The chat will start when you send the first message.
1Hawa ndio wana wa mfalme Daudi waliozaliwa wakati alipokuwa huko Hebroni:
Amnoni, mzaliwa wake wa kwanza; mama yake aliitwa Ahinoamu, Myezreeli; wa pili Danieli ambaye mama yake alikuwa Abigaili, Mkarmeli;
2wa tatu alikuwa Absalomu, ambaye mama yake alikuwa Maaka, bintiye Talmai mfalme wa Geshuri; wa nne alikuwa Adoniya, ambaye mama yake alikuwa Hagithi;
3wa tano alikuwa Shefatia, ambaye mama yake alikuwa Abitali; na wa sita alikuwa Ithreamu, ambaye mama yake alikuwa Egla.
4Wote sita, walizaliwa Hebroni ambako Daudi alitawala kwa muda wa miaka saba na nusu. Huko Yerusalemu, alitawala kwa muda wa miaka thelathini na mitatu.[#3:1-4 Hebroni ulikuwa mji mkuu wa utawala wa Daudi wakati alipokuwa mfalme wa Yuda kwa muda wa miaka saba na nusu kabla ya kuwa mfalme wa Waisraeli. Mji huu ulikuwa yapata kilomita thelathini na mbili kusini-magharibi ya Yerusalemu. Hebroni ni mojawapo ya miji ya zamani sana ukiwa umekaliwa tangu yapata mwaka 1600 K.K. Abrahamu alikaa huko baada ya kutengana na Lutu (Mwa 13:14-18), na huko Hebroni ndiko Absalomu alikoanzia uasi wake dhidi ya baba yake, Daudi (2Sam 15:7-12).]
5Wafuatao ni wana wa mfalme Daudi alipokuwa Yerusalemu: mkewe Bathshua, bintiye Amieli, alimzalia wana wanne: Himea, Shobabu, Nathani na Solomoni.[#3:5 Katika 2Sam 12:24 (Kiebrania) anatajwa kwa jina Bathsheba. Daudi alimwoa Bathsheba, mkewe Uria, baada ya kufanya mpango Uria auawe vitani. Mtoto aliyezaliwa kwa Daudi na Bathsheba alikufa. Lakini mtoto wao wa pili yaani Solomoni alipata kuwa mfalme baada ya Daudi, baba yake.]
6Na mbali na hao alikuwa na wana wengine tisa: Ibhari, Elishua, Elifaleti,
7Noga, Nefegi, Yafia,
8Elishama, Eliada na Elifeleti.
9Hao wote walikuwa wana wa Daudi, mbali na wale wengine waliozaliwa na masuria wake. Daudi alikuwa na binti pia, aliyeitwa Tamari.[#3:9 Huyu alikuwa dada yake Absalomu. Bila shaka Daudi alikuwa na binti wengi, lakini huyu anatajwa hapa kwa ajili ya kisa kilichotokea kati yake na Amnoni (rejea 2Sam 13:1-39; 14:27).]
10Wazawa wa mfalme Solomoni: Solomoni alimzaa Rehoboamu, aliyemzaa Abiya, aliyemzaa Asa, aliyemzaa Yehoshafati,
11aliyemzaa Yehoramu, aliyemzaa Ahazia, aliyemzaa Yoashi,
12aliyemzaa Amazia, aliyemzaa Uzia, aliyemzaa Yothamu,
13aliyemzaa Ahazi, aliyemzaa Hezekia, aliyemzaa Manase,
14aliyemzaa Amoni, aliyemzaa Yosia.
15Yosia alikuwa na wana wanne: Yohanani, mzaliwa wake wa kwanza, wa pili Yehoyakimu, wa tatu Sedekia na wa nne Shalumu.[#3:10-16 Rehoboamu alikuwa mfalme wa kwanza (931-913) na Sedekia wa mwisho (598-587) miongoni mwa wafalme wa utawala wa kusini, yaani Yuda, baada ya mgawanyiko uliotukia mwaka 931 K.K. ambao ulisababisha kuwa na falme mbili — Israeli na Yuda. Jina la Sedekia la kwanza lilikuwa Matania. “Yohanani” (aya 15) na “Sedekia” (aya 16) hawajulikani isipokuwa kama huyu “Sedekia” ni sawa na “Sedekia” wa 3:15 jambo ambalo linafanya aya hizi mbili kuwa ngumu kuzifafanua.]
16Yehoyakimu alikuwa na wana wawili: Yekonia na Sedekia.
17Wana wa Yekonia aliyechukuliwa mateka na Wababuloni walikuwa saba: Shealtieli,
18Malkiramu, Pedaya, Shenazari, Yekamia, Hoshama na Nedabia.
19Wana wa Pedaya walikuwa Zerubabeli na Shimei. Zerubabeli alikuwa na wana wawili: Meshulamu na Hanania, na binti mmoja, jina lake Shelomithi.[#3:17-19 Mwandishi wa Mambo ya Nyakati hapa anaendelea na orodha ya wazawa wa Daudi baada ya kurudi kwa Waisraeli kutoka Babuloni yapata mwaka 538 K.K. Zerubabeli anaitwa mwana wa Shealtieli. Alikuwa gavana kule Yerusalemu na aliwasimamia watu wakati wa kujenga upya hekalu la Yerusalemu (Hag 1:2).]
20Zerubabeli pia alikuwa na wana wengine watano: Hashuba, Oheli, Berekia, Hasadia na Yushab-hesedi.
21Wana wa Hanania walikuwa Pelatia na Yeshaya. Yeshaya alimzaa Refaya, aliyemzaa Arnani, aliyemzaa Obadia, aliyemzaa Shekania.[#3:21 Aya hii katika Kiebrania si dhahiri.]
22Shekania alimzaa Shemaya. Wana wa Shemaya walikuwa sita: Hatushi, Igali, Baria, Nearia na Shafati.
23Nearia alikuwa na wana watatu: Eliehonai, Hizkia na Azrikamu.
24Eliehonai alikuwa na wana saba: Hodavia, Eliashibu, Pelaya, Akubu, Yohanani, Delaya na Anani.