The chat will start when you send the first message.
1Ninalolisema ni hili: Wakati mrithi wa vyote alivyomiliki baba yake bado ni mdogo, hana tofauti yoyote na mtumwa. Haijalishi kuwa anamiliki vitu vyote.
2Wakati wa utoto bado anapaswa kuwatii wale waliochaguliwa kumtunza. Lakini anapoufikia umri ambao baba yake ameuweka, anakuwa huru.
3Ndivyo ilivyo hata kwetu sisi. Mwanzoni tulikuwa kama watoto, tukiwa watumwa wa mamlaka za uovu zinazoutawala ulimwengu huu wa sasa.[#4:3 Ina maana pia ya nguvu za giza.]
4Lakini wakati sahihi ulipofika, Mungu akamtuma Mwanawe, aliyezaliwa na mwanamke na akaishi chini ya sheria.
5Mungu alifanya hivi ili aweze kuwaweka huru wale waliokuwa chini ya sheria. Kusudi la Mungu lilikuwa kutuasili sisi kama watoto wake.[#4:5 Ina maana ya kutufanya watoto wake na kutupa haki zote.]
6Ninyi sasa ni watoto wa Mungu. Na ndiyo sababu Mungu amemtuma Roho wa Mwanaye mioyoni mwetu. Huyo Roho aliye ndani yetu hulia “Aba, yaani Baba.”[#4:6 Ni neno la Kiaramu lililotumiwa na watoto wa Kiyahudi kama jina la kuwaita baba zao.]
7Sasa ninyi si watumwa kama mwanzo. Ni watoto wa Mungu, na mtapokea kila kitu ambacho Mungu aliwaahidi watoto wake. Hii yote ni kwa sababu ya yale ambayo Mungu amewatendea ninyi.
8Zamani hamkumjua Mungu. Mlikuwa watumwa wa miungu isiyokuwa halisi.
9Lakini sasa mnamjua Mungu wa kweli. Hakika, Mungu ndiye anayewajua ninyi. Hivyo kwa nini sasa mnavigeukia vikosi dhaifu na visivyo na manufuaa yoyote mlivyovifuata hapo mwanzo? Mnataka kuwa watumwa wa mambo haya tena?
10-11Inanipa wasiwasi kwa kuwa mnaadhimisha siku, miezi, misimu na miaka. Nina hofu ya kuwa nimefanya kwa bidii kazi bure kwa ajili yenu.
12Ndugu zangu, naomba mniige mimi kama ambavyo mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunikosea kwa jambo lololote.
13Mnajua kuwa nilikuja kwenu mara ya kwanza kwa sababu nilikuwa mgonjwa. Ndipo nilipowaeleza ninyi Habari Njema.
14Ugonjwa wangu uliwaelemea. Hata hivyo hamkunikataa kutokana na fadhaa ama hofu. Bali, mlinikaribisha kama vile nilikuwa malaika kutoka kwa Bwana. Mlinipokea kama vile nilikuwa Kristo Yesu mwenyewe!
15Mlikuwa na furaha sana wakati huo. Nini kimetokea kwa imani yenu ya awali kwamba mimi nilikuwa mtu niliyebarikiwa kipekee na Mungu? Naweza kusema bila shaka yoyote kwamba mngeliweza kufanya kitu chochote kunisaidia. Kama ingeliwezekana, mngeliyang'oa hata macho yenu na kunipa mimi.
16Je! nimekuwa sasa adui yenu kwa sababu nawaambia ukweli?
17Watu hawa wanajitahidi sana kuonesha kuvutiwa nanyi, lakini hiyo siyo nzuri kwenu. Wanataka kuwashawishi ninyi ili mtugeuke sisi na kuambatana nao.[#4:17 Walimu wa uongo waliokuwa wanawasumbua waamini kule Galatia. Tazama Gal 1:7.; #4:17 Ina maana ya “wanakereketwa sana kwa mambo yenu”.]
18Inapendeza daima kuwa na mtu anayevutiwa nawe katika jambo lililo jema. Hivyo ndivyo nilivyofanya nilipokuwa pamoja nanyi. Siku zote inapendeza, na si pale tu mimi nikiwapo.
19Watoto wangu wadogo, nasikia uchungu tena kwa ajili yenu, kama mama anayejifungua. Nitaendelea kusikia uchungu huu mpaka watu watakapofikia kumwona Kristo wawatazamapo ninyi.
20Natamani ningekuwa nanyi sasa. Ndipo labda ninapoweza kubadilisha namna ninavyoongea nanyi. Sasa sielewi nifanye nini juu yenu.
21Baadhi yenu mnataka kuwa chini ya sheria. Niambieni, mnajua sheria inavyosema?
22Maandiko yanasema kwamba Abrahamu alikuwa na wana wawili. Mama wa mwana mmoja alikuwa ni mjakazi, na mama wa mwana mwingine alikuwa wa mwanamke aliye huru.
23Mwana wa Abrahamu kutoka kwa mjakazi alizaliwa kwa namna ya kawaida ya kibinadamu. Lakini mwana kutoka kwa mwanamke aliyekuwa huru alizaliwa kwa sababu ya ahadi ambayo Mungu alimpa Abrahamu.
24Habari hii ina maana nyingine kwenu. Wanawake wawili ni sawa na maagano mawili baina ya Mungu na watu wake. Agano moja ni sheria ambayo Mungu aliifanya katika Mlima Sinai, inayowafanya watu wawe watumwa. Mwanamke aliyeitwa Hajiri yuko kama agano la kwanza.
25Hivyo Hajiri anauwakilisha Mlima Sinai uliopo Arabia. Na anafanana na Yerusalemu wa sasa, kwa sababu mji huu uko utumwani pamoja na watu wake.
26Lakini Yerusalemu ya mbinguni ulio juu uko kama mwanamke aliye huru, ambaye ndiye mama yetu.
27Maandiko yanasema,
“Ufurahi mwanamke, wewe uliye tasa.
Ufurahi kwani hukuwahi kuzaa.
Piga kelele na ulie kwa furaha!
Hukupata uchungu wa kuzaa.
Mwanamke aliye peke yake atapata watoto zaidi
zaidi ya mwanamke aliye na mume.”
28Ndugu zangu, ninyi ni watoto mliozaliwa kwa sababu ya ahadi ya Mungu, kama Isaka alivyozaliwa.
29Lakini mwana mwingine wa Abrahamu, aliyezaliwa kwa njia ya kawaida, alisababisha matatizo kwa yule aliyezaliwa kwa nguvu ya Roho. Ndivyo ilivyo leo.
30Lakini Maandiko yanasemaje? “Mfukuze mjakazi na mwanawe! Mwana wa mwanamke aliye huru atapokea kila kitu alicho nacho baba yake, lakini mwana wa mjakazi hatapokea kitu.”[#Mwa 21:10]
31Hivyo, kaka na dada zangu, sisi si watoto wa mjakazi. Ni watoto wa mwanamke aliye huru.