wasio na ustaarabu wa kibinadamu.]
12Mungu amewachagua na kuwafanya ninyi kuwa watu wake walio watakatifu. Anawapenda. Hivyo, jivikeni matendo haya na muwe na huruma: wema, wanyenyekevu, wapole na wenye subira.
13Msikasirikiane, bali msameheane. Mtu yeyote akikukosea, msamehe. Wasameheni wengine kwa sababu Bwana amewasamehe ninyi.
14Pamoja na haya yote, vaeni upendo. Upendo ndicho kitu kinachounganisha kila kitu katika umoja mkamilifu.
15Amani inayotoka kwa Kristo itawale fahamu zenu. Mliitwa kwa ajili ya amani ili muwe pamoja katika mwili mmoja. Muwe na shukrani daima.[#3:15 Mwili wa kiroho wa Kristo, yaani Kanisa ambalo ni watu wake.]
16Na mafundisho ya Kristo yakae kwa wingi ndani yenu. Mfundishane na mshauriane ninyi kwa ninyi kwa hekima yote, mkiimba zaburi, nyimbo za sifa na nyimbo zinaowezeshwa na roho na kumshukuru Mungu katika mioyo yenu.[#3:16 Yaani Injili au Ujumbe kuhusu Kristo au Neno la Mungu.]
17Kila mnachosema na kutenda, mkifanye kwa ajili ya Yesu Kristo Bwana wenu huku mkimshukuru Mungu Baba kupitia Yesu Kristo.
18Wake, muwe radhi kuwatumikia waume zetu. Ni jambo sahihi kufanya katika kumfuata Bwana.
19Waume wapendeni wake zenu na msiwe na hasira nao.
20Watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote. Hili humfurahisha Bwana.
21Wababa, msiwakorofishe watoto wenu, mkiwa wagumu kupendezwa nao; wanaweza kukata tamaa.
22Enyi watumwa, watiini mabwana zenu katika mambo yote. Muwe watii kila wakati, hata kama wao hawawezi kuwaona. Msijifanye kazi kwa bidii ili wawatendee mema. Mnapaswa kuwatumikia mabwana zenu kwa moyo kwa sababu mna hofu ya Bwana.[#3:22 Au “wakuu wenu”.]
23Kila kazi mnayoifanya, ifanyeni kwa bidii. Fanyeni kama mnamfanyia Bwana wenu wa mbinguni, na si kama mnamfanyia bwana wa dunia hii.
24Mnajua kwamba mtapokea kutoka kwa Bwana ujira aliowaahidi watu wake. Ndiyo, mnamtumikia Kristo aliye Bwana wenu halisi.[#3:24 Au “Mkuu”.]
25Kumbukeni kuwa Mungu hana upendeleo; kila anayefanya uovu ataadhibiwa kwa sababu ya uovu wake.