Methali 27

Methali 27

1Usijisifie ya kesho,[#Taz Yak 4:13-16]

hujui nini kitatokea leo mpaka kesho.

2Acha watu wengine wakusifu,

kuliko mdomo wako wewe mwenyewe.

3Jiwe ni zito na mchanga kadhalika,

lakini usumbufu wa mpumbavu ni mzito zaidi.

4Ghadhabu ni katili na hasira huangamiza;

lakini ni nani awezaye kuukabili wivu?

5Afadhali mtu anayekuonya waziwazi,

kuliko yule afichaye upendo.

6Makaripio ya rafiki yaonesha uaminifu,

lakini busu la adui ni udanganyifu.

7Aliyeshiba hata asali huikataa,

lakini kwa mwenye njaa kila kichungu ni kitamu.

8Mtu aliyepotea mbali na kwake,

ni kama ndege aliyepotea mbali na kiota chake.

9Mafuta na manukato huufurahisha moyo,

lakini taabu hurarua roho.

10Usisahau rafiki zako wala wa baba yako.

Ukipatwa na janga usikimbilie kwa nduguyo;

afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali.

11Uwe na hekima mwanangu upate kunifurahisha moyo,

nami sitakosa la kumjibu yeyote anayenilaumu.

12Mwenye busara huona hatari akajificha,

lakini mjinga hujitokeza mbele akaumia.

13Mtu akiahidi mbele yako kumdhamini mgeni, chukua nguo yake;

mfanye awajibike kwa kuwadhamini wageni.

14Amwamkiaye jirani kwa kelele alfajiri,

itaeleweka kwamba amemtakia laana.

15Mke mgomvi daima,

ni sawa na tonatona ya maji siku ya mvua.

16Kumzuia ni sawa na kuzuia upepo,

au kukamata mafuta kwa mkono.

17Chuma hunoa chuma,

kadhalika mtu hufundishwa na wenzake.

18Anayeutunza mtini hula tini,

anayemhudumia bwana wake ataheshimiwa.

19Kama uso ujionavyo wenyewe majini,

ndivyo ujijuavyo mwenyewe moyoni.

20Kuzimu na Uharibifu kamwe havishibi,

kadhalika na macho ya watu hayashibi.

21Ubora wa fedha au dhahabu hupimwa kwa moto,

na mtu hupimwa kutokana na sifa zake.

22Mtwange mpumbavu katika kinu pamoja na nafaka,

lakini hutafaulu kumtenganisha na upumbavu wake.

23Angalia vizuri hali ya mifugo yako;

tunza vizuri wanyama wako.

24Maana utajiri haudumu milele,

wala taji haidumu vizazi vyote.

25Baada ya kukata nyasi na kuzihifadhi,

kata majani toka milimani,

huku nyasi zinachipua upya.

26Kondoo watakupatia sufu kwa mavazi,

mbuzi nao utauza na kujinunulia mashamba;

27watakupa maziwa ya kukutosha wewe na jamaa yako,

na kwa ajili ya watumishi wako wa kike.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania