The chat will start when you send the first message.
1Dhambi huongea na mtu mwovu,[#Taz Rom 3:18]
ndani kabisa moyoni mwake;
jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake.
2Mwovu hujipendelea mwenyewe,
hufikiri uovu wake hautagunduliwa na kulaaniwa.
3Kila asemacho ni uovu na uongo;
ameacha kutumia hekima na kutenda mema.
4Alalapo huwaza kutenda maovu,
hujiweka katika njia isiyo njema,
wala haachani na uovu.
5Fadhili zako ee Mwenyezi-Mungu zaenea hata mbinguni;
uaminifu wako wafika mawinguni.
6Uadilifu wako ni kama milima mikubwa,
hukumu zako ni kama vilindi vya bahari.
Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wawalinda wanadamu na wanyama
7Jinsi gani zilivyo bora fadhili zako!
Wanadamu hukimbilia kivulini mwa mabawa yako.
8Wawashibisha kwa utajiri wa nyumba yako;
wawanywesha kutoka mto wa wema wako.
9Wewe ndiwe asili ya uhai;
kwa mwanga wako twaona mwanga.
10Uendelee kuwafadhili wale wanaokutambua;
uzidi kuwa mwema kwa wanyofu wa moyo.
11Usikubali wenye majivuno wanivamie,
wala watu waovu wanikimbize.
12Kumbe watendao maovu wameanguka;
wameangushwa chini, hawawezi kuinuka.