Maombolezo 3

Maombolezo 3

Adhabu, toba na tumaini

1Mimi ni mtu niliyepata mateso

kwa fimbo ya ghadhabu yake Mungu.

2Amenichukua akanipeleka

mpaka gizani kusiko na mwanga.

3Amenyosha mkono wake dhidi yangu mimi tu,

akanichapa tena na tena mchana kutwa.

4Amenichakaza ngozi na nyama,

mifupa yangu ameivunja.

5Amenizingira na kunizungushia

uchungu na mateso.

6Amenikalisha gizani

kama watu waliokufa zamani.

7Amenizungushia ukuta nisitoroke,

amenifunga kwa minyororo mizito.

8Ingawa naita na kulilia msaada

anaizuia sala yangu isimfikie.

9Njia zangu ameziziba kwa mawe makubwa

amevipotosha vichochoro vyangu.

10Yeye ni kama dubu anayenivizia;

ni kama simba aliyejificha.

11Alinifukuza njiani mwangu,

akanilemaza na kuniacha mkiwa.

12Aliuvuta upinde wake,

akanilenga mshale wake.

13Alinichoma moyoni kwa mishale,

kutoka katika podo lake.

14Nimekuwa kitu cha dhihaka kwa watu wote,

mchana kutwa nimekuwa mtu wa kuzomewa.

15Amenijaza taabu,

akanishibisha uchungu.

16Amenisagisha meno katika mawe,

akanifanya nigaegae majivuni.

17Moyo wangu haujui tena amani,

kwangu furaha ni kitu kigeni.

18Nimewaza “Nimekata tamaa kabisa,

tumaini langu kwa Mwenyezi-Mungu limetoweka.”

19Kukumbuka taabu na kutangatanga kwangu

kwanipa uchungu kama wa nyongo.

20Nayafikiria hayo daima,

nayo roho yangu imejaa majonzi.

21Lakini nakumbuka jambo hili moja,

nami ninalo tumaini:

22Kwamba fadhili za Mwenyezi-Mungu hazikomi,

huruma zake hazina mwisho.

23Kila kunapokucha ni mpya kabisa,

uaminifu wake ni mkuu mno.

24Mwenyezi-Mungu ndiye hazina yangu

hivyo nitamwekea tumaini langu.

25Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wanaomtegemea,

ni mwema kwa wote wanaomtafuta.

26Ni vema mtu kungojea kwa saburi

ukombozi utokao kwa Mwenyezi-Mungu.

27Ni vema mtu kujifunza uvumilivu

tangu wakati wa ujana wake.

28Heri kukaa peke na kimya,

mazito yanapompata kutoka kwa Mungu.

29Yampasa kuinama na kujinyenyekesha,

huenda ikawa tumaini bado lipo.

30Yampasa kumgeuzia shavu mwenye kumpiga,

na kuwa tayari kupokea matusi yake.

31Mwenyezi-Mungu hatatutupa milele.

32Ingawa atufanya tuhuzunike,

atakuwa na huruma tena

kadiri ya wingi wa fadhili zake.

33Yeye hapendelei kuwatesa

wala kuwahuzunisha wanadamu.

34Wafungwa wote nchini

wanapodhulumiwa na kupondwa;

35haki za binadamu zinapopotoshwa

mbele yake Mungu Mkuu,

36kesi ya mtu inapopotoshwa mahakamani,

je, Mwenyezi-Mungu haoni hayo?

37Nani awezaye kuamuru kitu kifanyike

Mwenyezi-Mungu asipopanga iwe hivyo?

38Maafa na mema hutokea tu

kwa amri yake Mungu Mkuu.

39Kwa nini mtu anung'unike,

ikiwa ameadhibiwa kwa dhambi zake?

40Na tupime na kuchunguza mwenendo wetu,

tupate kumrudia Mwenyezi-Mungu.

41Tumfungulie Mungu huko mbinguni

mioyo yetu na kumwomba:

42“Sisi tulikukosea na kukuasi

nawe bado hujatusamehe.

43“Umejizungushia hasira yako ukatufuatia,

ukatuua bila huruma.

44Umejizungushia wingu zito,

sala yeyote isiweze kupenya humo.

45Umetufanya kuwa takataka na uchafu

miongoni mwa watu wa mataifa.

46“Maadui zetu wote wanatuzomea.

47Kitisho na hofu vimetuandama,

tumepatwa na maafa na maangamizi.

48Macho yangu yabubujika mito ya machozi

kwa sababu ya kuangamizwa kwa watu wangu.

49“Machozi yatanitoka bila kikomo,

50mpaka Mwenyezi-Mungu kutoka huko mbinguni

aangalie chini na kuona.

51Nalia na kujaa majonzi,

kuona yaliyowapata kina mama wa mji wangu.

52“Nimewindwa kama ndege

na hao wanichukiao bila sababu.

53Walinitupa shimoni nikiwa hai

na juu yangu wakarundika mawe.

54Maji yalianza kunifunika kichwa,

nami nikafikiri, ‘Huu ni mwisho wangu.’

55“Kutoka chini shimoni

nilikulilia ee Mwenyezi-Mungu.

56Wewe umenisikia nikikulilia:

‘Usiache kusikia kilio changu cha msaada

bali unipatie nafuu.’

57Nilipokuita ulinijia karibu

ukaniambia, ‘Usiogope!’

58“Umenitetea katika kisa changu ee Mwenyezi-Mungu,

umeyakomboa maisha yangu.

59Umeuona uovu niliotendewa ee Mwenyezi-Mungu,

uniamulie kwa wema kisa changu.

60Umeuona uovu wa maadui zangu,

na mipango yao yote ya hila dhidi yangu.

61“Umesikia matukano yao ee Mwenyezi-Mungu,

na mipango yao yote ya hila dhidi yangu.

62Maneno na mawazo ya maadui zangu siku nzima

ni juu ya kuniangamiza mimi.

63Wakati wote, wamekaa au wanakwenda,

mimi ndiye wanayemzomea.

64Uwalipize, ee Mwenyezi-Mungu

kadiri ya hayo matendo yao,

kadiri ya mambo waliyotenda wenyewe.

65Uipumbaze mioyo yao,

na laana yako iwashukie.

66Uwafuatie kwa hasira, uwaangamize,

uwafanye watoweke ulimwenguni.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania