Zaburi 75

Zaburi 75

Mungu hakimu

1Tunakushukuru, ee Mungu,

tunakushukuru!

Tunatangaza ukuu wa jina lako

na kusimulia juu ya matendo yako makuu.

2Mungu asema: “Mimi nimeweka wakati maalumu!

Wakati huo nitahukumu kwa haki.

3Nchi ikitetemeka na vyote vilivyomo,

mimi ndiye ninayeitegemeza misingi yake.

4Nawaambia wenye kiburi:

‘Acheni kujigamba’;

na waovu: ‘Msioteshe pembe za kiburi!

5Msijione kuwa watu wa maana sana,

wala kusema maneno ya majivuno.’”

6Hukumu haitoki mashariki au magharibi;

wala haitoki nyikani au mlimani.

7Mungu mwenyewe ndiye hakimu;

humshusha mmoja na kumkweza mwingine.

8Mwenyezi-Mungu, anashika kikombe mkononi,

kimejaa divai kali ya hasira yake;

anaimimina na waovu wote wanainywa;

naam, wanainywa mpaka tone la mwisho.

9Lakini mimi nitafurahi milele,

nitamwimbia sifa Mungu wa Yakobo.

10Atavunja nguvu zote za watu waovu;

lakini nguvu za waadilifu ataziimarisha.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania