Sira 2

Sira 2

Uaminifu kwa Mungu

1Mwanangu, ukienda kumtumikia Bwana,

uwe tayari kupata majaribu.

2Uwe mnyofu wa moyo na nia moja;

na usihangaike wakati wa taabu.

3Ambatana na Bwana wala usimwache kamwe,

nawe utafanikiwa mwishoni mwa maisha yako.

4Uyapokee yote yatakayokupata,

hata ukiaibishwa uwe na uvumilivu,

5maana dhahabu hujaribiwa kwa moto

na watu wanaokubaliwa na Mungu kwa tanuri ya aibu.

6Mtegemee Mungu, naye atakusaidia,

shika njia nyofu na kumtumaini yeye.

7Enyi mnaomcha Bwana ngojeni huruma yake,

msigeuke upande, msije mkaanguka.

8Enyi mnaomcha Bwana, mtumainini yeye,

nanyi hamtakosa tuzo lenu.

9Enyi mnaomcha Bwana muwe na tumaini la fanaka;

mtazamie kupata furaha ya milele na huruma.

10Fikirini juu ya vizazi vilivyopita mkajiulize:

“Nani aliyepata kumtegemea Bwana, akaaibika?

Nani aliyedumu katika kumcha Bwana, akaachwa naye?

Nani aliyemwomba Bwana, akasahauliwa naye?

11Maana Bwana ni mpole na mwenye huruma.

Yeye husamehe watu dhambi

na kuokoa wakati wa shida.

12“Ole wake mtu asiye imara moyoni na anayelegalega!

Ole wake mwenye dhambi anayefuata njia mbili!

13Ole wake mtu aliye mwoga moyoni asiye na tumaini!

Mtu wa namna hiyo hatalindwa.

14Ole wenu nyinyi mliopoteza matumaini yenu;

mtafanya nini Mungu atakapofika kuwaadhibu?

15Wanaomcha Bwana hawaachi kamwe kutii maneno yake;

wale wanaompenda huzifuata njia zake.

16Wanaomcha Bwana hutafuta kumpendeza,

wale wanaompenda huzingatia sheria yake.

17Wanaomcha Bwana wako tayari daima kumtumikia,

Wao hunyenyekea mbele yake na kusema:

18Tujiweke mikononi mwa Bwana

na sio mikononi mwa watu ambao hufa.

Maana kama ulivyo ukuu wake

ndivyo pia huruma yake.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania