1 Yohane 3

1 Yohane 3

Watoto wa Mungu

1Oneni, basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu.

2Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba, wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo.

3Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo, hujiweka safi kama vile Kristo alivyo safi kabisa.[#3:3 Maana yake hali isiyochafuliwa na dhambi (wazo kuu katika 3:4-10).]

4Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana dhambi ni uvunjaji wa sheria.[#3:4 Kama vile katika 2Thes 2:3-8; neno hilo linachukua maana ya pekee hapa na laweza kutafsiriwa pia kwa neno: Uovu kwa maana ya upinzani kamili dhidi ya Mungu nyakati za mwisho.]

5Mnajua kwamba Kristo alikuja kuziondoa dhambi zetu, na kwamba kwake hamna dhambi yoyote.[#3:5 Yoh 1:29; ling 1Pet 2:24.; #3:5 Yoh 8:46; 1Pet 2:22; ling 2Kor 5:21; Ebr 4:15; 7:26.]

6Basi, kila aishiye katika muungano na Kristo hatendi dhambi; lakini kila mtu atendaye dhambi hakupata kamwe kumwona wala kumjua Kristo.[#3:6 Kinachosemwa hapa ni matokeo ya mambo yaliyotajwa katika aya zilizotangulia: Kule kuungana na Kristo hakuwezi kabisa kuendana na dhambi. Ling aya 9 na pia Rom 6:1-14.]

7Basi, watoto wangu, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote. Mtu atendaye matendo maadilifu ni mwadilifu kama vile Kristo alivyo mwadilifu kabisa.

8Lakini atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi ametenda dhambi tangu mwanzo. Lakini Mwana wa Mungu alikuja duniani kuiharibu kazi ya Ibilisi.[#3:8 Yoh 8:44; maneno tangu mwanzo yamkini yanaeleweka kulingana na matumizi ya 3:12 ambapo yule Mwovu ndiye aliyemwongoza Kaini kumwua nduguye; au, tangu mwanzo kwa maana ya wakati Mungu alipoumba vema vitu vyote.; #3:8 Ebr 2:14.]

9Kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, maana anayo hali ya kimungu ndani yake; hawezi kutenda dhambi kwa sababu yeye ni mtoto wa Mungu.[#3:9 Tafsiri ya neno la Kigiriki lenye maana ya kawaida ya “mbegu” lakini hapa au ni hali yake Mungu au ni Roho wa Mungu (taz 2:27; 3:24; 4:13; Yoh 3:5-8; 14:16-17 kuhusu nafasi na matokeo ya Roho wa Mungu ndani ya mwaamini). Katika 5:18 kisa cha mwaamini kutotenda dhambi ni kwa vile “Mwana wa Mungu hutulinda salama”. Kwa vyovyote hali yake Mungu yahusika au kwa njia ya Mwanawe au kwa Roho wake.]

10Lakini yeyote asiyetenda mambo maadilifu, au asiyempenda ndugu yake, huyo si mtoto wa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi.

Pendaneni

11Na, ujumbe mliousikia tangu mwanzo ndio huu: Tunapaswa kupendana![#3:11 Yoh 13:34; 15:12; ling 1Yoh 2:7-11; 3:18,23; 4:7-12; 4:20-5:2.]

12Tusiwe kama Kaini ambaye, kwa kuongozwa na yule Mwovu, alimuua ndugu yake. Na, kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa maovu, lakini yale ya ndugu yake yalikuwa mema!

13Basi, ndugu zangu, msishangae kama ulimwengu unawachukia nyinyi.[#3:13 Yoh 15:18-25; 17:14. Na, kuhusu matumizi ya “ulimwengu” hapa taz 2:15.]

14Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo na kuingia katika uhai kwa sababu tunawapenda ndugu zetu. Mtu asiye na upendo hubaki katika kifo.

15Kila anayemchukia ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua kwamba muuaji yeyote yule hana uhai wa milele ndani yake.[#3:15 Linga Mat 5:21-22.]

16Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu.[#3:16 Yoh 10:11; 15:13; ling Gal 2:20. Kuhusu kumwiga Yesu taz 1:7 maelezo.]

17Basi, mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona ndugu yake ana shida, lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma, anawezaje kusema kwamba anampenda Mungu?

18Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe upendo wa kweli na wa vitendo.

Uthabiti wetu mbele ya Mungu

19Hivyo ndivyo tuwezavyo kuwa na hakika kwamba sisi ni watu wa ukweli; na hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu.

20Kwa maana, hata kama dhamiri zetu zatuhukumu, twajua kwamba Mungu ni mkuu kuliko dhamiri, na kwamba yeye ajua kila kitu.[#3:20 Yaonekana kwamba aya hii ngumu ina lengo la kuwahakikishia waumini wasife moyo kwani Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu inayotuhukumu naye aweza kusamehe na anajua kila kitu.]

21Wapenzi wangu, kama dhamiri zetu hazina lawama juu yetu, basi, twaweza kuwa na uthabiti mbele ya Mungu,

22na kupokea kwake chochote tunachoomba, maana tunazitii amri zake na kufanya yale yanayompendeza.

23Na, amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Yesu Kristo, na kupendana kama alivyotuamuru.[#3:23 Yoh 13:34; 15:12,17.]

24Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na Mungu na Mungu anaishi katika muungano naye. Kwa njia ya Roho ambaye Mungu ametujalia, sisi twajua kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania