Sira 12

Sira 12

1Ukitaka kutenda wema chagua mtu wa kumtendea;

nawe utapata shukrani kwa wema wako.

2Mtendee wema mcha Mungu nawe utatuzwa;

utatuzwa na mtu huyo, au hakika na Mungu Mkuu.

3Hakuna jema litakalomjia mtu anayedumu katika uovu,

au mtu ambaye anakataa kutoa zaka.

4Wape msaada watu wamchao Mungu,

lakini usiwasaidie wenye dhambi.

5Watendee wema watu wanyenyekevu

lakini usiwape kitu wasiomcha Mungu.

Usiwape chakula chochote kile,

la sivyo watakitumia kukuangusha;

nawe, ukalipwa uovu maradufu

kwa wema uliowatendea hao.

6Hata Mungu Mkuu huwachukia wenye dhambi,

naye atawaadhibu hao wasiomcha Mungu.

7Mpe msaada mtu mwema,

lakini usimsaidie mwenye dhambi.

8Rafiki haonekani wakati wa fanaka;

na katika shida hutakosa kumjua adui ni nani.

9Mtu anapofanikiwa maadui zake huhuzunika,

lakini katika shida hata rafiki yake hujitenga naye.

10Kamwe usimwamini adui;

uovu wake uko kama kutu ya shaba.

11Hata kama ananyenyekea na kuinama mbele yako

jichunge na kuchukua tahadhari dhidi yake.

Yeye ni kama kioo kinachopata kutu

kama huendelei kukisafisha.

12Usimweke adui karibu nawe,

la sivyo atakupindua na kuchukua mahali pako.

Usimkalishe kwenye mkono wako wa kulia

la sivyo, atachukua kiti chako cha heshima;

na mwishowe utatambua ukweli wa maneno yangu,

nawe utajuta kutokana na hayo niliyosema.

13Mchezea nyoka akiumwa hahurumiwi na mtu yeyote!

Kadhalika na mtu anayewakaribia wanyama wakali!

14Hivyo, hakuna amhurumiaye anayeshiriki na wenye dhambi

na kujihusisha na dhambi zake.

15Mwenye dhambi atakaa nawe kwa kitambo tu,

lakini ukipatwa na matatizo atakukimbia.

16Adui ataongea nawe maneno matamu,

lakini moyoni mwake atapanga kukutupa shimoni.

Adui atatoa machozi mengimengi,

lakini akipata nafasi, atatimiza haja yake ya kukuua.

17Ukipatwa na maafa utamkuta hapo anakungojea,

akijidai kwamba anakusaidia, atakutegea kukumaliza.

18Atatikisa kichwa na kupiga makofi;

atanongoneza mengi na kuwa mtu mwingine kabisa.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania