The chat will start when you send the first message.
1Karibieni mkasikilize enyi mataifa,
tegeni sikio enyi watu.
Sikiliza ee dunia na vyote vilivyomo,
ulimwengu na vyote vitokavyo humo!
2Mwenyezi-Mungu ameyakasirikia mataifa yote,
ameghadhabika dhidi ya majeshi yao yote.
Ameyapangia mwisho wao,
ameyatoa yaangamizwe.
3Maiti zao zitatupwa nje;
harufu ya maiti zao itasambaa;
milima itatiririka damu yao.
4Jeshi lote la angani litaharibika,[#34:4 Taz Mat 24:29; Marko 13:25; Luka 21:26; Ufu 6:13-14]
anga zitakunjamana kama karatasi.
Jeshi lake lote litanyauka,
kama majani ya mzabibu yanyaukavyo,
naam, kama tunda la mtini linyaukavyo.
5Upanga wa Mungu uko tayari juu mbinguni.[#34:5-17 Taz Isa 63:1-6; Yer 49:7-22; Eze 25:12-14; 35:1-15; Amo 1:11-12; Oba]
Tazama, washuka kuwaadhibu Waedomu,
watu ambao ameamua kuwaangamiza.
6Upanga utalowa damu na kutapakaa mafuta,
kama kwa damu ya kondoo na mbuzi,
na mafuta ya figo za kondoo dume.
Maana Mwenyezi-Mungu atatoa kafara huko Bosra,
kutakuwa na mauaji makubwa nchini Edomu.
7Nyati wataangamia pamoja nao,
ndama kadhalika na mafahali.
Nchi italoweshwa damu,
udongo utarutubika kwa mafuta yao.
8Maana Mwenyezi-Mungu anayo siku ya kisasi;
mwaka wa kulipiza maadui wa Siyoni.
9Vijito vya Edomu vitatiririka lami,
udongo wake utakuwa madini ya kiberiti;
ardhi yake itakuwa lami iwakayo.
10Itawaka usiku na mchana bila kuzimika,[#34:10 Taz Ufu 14:11; 19:3]
moshi wake utafuka juu milele.
Nchi itakuwa jangwa siku zote,
hakuna atakayepitia huko milele.
11Itakuwa makao ya kozi na nungunungu,
bundi na kunguru wataishi humo.
Mwenyezi-Mungu atawaletea ghasia,
na timazi la fujo kwa wakuu wake.
12Nchi itaitwa “Nchi bila Mfalme;”
wakuu wake wote wametoweka.
13Miiba itaota katika ngome zake,
viwavi na michongoma mabomani mwao.
Itakuwa makao ya mbwamwitu, maskani yao mbuni.
14Pakamwitu na fisi watakuwa humo,
majini yataitana humo;
kwao usiku utakuwa mwanga,
na humo watapata mahali pa kupumzikia.
15Humo bundi watataga mayai na kuyaatamia,
wataangua vifaranga na kuviweka kivulini mwao.
Humo vipanga watakutania,
kila mmoja na mwenzake.
16Someni katika kitabu cha Mwenyezi-Mungu:
“Hakuna hata kiumbe kimoja kitakachokosekana,
kila kimoja kitakuwako na mwenzake.”
Maana Mwenyezi-Mungu mwenyewe ametamka hivyo,
roho yake itawakusanya hao wote.
17Mwenyezi-Mungu amepanga sehemu ya kila mmoja wao,
ametumia kamba kuwapimia nchi hiyo;
wataimiliki milele na milele,
wataishi humo kizazi hata kizazi.