Zaburi 25

Zaburi 25

Kumwomba Mungu uongozi na ulinzi

1Ee Mwenyezi-Mungu, kwako naielekeza nafsi yangu!

2Nakutumainia wewe, ee Mungu wangu,

usiniache niaibike;

adui zangu wasifurahie kushindwa kwangu.

3Usimwache anayekutumainia apate aibu;

lakini waaibike wote wanaokuasi kwa makusudi.

4Unijulishe njia zako, ee Mwenyezi-Mungu;

unifundishe nifuate unayotaka.

5Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha,

kwani wewe ni Mungu, mwokozi wangu;

ninakutegemea wewe kila siku.

6Uikumbuke huruma yako ee Mwenyezi-Mungu;

uzikumbuke na fadhili zako kuu,

ambazo zimekuwako tangu kale.

7Usikumbuke dhambi na makosa ya ujana wangu;

unikumbuke kadiri ya fadhili zako,

kwa ajili ya wema wako, ee Mwenyezi-Mungu.

8Mwenyezi-Mungu ni mwema na mnyofu,

kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia.

9Huwaongoza wanyenyekevu katika uadilifu;

naam, huwafundisha hao njia yake.

10Mwenyezi-Mungu hutenda kwa fadhili na uaminifu,

kwa wale wanaoshika agano lake na maamuzi yake.

11Kwa ajili ya jina lako, ee Mwenyezi-Mungu,

unisamehe kosa langu kwani ni kubwa.

12Kila mtu anayemcha Mwenyezi-Mungu,

Mwenyezi-Mungu atamfunza njia ya kufuata.

13Mtu wa namna hiyo atafanikiwa daima,

na wazawa wake watamiliki nchi.

14Mwenyezi-Mungu ni rafiki ya wale wamchao;

yeye huwajulisha hao agano lake.

15Namwangalia Mwenyezi-Mungu daima;

yeye atainasua miguu yangu mtegoni.

16Unielekee, ee Mungu, unionee huruma,

maana mimi ni mpweke na mnyonge.

17Uniondolee mahangaiko ya moyoni mwangu;

unitoe katika mashaka yangu.

18Uangalie mateso yangu na dhiki yangu;

unisamehe dhambi zangu zote.

19Angalia jinsi walivyo wengi maadui zangu;

ona jinsi wanavyonichukia kwa ukatili.

20Uyalinde maisha yangu, uniokoe;

nakimbilia usalama kwako,

usikubali niaibike.

21Wema na uadilifu vinihifadhi,

maana ninakutumainia wewe.

22Ee Mungu, uwaokoe watu wako, Israeli;

uwaokoe katika taabu zao zote.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania