Sira 15

Sira 15

1Ndivyo afanyavyo mtu anayemcha Bwana;

mtu ashikaye sheria zake atampata Hekima.

2Hekima atakuja kumlaki kama mama,

atamkaribisha kama bibi arusi wake.

3Atamlisha chakula cha maarifa,

atamnywesha maji ya Hekima.

4Mtu huyo atamwegemea hekima na hataanguka;

atamtegemea na hataaibishwa.

5Hekima atamtukuza juu ya jirani zake;

na katikati ya mkutano atamwezesha kusema.

6Mtu huyo atapata furaha na fahari ya shangwe,

na jina lake kukumbukwa daima.

7Lakini wapumbavu hawawezi kumpata Hekima

wenye dhambi hawatamwona.

8Hekima yu mbali na wenye kiburi,

na waongo hawataweza kamwe kumfikiria.

9Mwenye dhambi hafai kuimba nyimbo za sifa,

maana hajapelekewa kutoka kwa Bwana.

10Nyimbo za sifa yabidi ziimbwe kwa hekima,

hapo Bwana atazifanikisha.

Kuchagua kwa hiari

11Usiseme: “Bwana ndiye aliyesababisha nianguke”,

maana yeye hawezi kusababisha jambo analochukia.

12Usiseme: “Yeye ndiye aliyenipotosha”,

maana yeye hahitaji msaada wa mwenye dhambi.

13Bwana anayachukia machukizo yote;

hata wale wanaomcha wanayachukia hayo.

14Bwana ndiye aliyemwumba binadamu mwanzoni,

akampa uwezo wa kujiamulia mambo yake mwenyewe.

15Ukitaka, unaweza kuzitii amri,

kuishi kwa uaminifu au la, ni chaguo lako.

16Bwana ameweka mbele yako moto na maji:

Nyosha mkono wako, ujichukulie upendacho.

17Binadamu amewekewa mbele yake uhai na kifo;

kile atakachochagua atapewa.

18Maana hekima ya Bwana ni kuu.

Yeye ni mwenye nguvu na anaona yote.

19Bwana huwaangalia kwa wema wale wanaomcha;

yeye anajua kila kitu afanyacho binadamu.

20Yeye hajamwamuru yeyote kutomcha Mungu,

wala hajamruhusu mtu yeyote kutenda dhambi.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania