Wafilipi 2

Wafilipi 2

Iweni katika Umoja na Msaidiane

1Fikirini kuhusu kile ambacho tulichonacho kwa sababu tunamilikiwa na Kristo: hamasa aliyotuletea, faraja ya upendo wake, ushirika katika Roho wake, huruma na wema aliotuonyesha. Ikiwa mnazifurahia baraka hizi,

2basi fanyeni yale yatakayoikamilisha furaha yangu: iweni na nia moja na mpendane ninyi kwa ninyi. Iweni na umoja katika malengo yenu na katika kufikiri kwenu.

3Msiruhusu ubinafsi au kiburi viwe dira yenu. Badala yake muwe wanyenyekevu mkiwathamini wengine kuliko ninyi wenyewe.

4Kila mmoja wenu asijishugulishe kwa mema yake yeye mwenyewe bali kwa mema ya wengine.

5Hivi ndivyo mnapaswa kufikiri, kuhisi na kutenda katika maisha yenu kwa pamoja, kama vile Kristo Yesu alivyofikiri:

6Alikuwa sawa na Mungu katika namna zote,

lakini hakufikiri kwamba kuwa sawa na Mungu

kilikuwa kitu cha manufaa kwake.

7Badala yake, aliacha kila kitu,

hata sehemu yake pamoja na Mungu.

Akakubali kuwa kama mtumwa,

akiwa katika umbo la binadamu.

Wakati wa maisha yake kama mtu,

8Alijinyenyekeza na akawa mtiifu kabisa kwa Mungu,

hata jambo hilo liliposababisha kifo chake msalabani.

9Hivyo ndiyo sababu Mungu alimpa mahali pa heshima sana,

na akampa jina lililo kuu kuliko majina yote.

10Hivyo kila mtu atasujudu kumheshimu Yesu.

Kila mmoja aliye mbinguni, duniani na wale walio chini ya dunia.

11Wote watakiri kwamba, “Yesu Kristo ni Bwana,”

na hili litamtukuza Mungu Baba.

Iweni Kama Mungu Anavyotaka

12Rafiki zangu wapendwa, daima mnatii yale mliyofundishwa. Kama mlivyotii nilipokuwa pamoja nanyi, ni muhimu zaidi na zaidi kwamba mtii wakati huu ambapo sipo pamoja nanyi. Hivyo ni lazima mwendelee kuishi katika namna inayoleta maana kwa wokovu wenu. Fanyeni hivi kwa wingi wa heshima na utii kwa Mungu.

13Ndiyo, Mungu ndiye anayetenda kazi ndani na miongoni mwenu. Anawasaidia ninyi kutaka kutenda yanayomfurahisha, naye anawapa nguvu ya kuyatenda.

14Fanyeni mambo yote pasipo kulalamika wala kubishana.

15Nanyi mtakuwa watoto wa Mungu wasiolaumiwa na wasio na hatia. Ijapokuwa mnaishi mkiwa mmezungukwa na watu wasio waaminifu wasiojali thamani haki. Katikati ya watu hao mnang'ara kama mianga katika ulimwengu wenye giza,

16nanyi mnawapa mafundisho yanayotoa uhai. Hivyo nitaona fahari juu yenu wakati Kristo atakapokuja tena. Ninyi ndiyo mtakaothibitisha kuwa kazi niliyoifanya haikukosa matokeo, ya kwamba nilishindana mbio na nikashinda.

17Imani yenu inayatoa maisha yenu kama sadaka katika kumtumikia Mungu. Hata kama ni kweli kwamba sasa ninajimimina mimi mwenyewe kama sadaka ya kinywaji pamoja na sadaka yenu, ninayo furaha, na nitawashirikisha ninyi nyote furaha yangu.

18Ninyi pia mnapaswa kufurahi na kunishirikisha furaha yenu.

Habari Kuhusu Timotheo na Epafrodito

19Kwa baraka za Bwana Yesu, ninategemea kuwa nitamtuma Timotheo kwenu hivi karibuni. Naye atarejesha kwangu taarifa kuhusu ninyi ili nifurahi.

20Sina mtu mwingine yeyote kama Timotheo, ambaye kwa dhati kabisa anayajali mambo yanayowahusu.

21Wengine wote wanajishughulisha na maisha yao wenyewe. Hawajali kazi ya Yesu Kristo.

22Mnafahamu Timotheo amejithibitisha kuwa ni mtu wa aina gani. Ametumika pamoja nami katika kuhubiri Habari Njema kwa njia ambavyo mwana angemtumikia baba yake.

23Ninategemea kumtuma aje kwenu haraka baada ya kujua yatakayonipata.

24Bwana hunifanya niwe jasiri ili niweze pia kuja kwenu haraka.

25Kwa sasa, nadhani ni lazima nimrudishe Epafrodito kwenu. Ni mtumishi na mtenda kazi pamoja nami na askari mwenzangu katika jeshi la Bwana. Nilipotaka msaada, mlimtuma kwangu. Kama mjumbe wenu, alinihudumia mahitaji yangu.

26Lakini sasa anataka kuwaona ninyi nyote tena. Ana wasiwasi sana kwa sababu mlisikia kuwa alikuwa mgonjwa.

27Alikuwa mgonjwa karibu ya kufa. Lakini Mungu alimsaidia yeye na mimi ili nisiwe na huzuni zaidi.

28Hivyo ninataka sana kumtuma kwenu. Ili mtakapomwona, mfurahi. Nami nitaacha kuwa na wasiwasi juu yenu.

29Mkaribisheni kwa furaha nyingi katika Bwana. Waheshimuni watu kama Epafrodito.

30Anapaswa kuheshimiwa kwa sababu alikaribia kufa akifanya kazi kwa ajili ya Kristo. Aliyaweka maisha yake katika hatari ili aweze kunisaidia. Ni msaada ambao msingeweza kunisaidia.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International