Yobu 35

Yobu 35

1Kisha Elihu akaendelea kusema:

2“Je, Yobu, unaona jambo hili ni sawa

na kufikiri kinyume cha Mungu

3ukiuliza: ‘Nimepata faida gani

kama sikutenda dhambi?

Nimefaidika kuliko kama ningalitenda dhambi?’

4Mimi nitakujibu wewe,

na rafiki zako pia.

5Hebu zitazame mbingu!

Tazama mawingu yaliyo juu kuliko wewe!

6Ukitenda dhambi, je, Mungu ndiye unayemdhuru?[#Taz Yobu 22:2-3]

Na kama ukizidisha makosa yako, wadhani unamwumiza?

7Kama wewe ni mwema, je, unampatia faida,

au yeye anapokea kitu kutoka kwako?

8Uovu wako utamdhuru binadamu kama wewe,

wema wako utamfaa binadamu mwenzako.

9“Kwa sababu ya udhalimu mwingi watu hulia,

huomba msaada kwa sababu ya mapigo ya wenye nguvu.

10Lakini hakuna asemaye, ‘Yuko wapi Mungu, Muumba wangu,

mwenye kunifanya niwe mchangamfu usiku,

11anayetuelimisha kuliko wanyama,

na kutufanya wenye hekima kuliko ndege!’

12Watu hao huomba msaada lakini Mungu hawajibu,

kwa sababu ya majivuno ya watu waovu.

13Kweli Mungu hasikilizi kilio cha bure;

Mungu Mwenye Nguvu hajali kilio hicho.

14Atakujibu vipi wakati wewe

unasema kwamba humwoni

na kwamba kesi yako iko mbele yake

na wewe unamngojea!

15Sasa, kwa vile Mungu anazuia hasira yake,

wala hajali sana makosa ya watu,

16Yobu unafungua mdomo kusema maneno matupu,

unazidisha maneno bila akili.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania