Zaburi 63

Zaburi 63

Hamu ya kuwa pamoja na Mungu

1Ee Mungu, wewe u Mungu wangu,

nami nakutafuta kwa moyo;

roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu;

nina kiu kama nchi kavu isiyo na maji.

2Nimetaka kukuona patakatifuni pako,

niione nguvu yako na utukufu wako.

3Fadhili zako ni bora kuliko maisha,

nami nitakusifu kwa mdomo wangu.

4Nitakushukuru maisha yangu yote;

nitainua mikono yangu na kukuomba.

5Roho yangu inafurahi kama kwa karamu na vinono;

kwa shangwe nitaimba sifa zako.

6Niwapo kitandani ninakukumbuka,

usiku kucha ninakufikiria;

7maana wewe umenisaidia daima.

Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

8Roho yangu inaambatana nawe kabisa,

mkono wako wa kulia wanitegemeza.

9Lakini hao wanaotaka kuyaangamiza maisha yangu,

watatumbukia chini kwenye makao ya wafu.

10Watauawa kwa upanga,

watakuwa chakula cha mbweha.

11Lakini mfalme atafurahi kwa sababu ya Mungu;

wanaoahidi kwa jina la Mungu watamsifu,

lakini vinywa vya waongo vitafumbwa.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania