Wimbo Ulio Bora 5

Wimbo Ulio Bora 5

Bwana arusi

1Naingia bustanini mwangu,

dada yangu, bi arusi.

Nakusanya manemane na viungo,

nala sega langu la asali,

nanywa divai yangu na maziwa yangu.

Bibi arusi

Kuleni enyi marafiki, kunyweni;

kunyweni sana wapendwa wangu.

Shairi la nne

Bibi arusi

2Nililala, lakini moyo wangu haukulala.

Sauti ya mpenzi wangu anabisha hodi.

Bwana arusi

“Nifungulie, dada yangu mpenzi wangu, bibiarusi wangu,

hua wangu, usiye na kasoro.

Kichwa changu kimelowa umande

na nywele zangu manyunyu ya usiku.”

Bibi arusi

3Nimekwisha yavua mavazi yangu,

nitayavaaje tena?

Nimekwisha nawa miguu yangu,

niichafueje tena?

4Hapo mpenzi wangu akaugusa mlango,

moyo wangu ukajaa furaha.

5Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu.

Mikono yangu imejaa manemane,

na vidole vyangu vyadondosha manemane,

nilipolishika komeo kufungua mlango.

6Nilimfungulia mlango mpenzi wangu,

lakini kumbe, alikuwa amekwisha toweka.

Moyo wangu ulifurahi alipokuwa akizungumza!

Nilimtafuta, lakini sikumpata;

nilimwita, lakini hakuniitikia.

7Walinzi wa mji waliniona,

walipokuwa wanazunguka mjini;

wakanipiga na kunijeruhi;

nao walinzi wa lango wakaninyanganya shela langu.

8Nawasihini, enyi wanawake wa Yerusalemu,

mkimwona mpenzi wangu,

mwelezeni kwamba naugua kwa mapenzi!

Wanawake

9Ewe upendezaye kuliko wanawake wote!

Kwani huyo mpenzi wako ana nini cha zaidi ya mpenzi mwingine,

hata utusihi kwa moyo kiasi hicho?

Bibi arusi

10Mpenzi wangu ni mzuri na mwenye nguvu,

mashuhuri miongoni mwa wanaume elfu kumi.

11Kichwa chake kizuri kama dhahabu safi,

nywele zake ni za ukoka,

nyeusi ti kama kunguru.

12Macho yake ni kama ya hua kandokando ya kijito,

ni kama njiwa waliooga maziwa kando ya kijito.

13Mashavu yake ni kama matuta ya rihani

kama bustani iliyojaa manukato na manemane.

Midomo yake ni kama yungiyungi,

imelowa manemane kwa wingi.

14Mikono yake imewekwa bangili za dhahabu,

amevalia johari za Tarshishi.

Kiwiliwili chake ni kama pembe za ndovu

zilizopambwa kwa vito vya johari ya rangi ya samawati.

15Miguu yake ni kama nguzo za alabasta

zilizosimikwa katika misingi ya dhahabu.

Umbo lake ni kama Lebanoni,

ni bora kama miti ya mierezi.

16Kinywa chake kimejaa maneno matamu,

kwa ujumla anapendeza.

Basi, hivyo ndivyo alivyo mpenzi wangu,

naam, ndivyo alivyo rafiki yangu,

enyi wanawake wa Yerusalemu.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania