Sira 23

Sira 23

1Ee Bwana, Baba na Mtawala wa maisha yangu,

usiniache niangamizwe na maneno yangu,

wala usikubali nifanye makosa kwa sababu yake!

2Laiti mawazo yangu yangechapwa fimbo,

na moyo wangu ungefunzwa nidhamu ya busara.

Hapo singeachwa kukosolewa makosa yangu,

na dhambi yangu yoyote kuadhibiwa;

3ili makosa yangu yasiongezeke zaidi,

na dhambi zangu zisiwe nyingi.

Hapo sitaanguka mikononi mwa maadui zangu;

maadui zangu hawatafurahi dhidi yangu.

4Ee Bwana, Baba na Mtawala wa maisha yangu,

nakuomba nisiwe na majivuno.

5Nakuomba uniondolee tamaa mbaya.

6Usiruhusu niwe mchoyo au niwe na tamaa mbaya.

Usiniache kutawaliwa na tamaa hizo mbaya.

Kuapa

7Wanangu, sikilizeni mafunzo kuhusu kusema vizuri;

mtu atakayefuata hayo hatanaswa mitegoni.

8Mwenye dhambi hukamatwa kwa maneno yake,

wafidhuli na wenye kiburi hunaswa nayo.

9Usiuzoeshe mdomo wako kuapa,

wala kuzoea kutaja jina la Mungu Mtakatifu.

10Maana kama mtumishi anayechunguliwa sana,

naye hatakosa kuchapwa viboko,

vivyo hivyo anayeapa daima kwa kutaja jina la Mungu,

hakika hataepukana na dhambi.

11Mtu anayeapa kwa wingi amejaa uovu,

na majanga hayatatoka nyumbani kwake.

Akikiuka kiapo chake atakuwa na hatia;

na akikidharau atakuwa na hatia maradufu.

Kama ameapa bure hatafikiriwa kuwa hana kosa,

hata hivyo ni mkosaji tu, ataadhibiwa;

na nyumbani kwake kutakuwa na maafa daima.

Mazungumzo machafu

12Kuna namna ya kusema ambayo ni kama kifo.

Hiyo na isiwepo kamwe katika wazawa wa Yakobo.

Wamchao Mungu watayaepa makosa hayo yote

hawatagaagaa katika dhambi.

13Usiuzoeshe mdomo wako kusema machafu,

maana kusema hivyo kunahusika na dhambi.

14Unapoketi miongoni mwa wakuu

kumbuka baba yako na mama yako,

usije ukawasahau mbele ya hao wakuu,

ukaonekana kuwa mpumbavu kwa tabia yako.

Hapo utatamani kuwa heri usingelizaliwa

na kuilaani siku ile ulipozaliwa.

15Mtu aliyezoea kutumia lugha chafu

kamwe hatakuwa na nidhamu maishani.

Zinaa

16Watu wa namna mbili hurudiarudia dhambi,

na namna ya tatu husababisha ghadhabu ya Mungu.

Mtu anawaka tamaa kama moto

na hawezi kupoa mpaka imezimwa.

Mtu anakuwa na tamaa kuzini na mwili wake mwenyewe

na hataacha mpaka yeye mwenyewe ameteketezwa.

17Kwa mzinzi, kila cha kula ni kitamu,

hatachoka nacho mpaka amekufa!

18Mtu anavunja nadhiri yake ya ndoa

na kujisemea: “Nani ananiona?

Giza limenizunguka na ukuta umenificha!

Hakuna mtu anayeniona,

ya nini niogope?

Mungu Mkuu hataona dhambi yangu!”

19Woga wa mtu huyo ni kwa watu tu.

Hajui kuwa macho ya Bwana ni maangavu mara elfu kumi kuliko jua.

Yanaziona njia zote za binadamu,

hata zile sehemu zote zilizofichika.

20Kabla ulimwengu haujaumbwa, ulijulikana kwake;

hata baada ya ulimwengu kumalizika kuumbwa.

21Mtu huyo ataadhibiwa mji wote ukitazama,

atakamatwa wakati ambapo hatazamii kabisa.

22Ndivyo ilivyo pia kwa mwanamke anayemwacha mumewe,

akazaa watoto na mwanamume mwingine.

23Kwanza, mwanamke huyo amekaidi sheria ya Mungu Mkuu;

pili, amefanya kosa dhidi ya mumewe;

na tatu, amefanya uzinzi kwa umalaya wake,

akazaa watoto kwa mwanamume mwingine.

24Yeye mwenyewe ataletwa mbele ya baraza,

na atakabiliwa na adhabu kuhusu watoto wake.

25Watoto wake hawatadumu imara,

chipukizi hao wake hawatakuwa na matunda.

26Ataacha duniani kumbukumbu la laana;

aibu aliyoifanya haitafutwa kamwe.

27Wale watakaoachwa hai baada yake

watatambua kuwa hakuna lililo bora kuliko kumcha Bwana,

na hakuna kilicho kitamu kuliko kutii amri za Bwana.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania