1 Wafalme 19

1 Wafalme 19

Elia mlimani Horebu

1Mfalme Ahabu alimsimulia mkewe Yezebeli mambo yote aliyofanya Elia na jinsi alivyowaua manabii wa Baali kwa upanga.

2Yezebeli akatuma mjumbe kwa Elia amwambie: “Miungu waniulie mbali, nakuapia, ikiwa saa hizi kesho sitakuwa nimekufanya kama mmoja wa hao manabii.”

3Elia akakimbilia mjini Beer-sheba mkoani Yuda, alikomwacha mtumishi wake,[#19:3 Mji uliokuwa kusini mwa eneo la Yuda katika sehemu ya nyika ijulikanayo kama Negebu. Ulikuwa mji maarufu kama kituo cha biashara kati ya Israeli na Misri.]

4naye akatembea mwendo wa siku nzima kuingia jangwani. Basi, akafika, akaketi chini ya mti mmoja, mretemu. Hapo, akaomba afe, akisema, “Imetosha! Siwezi tena. Ee Mwenyezi-Mungu, sasa utoe uhai wangu. Mimi si bora kuliko wazee wangu.”[#19:4 Mti ambao huota nyikani kukavu na ambao huweza kuwapatia wasafiri kivuli ingawa si mkubwa.]

5Basi, Elia akalala chini ya mti huo, akashikwa na usingizi. Punde, malaika akaja, akamgusa na kumwambia, “Amka ule.”

6Elia alipotazama, akaona mkate uliookwa juu ya makaa, na chupa ya maji karibu na kichwa chake. Basi, akala, akanywa, akalala tena.

7Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamjia tena mara ya pili, akamgusa na kumwambia, “Amka ule, la sivyo safari itakuwa ngumu mno kwako.”

8Elia akaamka, akala na kunywa. Kisha akatembea kwa nguvu ya chakula hicho mwendo wa siku arubaini, mchana na usiku, mpaka Horebu, mlima wa Mungu.[#19:8 Jina lingine la Sinai (taz Kut 3:1). Elia anakwenda kwenye mlima wa Mungu ambako Mungu alijijulisha kwa watu wake na kufanya agano nao. Kwa namna moja au nyingine kurudi hapa kunaweza kueleweka kwamba Mungu anataka kurekebisha tena imani ya Israeli. Tena Elia anatumia siku arubaini kuwasili huko. Mose alikaa siku arubaini kule mlimani (Kut 24:15-18) na katika A.J. Yesu alikaa siku arubaini jangwani kabla ya kuanza huduma yake ya ukombozi (Mat 4:2).]

9Huko, akafika penye pango, akakaa humo. Mara neno la Mwenyezi-Mungu likamjia: “Elia! Unafanya nini hapa?”[#19:9 Kukutana huku kwa Elia na Mwenyezi-Mungu kuna tofauti kadhaa na jinsi Mungu alivyojijulisha kwa Waisraeli pale awali (rejea Kut 19:24; 33—34). Kulingana na Kut 19 Mwenyezi-Mungu alijionesha kwa Waisraeli katika tufani, tetemeko la nchi na moto. Hapa, ishara hizo zinatangulia tu upepo mwanana ambapo Mungu anajijulisha kwa Elia (aya 12). Wengine wanaona hapa kwamba Mwenyezi-Mungu ni tofauti na Baali ambaye wakati huo alijulikana kama mungu wa tufani, ngurumo na radi.]

10Naye akasema, “Naona uchungu na wivu, ewe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, kwa sababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda, waniue!”

11Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nenda ukasimame mlimani, mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mwenyezi-Mungu akapita na kuuvumisha upepo mkali ambao uliporomosha milima na kuvunja miamba. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika upepo huo. Upepo ukapita, kukawa na tetemeko la ardhi. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika tetemeko la ardhi.

12Tetemeko likapita, kukawa na moto. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika moto huo. Baada ya moto, pakatokea sauti ndogo, tulivu.

13Basi, Elia aliposikia sauti hiyo, alijifunika uso kwa joho lake, akatoka na kusimama mlangoni mwa pango. Hapo, akasikia sauti, “Elia! Unafanya nini hapa?”

14Naye akasema, “Naona uchungu na wivu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, kwa sababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda waniue!”

15Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi kwa kupitia njia ya jangwani mpaka Damasko. Utakapofika, mpake Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu.[#19:15 Kwanza, “Aramu” ni jina linalotumiwa katika Kiebrania kutaja nchi ya Siria ya kale na mji wake mkuu Damasko. Kupaka mafuta ya zeituni kilikuwa kitendo kilichomaanisha kwamba mpakwa mafuta huyo amekuwa mfalme, n.k. Nabii Samueli k.m. alikuwa amepewa agizo la namna hiyo kuhusu Shauli na baadaye kuhusu Daudi (1Sam 10—11; 16:1-13). Hazaeli hakuwa Mwisraeli; hata hivyo Elia anaagizwa kumpaka mafuta awe mfalme na jambo hili linaonesha kwamba Mwenyezi-Mungu ni Mungu wa mataifa yote.]

16Naye Yehu, mwana wa Nimshi, mpake mafuta awe mfalme wa Israeli. Elisha, mwana wa Shafati, wa Abel-mehola, utampaka mafuta awe nabii mahali pako.[#19:16 Kwa kawaida wafalme na makuhani ndio waliopakwa mafuta. Kitendo hiki cha kumpaka Elisha awe nabii ni cha pekee na si rahisi kukifafanua. Taz 1Fal 1:34 maelezo; Zab 2:2 maelezo; rejea Lawi 8:12.]

17Basi, yeyote atakayenusurika upanga wa Hazaeli, Yehu atamuua, na yeyote atakayenusurika upanga wa Yehu, Elisha atamuua.

18Lakini, nitaacha hai watu 7,000 nchini Israeli, ambao hawajamwinamia Baali, wala kuibusu sanamu yake.”[#19:18 Idadi hiyo inapatikana kwa kuzidisha idadi saba ambayo inachukuliwa mara nyingi katika Biblia kama idadi timilifu au kamilifu. Taz Mwa 4:23-24 maelezo. Ingawa idadi hiyo si kubwa sana ilitosha kumhakikishia Elia kwamba yeye ni mmoja wa wengi walio waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu. Taz Rom 11:2-6.]

Elisha anaitwa kuwa nabii

19Elia akaondoka, akamkuta Elisha, mwana wa Shafati, analima. Hapo, palikuwa na jozi kumi na mbili za ng'ombe wanalima, na jozi ya Elisha ilikuwa ya nyuma kabisa. Basi, Elia akavua joho lake na kumtupia.[#19:19 Kitendo hicho kilikuwa ishara kwamba Elia anamwita Elisha amfuate na kuwa nabii. Taz pia 2Fal 2:13-15.]

20Hapo, Elisha akawaacha ng'ombe wake, akamfuata Elia mbio na kumwambia, “Niruhusu kwanza niende kumpa baba yangu na mama yangu busu la kwaheri, kisha nikufuate.” Elia akamjibu, “Nenda! Kwani nimekuzuia?”[#19:20 Au: “Nenda, urudi upesi kwa kuwa jambo nililokutendea ni la maana”.]

21Basi, Elisha akamwacha Elia, akairudia jozi yake ya ng'ombe, akawachinja ng'ombe hao na kuwapika akitumia miti ya nira kama kuni, akawapa watu, wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Elia na kuwa mtumishi wake.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania