Isaya 5

Isaya 5

Wimbo wa shamba la mizabibu

1Nitaimba juu ya rafiki yangu,[#5:1-2 Taz Mat 21:33; Marko 12:1; Luka 20:9]

wimbo wa rafiki yangu na shamba lake la mizabibu:

Rafiki yangu alikuwa na shamba la mizabibu

juu ya kilima chenye rutuba nyingi.

2Alililima vizuri na kuondoa mawe yote,

akaotesha humo mizabibu iliyochaguliwa;

alijenga mnara wa ulinzi katikati yake,

akachimba kisima cha kusindikia divai.

Kisha akangojea lizae zabibu,

lakini likazaa zabibu chungu.

3Kwa hiyo rafiki yangu anasema hivi:

“Enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda,

amueni tafadhali kati yangu na shamba langu.

4Ni kitu gani nilichokosa kulifanyia shamba langu?

Na nilipotazamia lizae zabibu nzuri,

mbona basi, likazaa zabibu chungu?

5“Na sasa nitawaambieni

nitakavyolifanya hilo shamba langu.

Nitauondoa ua wake,

nalo litaharibiwa.

Nitaubomoa ukuta wake,

nalo litakanyagwakanyagwa.

6Nitaliacha liharibiwe kabisa,

mizabibu yake haitapogolewa wala kupaliliwa.

Litaota mbigili na miiba.

Tena nitayaamuru mawingu

yasinyeshe mvua juu yake.”

7Naam! Shamba la mizabibu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi

ni jumuiya ya Waisraeli,

na mizabibu mizuri aliyoipanda ni watu wa Yuda.

Yeye alitazamia watende haki,

badala yake wakafanya mauaji;

alitazamia uadilifu,

badala yake wakasababisha kilio!

Maovu wanayotenda watu

8Ole wao wanaonunua nyumba baada ya nyumba,

wanaoongeza mashamba juu ya mashamba yao,

mpaka kila sehemu inakuwa mali yao,

na hamna nafasi kwa wengine nchini.

9Nimemsikia Mwenyezi-Mungu wa majeshi akitamka hivi:

“Hakika nyumba nyingi zitabaki tupu,

majumba makubwa mazuri bila wakazi.

10Shamba la mizabibu la eka kumi

litatoa lita nane tu za divai;

anayepanda kilo 100 za mbegu

atavuna kilo 10 tu za nafaka.”

11Ole wao wanaoamka asubuhi na mapema

wapate kukimbilia kunywa kileo;

wanaokesha hata usiku,

mpaka divai iwaleweshe!

12Katika karamu zao, hapakosekani vinubi,

zeze, matari, filimbi na divai.

Lakini hawajali matendo ya Mwenyezi-Mungu,

wala kuzitambua kazi za mikono yake.

13Kwa hiyo, watu wangu watapelekwa uhamishoni

kwa sababu ya utovu wao wa akili.

Watu wenu mashuhuri watakufa njaa,

watu wengi watakufa kwa kiu.

14Kuzimu inawangoja kwa hamu kubwa,

imepanua kinywa chake mpaka mwisho.

Waheshimiwa pamoja na raia wa Yerusalemu

wanaingia humo makundi kwa makundi,

kadhalika na wote wanaousherehekea.

15Kila mtu atafedheheshwa,

na wenye kiburi wote wataaibishwa.

16Lakini Mwenyezi-Mungu wa majeshi atatukuzwa.

Yeye huonesha ukuu wake

kwa matendo yake ya haki,

kwa kuwahukumu watu wake.

17Wanakondoo, wanambuzi na ndama,

watapata malisho yao kwenye magofu ya miji yao,

kana kwamba hizo ni sehemu za malisho yao.

18Ole wao wanaoburuta uovu kama kwa kamba;

wanaokokota dhambi kama kwa kamba za mkokoteni.

19Wanasema:

“Mwache Mwenyezi-Mungu afanye haraka,

tunataka kuyaona aliyosema atayafanya!

Mtakatifu wa Israeli na atimize kusudi lake.

Hebu na tuone ana mipango gani!”

20Ole wao wanaosema uovu ni wema

na wema ni uovu.

Giza wanasema ni mwanga

na mwanga wanasema ni giza.

Kichungu wanasema ni kitamu

na kitamu wanakiona kuwa kichungu.

21Ole wao wanaojiona kuwa wenye hekima

ambao wanajiona kuwa wenye akili.

22Ole wao mabingwa wa kunywa divai,

hodari sana wa kuchanganya vileo.

23Kwa hongo kidogo wanawaachilia wenye hatia

na kuwanyima wasio na hatia haki yao.

24Kwa hiyo, kama moto uteketezavyo nyasi,

kama majani yateketeavyo katika mwali wa moto

ndivyo na mizizi yao itakavyooza,

na maua yao yatakavyopeperushwa juu kama vumbi.

Maana wameiacha sheria ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi,

wamedharau neno la yule Mtakatifu wa Israeli.

25Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwawakia watu wake,

akaunyosha mkono wake dhidi yao, akawachapa,

hata milima ikatetemeka,

maiti zao zikawa kama takataka

katika barabara za mji.

Hata hivyo, hasira yake haikutulia,

mkono wake bado ameunyosha kuwaadhibu.

26Mwenyezi-Mungu analiashiria taifa la mbali;

anawapigia mruzi watu kutoka miisho ya dunia;

nao waja mbio na kuwasili haraka!

27Hawachoki wala hawajikwai;

hawasinzii wala hawalali;

hakuna mshipi wao uliolegea

wala kamba ya kiatu iliyokatika.

28Mishale yao ni mikali sana,

pinde zao zimevutwa tayari.

Kwato za farasi wao ni ngumu kama mawe;

mwendo wa magurudumu ya magari ni kimbunga.

29Askari wao wananguruma kama simba;

wananguruma kama wanasimba

ambao wamekamata mawindo yao

na kuwapeleka mahali mbali

ambapo hakuna awezaye kuwanyanganya.

30Siku hiyo, watanguruma juu ya Israeli

kama mvumo wa bahari iliyochafuka.

Atakayeiangalia nchi kavu

ataona giza tupu na dhiki,

mwanga utafunikwa na mawingu.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania