Sira 30

Sira 30

Malezi

1Mzazi ampendaye mwanawe, atamrudi mara kwa mara,

ili amwonee fahari jinsi atakavyokua.

2Amfunzaye mwanawe nidhamu,

baadaye atafaidika naye.

Atajivunia mwanawe mbele ya wanaofahamiana naye.

3Anayemfundisha mwanawe atawafanya maadui zake waone wivu,

na kujivunia mwanawe mbele ya rafiki zake.

4Hata kama baba yake amekufa atakuwa kama hakufa,

maana ameacha nyuma mtoto anayefanana naye.

5Baba alipokuwa hai alifurahi kuwa pamoja naye,

na akifa hana haja ya kusikitika.

6Baba amemwacha nyuma atakayelipiza kisasi maadui zake,

na atakayelipa wema wa rafiki zake.

7Anayemharibu mwanawe, atakuwa na kazi ya kufunga vidonda,

na kwa kila kilio moyo wake utashtuka.

8Farasi aliyezoezwa vibaya atakuwa mkaidi,

na mtoto asiyefunzwa nidhamu atageuka kuwa mkaidi.

9Mbembeleze sana mtoto naye atakutisha,

chezacheza naye, naye atakusikitisha.

10Usichekecheke naye kama hupendi kulia naye baadaye;

matokeo yake mwishoni itakuwa kusaga meno.

11Usimruhusu kufanya apendavyo alipo bado mtoto,

na wala usiache kumkosoa anapokosa.

12Mfanye awe na utii angali bado mtoto,

mtandike wakati alipo bado kijana;

la sivyo, atakuwa mkaidi na kuacha kukutii,

na kukuhuzunisha mno rohoni.

13Mfunze mwanao nidhamu na kuwa mvumilivu,

ili usije ukaaibishwa na aibu yake.

Afya

14Afadhali maskini mwenye afya na nguvu mwilini,

kuliko tajiri anayeteseka mwilini mwake.

15Afya na nguvu ni bora kuliko dhahabu;

mwili wenye nguvu ni bora kuliko utajiri mwingi.

16Hakuna utajiri ulio bora kuliko afya ya mwili,

na hakuna furaha iliyo bora kuliko furaha ya moyoni.

17Afadhali kifo kuliko maisha ya taabu,

na pumziko la milele kuliko ugonjwa wa kudumu.

18Kumpa chakula bora mtu asiyeweza kula

ni kama kuweka chakula juu ya kaburi:

19Je, sadaka yafaa nini kwa sanamu

ambayo haiwezi kula wala kunusa?

Hivyo ndivyo alivyo mtu anayeteswa na Bwana.

20Mtu huyo huona kwa macho yake na kuguna,

kama towashi anayemkumbatia msichana na kuguna.

Furaha na huzuni

21Usijiachilie kupata huzuni,

wala usijiumize mwenyewe kwa makusudi.

22Furaha ya moyo ni uhai wa mtu;

furaha ndiyo inayompa maisha marefu.

23Jifurahishe na kuwa na utulivu wa moyo;

weka huzuni mbali nawe.

Maana huzuni imewaangamiza wengi,

wala haina faida kwa mtu yeyote.

24Wivu na hasira hufupisha maisha,

mahangaiko humfanya mtu azeeke upesi.

25Mwenye moyo mkunjufu na mwema,

atachukua hadhari juu ya chakula anachokula.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania