Sira 50

Sira 50

Simoni

1Aliyekuwa mkuu wa ndugu zake na fahari ya watu wake,

ni Simoni, kuhani mkuu, mwana wa Onia.

Katika maisha yake alilijenga upya hekalu,

na kulijengea ngome.

2Aliweka msingi wa kuta mbili za ua wa hekalu.

3Wakati wake kisima cha maji kilichimbwa,

hifadhi ya maji kubwa kama bahari.

4Alifikiria namna ya kuwaokoa watu wasiangamie,

akauimarisha mji kuukinga na mashambulizi.

5Jinsi gani alivyoheshimika akizungukwa na watu,

alipokuwa akitoka mahali patakatifu ndani.

6Alikuwa kama nyota ya asubuhi mawinguni,

alikuwa kama mwezi mpevu.

7Alikuwa kama jua linapoangaza juu ya hekalu la Mungu Mkuu,

kama upinde wa mvua unaongara katika mawingu.

8Alikuwa kama waridi wakati wa mazao ya kwanza,

kama yungiyungi kando ya kijito,

kama chipukizi mlimani Lebanoni wakati wa kiangazi,

9kama ubani katika moto ndani ya chetezo,

kama chombo cha dhahabu iliyofuliwa,

kilichopambwa kwa kila aina ya mawe ya thamani.

10Alikuwa kama mzeituni unapotoa matunda yake,

kama mberoshi mrefu mpaka mawinguni.

11Alipovaa mavazi yake ya fahari,

alipokwenda kwenye madhabahu matakatifu,

akiwa amevalia mavazi yake kikamilifu,

aliufanya ukumbi wa hekalu uwe na utukufu.

12Makuhani walipompa mafungu yake ya tambiko,

akiwa amesimama karibu na madhabahu,

amezungukwa na ndugu zake kama taji,

alikuwa kama mwerezi mchanga mlimani Lebanoni.

Ndugu zake walimzunguka kama mtende na matawi yake,

13yaani wazawa wote wa Aroni,

wakiwa wamevaa mavazi yao yenye utukufu,

wakiwa na tambiko za matoleo kwa Bwana mikononi,

wamesimama mbele ya jumuiya yote ya Israeli.

14Alipomaliza huduma yake madhabahuni,

na kuzipanga tambiko za Mungu Mkuu, Mwenye Nguvu,

15alinyosha mkono akachukua kikombe,

akaimimina divai kwenye msingi wa madhabahu,

ikiwa ni tambiko ya kinywaji,

impendezayo Mungu Mkuu, mfalme wa wote.

16Kisha wazawa wa Aroni, walipiga kelele,

na kupiga tarumbeta zao za fedha,

wakitangaza kuweko kwake Mungu Mkuu.

17Ndipo watu wote pamoja walifanya haraka,

wakasujudu na kumwabudu Bwana wao,

Mungu Mwenye Nguvu, Mungu Mkuu.

18Nao waimbaji wakamsifu kwa sauti zao,

kwa muziki mtamu na tuni kamili.

19Nao watu wakamsihi Bwana Mungu Mkuu,

wakamwomba yeye mwenye huruma

mpaka utaratibu wa kumwabudu Bwana ulipokwisha.

Ndivyo walivyokamilisha ibada yake.

20Kisha Simoni akatoka, akainua mikono yake

juu ya jumuiya yote ya Israeli,

ili kutamka baraka za Bwana kwa kinywa chake,

na kulitukuza jina lake.

21Nao wakasujudu kwa mara ya pili,

kupokea baraka za Mungu aliye juu ya yote.

Mausia

22Sasa msifuni Mungu wa wote,

ambaye hufanya makuu kila mahali;

ambaye hutunza maisha yetu tangu kuzaliwa,

na kututendea kadiri ya huruma zake.

23Na atupe furaha ya moyoni,

na kutujalia amani siku zetu katika Israeli

kama vile nyakati za kale.

24Huruma yake na iwe kati yetu;

yeye na atukomboe katika siku zetu.

25Kuna mataifa mawili ambayo nayachukia,

na la tatu halifai hata kuitwa taifa.

26Wakazi wa mlima Seiri na Wafilisti,

na wale watu wapumbavu wanaoishi Shekemu.

Maneno ya mwisho

27Nimeandika katika kitabu hiki

mafundisho ya hekima na maarifa.

Mimi ni Yoshua mwana wa Sira mwana wa Eleazari wa Yerusalemu

ambaye moyoni mwangu nimebubujika hekima.

28Heri mtu anayeyatafakari mambo hayo;

naye ayawekaye moyoni atapata hekima.

29Maana atakayeyatenda ataimarika daima,

kwa kuwa kumcha Bwana ni uhai.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania