Obadia 1

Obadia 1

1Maono ya Obadia. Mambo aliyosema Bwana Mwenyezi-Mungu kuhusu taifa la Edomu.[#Taz Isa 34:5-17; Yer 49:7-22; Eze 25:12-14; 35:1-15; Amo 1:11-12; Mal 1:2-5]

Mwenyezi-Mungu ataadhibu Edomu

Tumepata habari kutoka kwa Mwenyezi-Mungu;

mjumbe ametumwa kati ya mataifa:

“Inukeni! Twende tukapigane na Edomu!”

2Mwenyezi-Mungu aliambia taifa la Edomu:

“Nitakufanya mdogo miongoni mwa mataifa,

utadharauliwa kabisa na wote.

3Kiburi chako kimekudanganya:

Kwa kuwa mji wako mkuu ni ngome ya miamba imara

na makao yako yapo juu milimani,

hivyo wajisemea,

‘Nani awezaye kunishusha chini?’

4Hata ukiruka juu kama tai,

ukafanya makao yako kati ya nyota,

mimi nitakushusha chini tu.

Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.

5“Kama wezi au wanyang'anyi wangekujia usiku,

je, wasingechukua tu kiasi cha kuwatosha?

Ikiwa wavunaji zabibu wangekujia,

je, wasingekuachia kiasi kidogo tu?

Lakini wewe, adui zako wamekuangamiza kabisa.

6Enyi wazawa wa Esau, mali zenu zimetekwa;

hazina zenu zote zimeporwa!

7Washirika wenzenu wamewadanganya,

wamewafukuza nchini mwenu.

Mliopatana nao wamewashinda vitani,

rafiki wa kutegemewa ndio waliokutegea mitego,

nawe hukuelewa yaliyokuwa yanatendeka.

8Mimi Mwenyezi-Mungu nakuuliza hivi:

Je, siku hiyo, sitawaangamiza wenye hekima kutoka Edomu

na wenye maarifa kutoka mlima Esau?

9Ewe Temani, mashujaa wako watatishika

na kila mtu atauawa mlimani Esau.

Sababu za Edomu kuadhibiwa

10“Kwa sababu ya matendo maovu

mliyowatendea ndugu zenu wazawa wa Yakobo,

mtaaibishwa na kuangamizwa milele.

11Siku ile mlisimama kando mkitazama tu,

wakati wageni walipopora utajiri wao,

naam, wageni walipoingia malango yao

na kugawana utajiri wa Yerusalemu kwa kura.

Kwa hiyo nanyi mlitenda kama wazawa wao.

12Msingalifurahia siku hiyo ndugu zenu walipokumbwa na mikasa;

msingaliwacheka Wayuda

na kuona fahari wakati walipoangamizwa;

msingalijigamba wenzenu walipokuwa wanataabika.

13Msingeliingia katika mji wa watu wangu,

siku walipokumbwa na maafa;

msingelipora mali zao, siku hiyo ya maafa yao.

14Msingelisimama kwenye njia panda

na kuwakamata wakimbizi wao;

wala msingeliwakabidhi kwa adui zao

wale waliobaki hai.

Mungu atayahukumu mataifa

15“Siku inakaribia ambapo mimi Mwenyezi-Mungu

nitayahukumu mataifa yote.

Kama mlivyowatendea wengine, ndivyo mtakavyotendewa,

mtalipwa kulingana na matendo yenu.

16Maana, kama walivyokunywa kikombe cha ghadhabu yangu

kwenye mlima wangu mtakatifu

ndivyo na mataifa jirani yatakavyokunywa;

watakunywa na kupepesuka,

wataangamia kana kwamba hawakuwahi kuwapo duniani.

Waisraeli watashinda

17“Lakini mlimani Siyoni watakuwapo wale waliosalimika

nao utakuwa mlima mtakatifu.

Wazawa wa Yakobo wataimiliki tena nchi iliyokuwa yao.

18Wazawa wa Yakobo watakuwa kama moto

na wazawa wa Yosefu kama miali ya moto.

Watawaangamiza wazawa wa Esau

kama vile moto uteketezavyo mabua makavu,

asinusurike hata mmoja wao.

Mimi, Mwenyezi-Mungu, nimesema.

19Wale wanaokaa Negebu wataumiliki mlima Esau;

wale wanaokaa Shefela wataimiliki nchi ya Wafilisti.

Waisraeli watamiliki nchi za Efraimu na Samaria

na watu wa Benyamini wataimiliki nchi ya Gileadi.

20Waisraeli walio uhamishoni Hala

wataimiliki Foinike hadi Sarepta.

Watu wa Yerusalemu walio uhamishoni Sefaradi

wataimiliki miji ya Negebu.

21Waokoaji watapanda juu ya mlima Siyoni

ili kuutawala mlima Esau;

naye Mwenyezi-Mungu atakuwa ndiye Mfalme.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania