Warumi 10

Warumi 10

1Kaka na dada zangu, ninalotamani zaidi ni kwamba Waisraeli wote waokolewe. Hayo ndiyo maombi yangu kwa Mungu.

2Naweza kusema hili juu yao: Kwa hakika wana bidii sana ya kumtii Mungu, lakini hawaijui njia iliyo sahihi.

3Hawakuelewa kile ambacho Mungu alifanya ili kuwaokoa watu. Hivyo walijaribu kwa njia yao wenyewe kupata kibali kwa Mungu kwa kuishika sheria. Na wakakataa kuifuata njia ya Mungu ya kuwaokoa watu.

4Sheria ilifikia mwisho wake wakati Kristo alipolikamilisha kusudi lake. Sasa kila mtu anayeiweka imani yake kwake anahesabiwa haki mbele za Mungu.

5Musa anaandika juu ya kuhesabiwa haki kwa kuifuata sheria. Anasema: “Ili kupata uzima katika sheria imempasa mtu kuzitii.”[#Law 18:5]

6Lakini Maandiko yanasema haya kuhusu kuhesabiwa haki kwa njia ya imani: “Usiyaseme haya kwako wewe mwenyewe, ‘Nani atapanda kwenda mbinguni?’” (Hii inamaanisha “Nani atapanda mbinguni kumchukua Kristo na kumleta chini duniani?”)

7“Na usiseme, ‘Nani atashuka hadi ulimwengu uliopo chini huko?’” (Hii inamaanisha “Nani atashuka chini na kumchukua Kristo na kumfufua kutoka mauti?”)

8Hivi ndivyo Maandiko yanavyosema: “Mafundisho ya Mungu yako karibu nawe; yako katika kinywa chako na katika moyo wako.” Ni mafundisho ya imani tunayowaambia watu.[#Kum 30:12-14]

9Ukikiri wazi kwa kinywa chako, kwamba “Yesu ni Bwana” na kuamini moyoni mwako kuwa Mungu alimfufua kutoka mauti, utaokolewa.

10Ndiyo, tunamwamini Yesu mioyoni mwetu, na Mungu hutukubali kuwa wenye haki. Na tunakiri wazi wazi kwa vinywa vyetu kwamba tunamwamini Mungu na yeye anatuokoa.

11Ndiyo, Maandiko yanasema, “Yeyote anayemwamini hataaibika.”[#Isa 28:16 (Tafsiri ya Kiyunani)]

12Yanasema hivi kwa sababu hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi. Bwana yule yule ndiye Bwana wa watu wote. Naye humbariki sana kila amwombaye akitaka msaada.

13Ndiyo, “kila mtu anayemwita Bwana ili kupata msaada, ataokolewa.”[#10:13 Kihalisia, “anayeliita jina la Bwana”, ikimaanisha kuonesha imani katika yeye kwa kumwabudu au kumwomba yeye msaada.; #10:13 Yoe 2:32. Tazama pia Kut 2:23-25.]

14Lakini watu watawezaje kumwita Bwana na kupata msaada wake ikiwa hawamwamini yeye? Na watawezaje kumwamini Bwana ikiwa hawajawahi kuzisikia habari zake? Na watawezaje kuzisikia habari zake ikiwa hayupo mtu wa kuwaambia?

15Na mtu atawezaje kwenda na kuwaambia habari hizo ikiwa hajatumwa? Haya, hii ndiyo sababu Maandiko yanasema, “Ni jambo la kufurahisha kumwona mtu anayepeleka Habari Njema!”[#Isa 52:7]

16Lakini si watu wote walizipokea Habari Njema hizo. Na hii ndiyo sababu Isaya alisema, “Bwana, nani aliyeamini yale tuliyowaeleza?”[#Isa 53:1]

17Kwa hiyo imani hupatikana kutokana na kusikia Habari Njema. Na watu husikia Habari Njema wakati mtu anapowaeleza kuhusu Kristo.

18Lakini nauliza, “Je! watu hao walizisikia Habari Njema?” Ndio Kwa kweli walizisikia kama Maandiko yanavyosema,

“Sauti zao zilitoka na kuenea duniani kote.

Maneno yao yakaenda kila mahali ulimwenguni.”

19Lakini tena nauliza, “Je! watu wa Israeli hawakuelewa?” Ndiyo, walielewa. Musa alikuwa wa kwanza kujibu swali hili. Na anasema haya kwa ajili ya Mungu:

“Nitawatumia wale ambao siyo Taifa halisi ili liwafanye muone wivu.

Nitalitumia taifa ambalo halielewi ili mkasirike.”

20Kisha Isaya ana ujasiri wa kutosha kusema haya kwa ajili ya Mungu:

“Watu walionipata mimi hawakuwa wakinitafuta.

Nilijitambulisha kwa watu ambao hawakuwa wakinitafuta.”

21Lakini kuhusu watu wa Israeli Mungu anasema,

“Kutwa nzima nilisimama nikiwa tayari kuwakubali watu hawa,

lakini ni wakaidi na wamekataa kunitii.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International