1 Wafalme 14

1 Wafalme 14

Kifo cha mwana wa Yeroboamu

1Wakati huo, Abiya mwana wa mfalme Yeroboamu, akawa mgonjwa.[#14:1-20 Kuanzia hapa mpaka 2Fal 17 vitabu vyote viwili vya Wafalme vinasimulia kwa pamoja historia ya falme za Israeli na Yuda vikitaja kwa muundo wa kupokezana wafalme wawiliwawili. Tofauti na vitabu hivi, vitabu vya Mambo ya Nyakati, kwa kuzingatia ukoo wa Daudi, mara chache sana husimulia juu ya wafalme wa kaskazini wa Israeli.]

2Yeroboamu akamwambia mkewe, “Jisingizie kuwa mwingine, uende mjini Shilo anakokaa nabii Ahiya aliyesema kwamba mimi nitakuwa mfalme wa Israeli.

3Mpelekee mikate kumi, maandazi kadha, na asali chupa moja. Yeye atakuambia yatakayompata mtoto wetu.”[#14:2-3 Kutokana na vitu hivi ambavyo vyaweza kutolewa kama zawadi kutoka kwa mtu wa kawaida, huenda Yeroboamu alisema hivyo viwe ni mojawapo ya namna ya kujisingizia kwamba mkewe alikuwa mtu wa kawaida tu na sio mke wa mfalme.]

4Basi, mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda Shilo nyumbani kwa Ahiya. Wakati huo, Ahiya alikuwa hawezi tena kuona sawasawa kwa sababu ya uzee.

5Mwenyezi-Mungu alikuwa amekwisha mwambia Ahiya kwamba mke wa Yeroboamu alikuwa njiani, anakuja kumwuliza yatakayompata mwanawe mgonjwa, na jinsi atakavyomjibu.

Mkewe Yeroboamu alipofika, alijisingizia kuwa mtu mwingine.

6Lakini Ahiya alipomsikia anaingia mlangoni, alisema, “Karibu ndani mke wa Yeroboamu. Lakini mbona unajisingizia kuwa mtu mwingine? Ninao ujumbe usio mzuri kwako!

7Nenda ukamwambie Yeroboamu kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Nilikuteua miongoni mwa watu, nikakufanya kuwa kiongozi wa watu wangu, Israeli;

8nikaurarua ufalme utoke kwa wazawa wa Daudi, nikakupa wewe. Lakini wewe ni kinyume kabisa cha mtumishi wangu Daudi ambaye alizishika amri zangu, akafuata matakwa yangu kwa moyo wake wote na kutenda tu yaliyo sawa mbele ya macho yangu.

9Wewe umetenda uovu mbaya zaidi kuliko waliotenda wale waliokutangulia; wewe umenikasirisha kwa kujitengenezea miungu mingine na sanamu za kufua, kisha umeniacha.

10Haya basi, sasa nitailetea balaa jamaa hii yake, Yeroboamu, nitawaua wanaume wote wa jamaa zake katika Israeli, awe mtumwa au huru. Jamaa wake wote nitawateketeza kama mtu ateketezavyo mavi, mpaka yatoweke.

11Yeyote aliye wa jamaa ya Yeroboamu atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.’”

12Ahiya akamwambia mkewe Yeroboamu, “Haya inuka, uende zako nyumbani. Mara tu utakapoingia mjini, mwanao atakufa.

13Watu wote wa Israeli watafanya matanga na kumzika. Walakini, ni huyo tu wa jamaa ya Yeroboamu atakayezikwa, kwani ni yeye tu wa jamaa ya Yeroboamu aliyepata kumpendeza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

14Tena leo hii, Mwenyezi-Mungu ataweka mfalme mwingine katika Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu.

15Naam, tangu sasa, Mwenyezi-Mungu atawapiga watu wa Israeli, nao watatikisika kama unyasi unavyotikiswa mtoni. Atawang'oa kutoka nchi hii nzuri aliyowapa babu zao, na kuwatawanya mbali, ng'ambo ya mto Eufrate, kwa sababu wamemkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa kujitengenezea sanamu za Ashera, mungu wa kike.

16Mwenyezi-Mungu ataitupa Israeli kwa sababu ya dhambi alizotenda Yeroboamu, na kuwafanya watu wa Israeli pia watende dhambi.”[#14:16 Dhambi ya Yeroboamu inachukuliwa katika vitabu vya Wafalme kuwa mbaya sana na inatajwa mara kwa mara (rejea 1Fal 15:26,30,34; 16:2,13,19,26, n.k.).]

17Hapo, mkewe Yeroboamu akaondoka, akashika safari mpaka Tirza. Mara tu alipofika mlangoni, mtoto akafa.[#14:17 Labda Yeroboamu aliufanya mji huu kuwa mji mkuu wa ufalme wake, yaani ufalme wa Kaskazini wa Israeli, ingawa wataalamu wengi wa mambo ya Biblia wanafikiri mfalme Baasha ndiye aliyeufanya kuwa mji mkuu wa ufalme huo (1Fal 15:33). Mji huu ulikuwa kilomita kumi kaskazini-mashariki ya Shekemu. Inajulikana kwamba baadaye mfalme Omri aliuanzisha mji wa Samaria kuwa mji mkuu wa ufalme wa kaskazini (1Fal 16:23-24). Taz pia 1Fal 12:1 maelezo.]

18Watu wote wa Israeli wakamzika na kufanya matanga kama alivyosema Mwenyezi-Mungu, kwa njia ya nabii Ahiya, mtumishi wake.

Kifo cha Yeroboamu

19Matendo mengine ya mfalme Yeroboamu, jinsi alivyopigana vita na alivyotawala, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.[#14:19 Labda hicho kilikuwa kitabu ambacho waandishi wa ikulu ya wafalme waliandika matukio muhimu ya ikulu.]

20Yeroboamu alitawala kwa muda wa miaka ishirini na miwili, halafu akafariki, na Nadabu, mwanawe, akatawala mahali pake.

Mfalme Rehoboamu wa Yuda

(2 Nya 11:5—12:15)

21Rehoboamu, mwanawe Solomoni, alikuwa na umri wa miaka arubaini na mmoja alipoanza kutawala Yuda. Naye alitawala kwa muda wa miaka kumi na saba katika Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi-Mungu aliuchagua miongoni mwa miji ya makabila yote ya Israeli aabudiwe humo. Mama yake Rehoboamu alikuwa Naama kutoka Amoni.[#14:21 Kwamba mama yake alikuwa Mwamoni si ajabu kwa sababu ya Solomoni kuoa wake wengi wa kigeni.]

22Watu wa Yuda walitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Walimkasirisha kwa dhambi zao walizotenda, nyingi kuliko za babu zao.

23Walijitengenezea pia mahali pa ibada, minara ya kutambikia, na sanamu za Ashera, juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti wenye majani mabichi.[#14:23 Watu wa Yuda nao pia hawakuwa tofauti na watu wa Israeli kuhusu kuvunja amri ya Mungu iliyokataza kuabudu miungu mingine.]

24Tena, kukawa na ibada za ukahaba nchini; watu walitenda matendo ya kuchukiza ya mataifa ambayo Mungu aliyafukuza Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini Kanaani.[#14:24 Neno la Kiebrania linalotafsiriwa hapa linahusu malaya wa kike na wa kiume ambao walifanya vitendo hivyo kwenye mahali pa ibada (taz Kumb 23:17 maelezo).]

25Katika mwaka wa tano wa utawala wa Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri, aliushambulia mji wa Yerusalemu,

26akaichukua hazina yote ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya ikulu; alichukua kila kitu; pia alichukua ngao zote za dhahabu alizozitengeneza Solomoni.

27Badala ya ngao hizo, mfalme Rehoboamu alitengeneza ngao za shaba na kuziweka chini ya ulinzi wa wangojamlango wa ikulu.

28Kila wakati mfalme alipokwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walinzi walizibeba ngao hizo, na baadaye wakazirudisha katika chumba cha ulinzi.

29Matendo mengine ya mfalme Rehoboamu, na yote aliyoyafanya, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda.

30Daima kulikuwako vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu.

31Hatimaye, Rehoboamu alifariki na kuzikwa kwenye makaburi ya wazee wake, katika mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama kutoka Amoni, na Abiyamu mwanawe akatawala mahali pake.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania