Sira 48

Sira 48

Elia

1Kisha alizuka nabii Elia kama moto;

na maneno yake yaliwaka kama mwenge.

2Aliwaletea watu njaa,

na kwa bidii yake ya kumpenda Mungu akawafanya wawe wachache.

3Kwa neno la Bwana alizifunga mbingu,

na mara tatu akaleta moto.

4Kweli ewe Elia ulitukuka sana kwa matendo yako ya ajabu!

Hakuna mtu anayestahili kujivuna kama wewe?

5Wewe ulimfufua maiti;

kwa neno la Mungu Mkuu ukamwondoa ahera.

6Uliwaporomosha wafalme na kuwaangamiza;

na watu maarufu ukawafanya wawe wagonjwa.

7Wewe ulisikia makaripio huko Sinai,

na tangazo la adhabu huko Horebu.

8Ulimpaka mafuta mfalme awaadhibu watu,

na manabii wa kushika mahali pako.

9Ulichukuliwa mbinguni kwa kimbunga cha moto,

katika gari la farasi wa moto.

10Imeandikwa kuwa ulikuwa tayari kila wakati wake,

kuituliza ghadhabu ya Mungu kabla haijalipuka kwa wingi,

ukamfanya baba na mtoto kupatana,

na kuyarekebisha makabila ya Yakobo.

11Heri wale waliokuona wakafariki;

lakini heri yako wewe zaidi maana waishi.

Elisha

12Elia alipotoweka katika kimbunga

Elisha alijazwa nguvu za Elia.

Maisha yake yote hakutetemeka mbele ya mfalme,

wala hakuna mtu yeyote aliyekuwa na uwezo juu yake.

13Hakuna jambo lililokuwa gumu kwake,

na alipokwisha kufa mwili wake ulitoa unabii.

14Kama alivyotenda maajabu akiwa hai,

hata alipokwisha kufa alitenda maajabu.

15Hata kwa hayo yote watu hawakutubu.

Hawakuziacha dhambi zao,

mpaka wakachukuliwa mateka mbali na makwao,

wakatawanywa duniani kote.

Watu waliobaki nchini walikuwa wachache sana,

walitawaliwa na wazawa wa Daudi.

16Baadhi yao walimpendeza Bwana,

lakini wengine walizidi kutenda dhambi.

Hezekia

17Hezekia aliujengea ngome mji wake,

na kuleta maji ndani kwa mfereji.

Alichimba mtaro kwa chuma kwenye mwamba mgumu,

na kujenga mabawa ya maji.

18Katika siku zake Senakeribu alimshambulia,

akamtuma mkuu wa vikosi vyake,

akaushambulia mji wa Siyoni,

na kujigamba sana kwa kiburi.

19Kisha mioyo ya Waisraeli ikadunda na mikono ikatetemeka,

wakawa katika taabu kama mwanamke anayejifungua.

20Lakini walimwita Bwana mwenye huruma,

wakimwinulia mikono yao.

Naye Mtakatifu akawasikia mara kutoka mbinguni,

akawakomboa kwa mkono wa Isaya.

21Bwana akaipiga kambi ya Waashuru,

na malaika wake akawafutilia mbali.

22Hezekia alitenda mema

akazingatia nyayo za Daudi, babu yake,

kama alivyoamuru nabii Isaya

ambaye aliaminika kabisa katika maono yake.

23Nyakati zake Isaya jua lilirudi nyuma,

akayarefusha maisha ya mfalme.

24Kwa nguvu za roho aliyaona mambo ya mwisho,

akawafariji waliokuwa wanaomboleza mjini Siyoni.

25Aliwafunulia mambo yatakayotukia mwishoni,

akawaambia mambo ya siri kabla ya kutukia kwake.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania