1 Wafalme 1

1 Wafalme 1

Siku za mwisho za mfalme Daudi

1Mfalme Daudi, wakati alipokuwa mzee sana, watumishi wake walimfunika kwa mablanketi, lakini hata hivyo, hakuweza kupata joto.[#1:1-4 Sura 1—2 zinaendelea na simulizi lililoanza katika 2Sam 9 ambalo lilikatizwa katika 2Sam 20. Taz 2Sam 21—24 maelezo.; #1:1 Hapa umri wake hautajwi, lakini kutokana na madokezo yaliyo katika 2Sam 5:4-5 wakati huu Daudi angekuwa na umri upatao miaka 70.]

2Kwa hivyo wakamwambia, “Bwana wetu mfalme, afadhali tukutafutie msichana akutumikie na kukutunza; alale pamoja nawe kusudi akupatie joto.”

3Basi, wakatafutatafuta msichana mzuri kote nchini Israeli. Akapatikana msichana mmoja mzuri aitwaye Abishagi, Mshunami; wakamleta kwa mfalme.[#1:3 Au, “Abishagi kutoka Shunami”: mahali katika eneo la kabila la Isakari (Yos 19:18, 1Sam 28:4) kwenye tambarare ya Yezreeli.]

4Msichana huyo, alikuwa mzuri sana. Basi, akaanza kumtumikia na kumtunza mfalme; lakini mfalme hakulala naye.[#1:1-4 Kudhoofika kwake Daudi kimwili kunaashiria pia kukosa nguvu ya kutawala na wakati huohuo kusababisha fujo katika ikulu yake: watu mashuhuri wanajiweka katika makundi tofauti hasa wanaomuunga mkono Adoniya na wale walio upande wa Solomoni ambao wote wawili walinyemelea kiti cha enzi cha Daudi.]

Adoniya anajitakia ufalme

5Wakati huo, Adoniya, mwana wa Daudi na Hagithi, akaanza kujigamba kwamba yeye ndiye atakayekuwa mfalme. Basi, akajitayarishia magari ya kukokotwa, wapandafarasi na wapiga mbio hamsini wa kumtangulia na kumshangilia.[#1:5 Huyu, kwa vile ndiye aliyekuwa na umri mkubwa kuliko watoto wengine wa Daudi (2Sam 3:2-5), alijiona au kujisikia kwamba yeye ndiye aliyekuwa na haki ya kutawala baada ya baba yake, ingawaje kutokana na aya 20 jambo la mtoto wa kwanza kuwa na haki hiyo halikuwa bado desturi iliyozingatiwa.]

6Lakini baba yake, Daudi, hakuwa amemkemea mwanawe hata mara moja na kumwuliza kwa nini alikuwa amefanya hivyo. Adoniya, ama kwa hakika, alikuwa mwenye sura ya kupendeza sana; na alikuwa amemfuata Absalomu kwa kuzaliwa.[#1:6 Kuwa na uzuri wa umbo inaonekana kuliweza kuchukuliwa kama moja ya sifa vya kufaa kuwa mfalme. Taz k.m. uzuri wa Shauli na Daudi (1Sam 9:2; 16:12) na Absalomu (2Sam 14:25).]

7Adoniya akashauriana na Yoabu mwana wa Seruya, na kuhani Abiathari; nao wakamfuata na kumuunga mkono.

8Lakini kuhani Sadoki, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na nabii Nathani na Shimei, Rei pamoja na walinzi wa Daudi, hawakumuunga mkono Adoniya.

9Siku moja, Adoniya alitoa sadaka ya kondoo, ng'ombe na ndama wanono kwenye Jiwe la Nyoka, karibu na chemchemi iitwayo Enrogeli. Akawaalika kwenye karamu ya sadaka hiyo ndugu zake wote, yaani wana wengine wa mfalme, na watumishi wote wa mfalme waliokuwa wa kabila la Yuda.[#1:9 Tambiko hizo zilikuwa sehemu ya sherehe za kutawazwa mfalme.]

10Lakini, nabii Nathani, Benaya, walinzi wa mfalme na Solomoni ndugu yake hakuwaalika.

Solomoni anatawazwa kuwa mfalme

11Hapo, Nathani akamwendea Bathsheba mama yake Solomoni, akamwuliza, “Je, hujasikia kwamba Adoniya, mwanawe Hagithi, amejinyakulia mamlaka ya ufalme na bwana wetu Daudi hana habari?[#1:11 Hapo awali huyu alikuwa mke wa Uria, mmoja wa askari wake Daudi. Daudi alilala na Bathsheba na alipogundua kuwa amepata mimba alifanya mbinu za kumwua Uria kule vitani kusudi amchukue mke wake (2Sam 11:2-27). Mtoto aliyezaliwa kutokana na huo uhusiano wa Daudi na Bathsheba alikufa kama adhabu kwa dhambi hiyo ya Daudi. Solomoni ndiye aliyekuwa mtoto wao wa pili (2Sam 12:24).]

12Basi, kama ukitaka kuyaokoa maisha yako na ya mwanao Solomoni, nakushauri hivi:

13Mwendee mfalme Daudi, umwulize, ‘Je, bwana wangu mfalme, hukuniapia mimi mtumishi wako ukisema, “Mwana wako Solomoni atatawala mahali pangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?” Imekuwaje basi, sasa Adoniya anatawala?’[#1:13 Ahadi hiyo kwamba Solomoni angekuwa mfalme haikuandikwa popote pengine katika Biblia, lakini mazingira ya 2Sam 12:24-25 yanaweza kufikiriwa kwa ajili hiyo.]

14Na utakapokuwa bado unaongea na mfalme, mimi nitaingia na kuyathibitisha maneno yako.”

15Basi, Bathsheba alimwendea mfalme chumbani mwake (wakati huo mfalme alikuwa mzee sana, naye Abishagi, Mshunami alikuwa akimhudumia).

16Bathsheba aliinama, akamsujudia mfalme, naye mfalme akamwuliza, “Unataka nini?”

17Bathsheba akamjibu, “Bwana wangu, uliniapia mimi mtumishi wako mbele ya Bwana Mungu wako, ukisema: ‘Mwana wako Solomoni atatawala baada yangu, na ataketi juu ya kiti changu cha enzi.’

18Sasa, tazama, Adoniya anatawala ingawa wewe bwana wangu mfalme hujui kuhusu hayo.

19Ametoa sadaka ya ng'ombe, ya vinono, na kondoo wengi, na kuwaita wana wote wa mfalme, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini mtumishi wako Solomoni hakumkaribisha.

20Na sasa, bwana wangu mfalme, Waisraeli wote wanakungojea, ili uwaambie yule atakayeketi juu ya kiti chako baada yako, bwana wangu mfalme.

21La sivyo, itatokea ya kwamba, wakati ambapo wewe bwana wangu, mfalme, utakapofariki mimi pamoja na mwanangu Solomoni tutahesabika kama wenye hatia.”

22Wakati Bathsheba alipokuwa akizungumza na mfalme, nabii Nathani aliingia ikulu.

23Nao watu wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Naye alipomfikia mfalme, alimwinamia mfalme mpaka uso ukafika chini udongoni.

24Ndipo Nathani aliposema, “Bwana wangu, je, ulisema, ‘Adoniya atatawala baada yangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?’

25Kwa maana leo ameteremka, akatoa sadaka ya ng'ombe, vinono na kondoo wengi na amewakaribisha wana wa mfalme, Yoabu jemadari wa jeshi, na kuhani Abiathari, na, tazama, wanakula na kunywa mbele yake, na kusema, ‘Uishi mfalme Adoniya!’

26Lakini hakunialika mimi, mtumishi wako wala kuhani Sadoki, wala Benaya mwana wa Yehoyada na mtumishi wako Solomoni.

27Je, yote haya umeyafanya wewe bwana wangu, mfalme, bila kuwaambia watumishi wako mtu atakayekaa juu ya kiti chako cha enzi baada yako?”

