The chat will start when you send the first message.
1Kumkumbuka Yosia ni kama mchanganyiko wa ubani,
ambao umechanganywa na fundi stadi,
ni mtamu kama asali kwa kila mtu,
ni kama muziki kwenye karamu ya pombe.
2Aliongozwa sawa kuwaongoa watu,
akayangolea mbali machukizo yao ya uovu.
3Alikuwa mwaminifu kabisa kwa Bwana!
Wakati watu walipokuwa waovu,
yeye aliimarisha utendaji wa mema.
4Isipokuwa Daudi, Hezekia na Yosia,
wafalme wengine walitenda dhambi sana,
maana waliiacha sheria ya Mungu Mkuu,
wafalme wa Yuda, mpaka wa mwisho.
5Uwezo wao waliwaachia watu wengine,
na heshima yao wakawapa taifa la kigeni
6ambalo liliuteketeza kwa moto mji mteule wa hekalu,
likaiacha mitaa yake kuwa mitupu,
kulingana na neno la Yeremia.
7Maana walimtesa Yeremia,
ingawa alikuwa amewekwa wakfu kuwa nabii kabla ya kuzaliwa,
angoe, aharibu na kuangamiza,
na pia ajenge tena na kupanda.
8Ezekieli ndiye aliyeona maono ya utukufu,
ambayo Mungu alimwonesha juu ya gari la viumbe wenye mabawa.
9Maana Mungu aliwakumbuka maadui zake kwa tufani,
lakini akawatendea mema wale walioishi maisha yao vizuri.
10Mifupa ya manabii kumi na wawili na iimarike huko kaburini;
maana waliwatia moyo watu wa Yakobo,
na kuwakomboa kwa kuwapa tumaini thabiti.
11Tutamsifu Zerubabeli namna gani?
Yeye alikuwa pete ya mhuri katika mkono wa kulia!
12Kadhalika na Yoshua mwana wa Yozadaki.
Wakati wao, walijenga madhabahu,
na kusimika hekalu takatifu
ambalo utukufu wake wadumu milele.
13Ukumbusho wa Nehemia ni wa kudumu.
Yeye alitujengea tena kuta zilizoanguka,
akasimika tena malango na mifumo,
na kujenga upya nyumba zilizoharibiwa.
14Duniani hakuna aliyeumbwa kama Henoki alivyokuwa,
maana yeye alichukuliwa kutoka duniani.
15Na pia hakuna mtu aliyezaliwa duniani kama Yosefu alivyokuwa;
na mifupa yake inatunzwa.
16Shemu na Sethi waliheshimiwa na watu wao,
naye Adamu anaheshimika kuliko viumbe vyote hai duniani.