28Naye mfalme Daudi akajibu, “Niitie Bathsheba.” Bathsheba alimwendea mfalme na kusimama mbele yake.

29Halafu mfalme aliapa akisema, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, aliyekomboa roho yangu katika taabu nyingi,

30kama nilivyokuapia mbele za Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nikisema, ‘Mwanao Solomoni atatawala baada yangu, na kwamba atakaa juu ya kiti changu cha enzi badala yangu,’ ndivyo nitakavyofanya leo.”

31Ndipo Bathsheba alipoinama mpaka chini, akamsujudia mfalme, na kusema “Bwana wangu, mfalme Daudi, aishi milele!”

32Kisha mfalme Daudi akasema, “Niitie kuhani Sadoki, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada.” Nao wakamjia mfalme.

33Naye mfalme akawaambia, “Nenda na watumishi wangu mimi bwana wako, umpandishe mwanangu Solomoni juu ya nyumbu wangu, umpeleke Gihoni;[#1:33 Nyumbu ni mnyama mwenye nguvu ambaye anatokana na farasi na punda. Huko Mashariki ya Kati ya Kale nyumbu (au hata punda) walitumiwa hasa na wafalme (taz aya 38 na 44). Rejea 2Sam 18:9 na Zek 9:9 (hapa ikiwa ni punda).; #1:33 Hapa ina maana ya Chemchemi ya Gihoni, maarufu kabisa huko Yerusalemu kwa kuwa chanzo cha maji yote yaliyotumika humo. Wataalamu wa mambo ya kale waligundua mfereji wa chini kwa chini ambao ulianzia kwenye chemchemi nje ya mji mpaka ndani ya mji kwenye bwawa. Wakati wa vita watu waliweza kupata maji bila kwenda nje ya ukuta wa Yerusalemu.]

34halafu umruhusu kuhani Sadoki na nabii Nathani wampake mafuta kuwa mfalme wa Israeli; baadaye pigeni tarumbeta na kusema, ‘Mfalme Solomoni aishi!’[#1:34 Kitendo hiki cha kumtawaza mfalme au kumweka wakfu kilifanyika kwa kumpaka mhusika mafuta ya zeituni yaliyowekwa wakfu (aya 39). Kupakwa mafuta huko kulifikiriwa kumweka mfalme katika hali ya uhusiano wa pekee na Mungu (1Sam 16:13; Zab 89:20-21). Taz pia Zab 2:2.]

35Nanyi mtamfuata, naye atakuja na kuketi juu ya kiti changu cha enzi badala yangu; nami nimemteua kuwa mtawala juu ya Israeli na juu ya Yuda.”

36Ndipo Benaya mwana wa Yehoyada alipomjibu mfalme, “Amina! Bwana Mungu wa bwana wangu mfalme, na anene vivyo hivyo.

37Kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa na bwana wangu mfalme, awe pia na Solomoni, na akikuze kiti chake cha enzi kuliko kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme Daudi.”

38Basi, kuhani Sadoki, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada, na Wakerethi na Wapelethi, wote walishuka wakampandisha Solomoni kwenye nyumbu wa mfalme Daudi, na kumpeleka mpaka Gihoni.[#1:38 Katika 2Sam 8:18 tunajua kwamba Benaya alikuwa kiongozi wa Wakerethi na Wapelethi. Ndio kusema hao Wakerethi na Wapelethi walikuwa kundi la walinzi (wa kukodiwa) wa Daudi wakiongozwa na Benaya. Wakerethi labda walikuwa kutoka Krete nao Wapelethi awali walikuwa labda kutoka pwani ya Bahari ya Agea.]

39Kisha kuhani Sadoki alichukua pembe za mafuta kutoka hemani na kumpaka mafuta Solomoni kuwa mfalme. Kisha walipiga tarumbeta; na watu wote wakasema, “Aishi mfalme Solomoni!”[#1:39 Neno “hema” ambalo linatumiwa karibu mara hamsini katika Biblia ya Kiebrania mara nyingi linahusu lile hema ambalo Mungu alimwamuru Mose kutengeneza na ambalo lingekuwa mahali ambapo Waisraeli wangemwabudu Mwenyezi-Mungu na makuhani kumtambikia (Kut 26). Inasemekana kwamba Waisraeli walipovamia nchi ya Kanaani walikuwa na hilo hema, naye Daudi baadaye aliliweka mjini Yerusalemu. Ndani ya hema hilo kulikuwa na lile sanduku la agano.]

40Halafu watu wote walimfuata, wakipiga mazomari, wakafurahi kwa shangwe kubwa, hata nchi ikatikisika kwa sauti zao.

41Basi, Adoniya pamoja na wageni waliokuwa naye walisikia hao watu walipomaliza sherehe. Naye Yoabu aliposikia sauti ya tarumbeta alisema, “Makelele hayo mjini ni ya nini?”

42Alipokuwa akisema, kumbe, Yonathani mwana wa kuhani Abiathari akaingia; kisha Adoniya akasema, “Karibu, kwani wewe u mtu mwema; unaleta habari njema.”[#1:42 Kuhusu huyu Yonathani tunajua kuwa alikuwa mtumishi mwaminifu wa Daudi (taz 2Sam 15:36; 17:17-22).]

43Ndipo Yonathani alipomjibu Adoniya, “Hapana, kwa sababu mfalme Daudi amemtawaza Solomoni kuwa mfalme;

44naye mfalme amempeleka pamoja na kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada na Wakerethi na Wapelethi, nao wamempandisha juu ya nyumbu wa mfalme,

45kisha kuhani Sadoki na nabii Nathani wamemtia mafuta kuwa mfalme kule Gihoni; halafu wametoka hapo wakifurahi; ndicho kisa cha makelele hayo unayosikia.

46Sasa Solomoni anaketi juu ya kiti cha kifalme.

47Zaidi ya hayo, watumishi wa mfalme walikuja kumpongeza bwana wetu mfalme Daudi wakisema, ‘Mungu wako alifanye jina la Solomoni kuwa maarufu kuliko lako; pia akikuze kiti chake cha enzi kuliko kiti chako.’ Halafu mfalme akainama kitandani,

48na kuomba akisema, ‘Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, ambaye amemfanya mzawa wangu kuwa mfalme mahali pangu, na ambaye amenipa maisha hata nimeyaona haya.’”

49Basi, wageni wa Adoniya wakaogopa sana, wakaondoka na kutawanyika.

50Naye Adoniya, kwa kuwa alimwogopa Solomoni, akakimbilia katika hema la Mwenyezi-Mungu akazishika pembe za madhabahu apate kusalimika.[#1:50 Pembe za madhabahu zilikuwa zimefanywa kufanana karibu na pembe za mnyama. Kwa vile madhabahu, yaani mahali palipojengwa pa kutambikia, madhabahu ilikuwa takatifu, na mtu aliyekimbilia hapo na kushikilia pembe zake alichukuliwa kuwa salama, asiweze kuuawa na wale waliokuwa wanamfuatia. Lakini hiyo ilikuwa tu kwa wale ambao walikuwa wameua mtu bila kukusudia. Vile vile kulikuwa na miji iliyotengwa (rejea Hes 35:9-15; Kumb 4:41-43; 19:1-13; Yos 20) ambamo mtu aliyeua bila kukusudia angeweza kukimbilia usalama.]

51Mfalme Solomoni akapata habari kwamba Adoniya alikuwa amekimbilia hemani, na kwamba anashikilia pembe za madhabahu akisema, “Sitaondoka hapa mpaka mfalme Solomoni atakaponihakikishia kwamba hataamuru niuawe.”

52Mfalme Solomoni akasema, “Nikimwona kuwa mwaminifu basi, hatapata madhara yoyote. Lakini nikimwona kuwa mwovu, lazima afe.”

53Basi, mfalme Solomoni akaagiza Adoniya aitwe kutoka hemani, aje kwake. Adoniya akafika mbele ya mfalme, akainama kwa heshima. Mfalme akamwambia, “Nenda zako nyumbani.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania