The chat will start when you send the first message.
1Maadamu Kristo aliteseka kimwili, nanyi pia mnapaswa kujiimarisha kwa nia hiyo yake; maana mtu akisha teseka kimwili hahusiki tena na dhambi.[#4:1 Hapa, mwandishi anageukia lile wazo la 3:18.; #4:1 Lugha inayotumika hapa ni ile ya kujiweka imara kwa silaha; rejea Fil 2:5 na pia picha ya silaha za kiroho katika Efe 6:11-17.; #4:1 Wengine wanafafanua maneno haya kama kanuni ya jumla; wengine wanafikiri lazima yaeleweke pamoja na kufikiria juu ya Kristo katika mateso yake.; #4:1 Mkristo, kwa kuungana na Kristo, naye pia kwa kitendo cha Kristo cha kuondolea mbali dhambi na kuushinda uovu, anakata uhusiano na dhambi. Rejea Rom 6:2,7.]
2Tangu sasa, basi, maisha yaliyowabakia kuishi hapa duniani yanapaswa kuongozwa na matakwa ya Mungu, sio na tamaa za kibinadamu.
3Wakati uliopita mlikuwa na muda mrefu wa kufanya mambo wanayofanya watu wasiomjua Mungu. Mliishi maisha ya anasa, ubinafsi, ulevi, ugomvi, kunywa mno na ya ibada haramu za sanamu.[#4:3 Rejea orodha ya mazoea mabaya au maovu yanayotajwa katika Rom 1:29-31 na pia taz maelezo ya Rom 1:29-32.]
4Sasa, watu hao wasiomjua Mungu wanashangaa wanapoona kwamba hamwandamani nao tena katika hali ya kuishi vibaya, na hivyo wanawatukaneni.
5Lakini watapaswa kutoa hoja juu ya jambo hilo mbele yake Mungu aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa!
6Ndiyo maana Habari Njema ilihubiriwa hata kwa hao waliokufa, ili baada ya kuhukumiwa katika maisha yao ya kimwili kama wengine, waishi kwa ajili ya Mungu kwa njia ya Roho.[#4:6 Haisemwi moja kwa moja ni nani aliyehubiri; na hata hao walengwa, “waliokufa”, si dhahiri ni akina nani. Mara nyingine wafafanuzi wa Maandiko Matakatifu huhusisha simulizi hili na yale yanayosemwa katika Mat 27:52. Si yamkini kwamba maneno haya yana uhusiano na yale yanayotajwa katika 3:19-20.]
7Mwisho wa vitu vyote umekaribia. Kwa hiyo mnapaswa kuwa na utaratibu na kukesha ili muweze kusali.
8Zaidi ya yote pendaneni kwa moyo wote, maana upendo hufunika dhambi nyingi.[#4:8 Yaani huondoa dhambi. Yawezekana kueleweka kwamba wanaopendana husameheana makosa yao, wao kwa wao; au, Mungu huwasamehe dhambi wale wanaotekeleza upendo wa kindugu. Rejea Meth 10:12 (ling pia 1Kor 13:7; Yak 5:20).]
9Muwe na ukarimu nyinyi kwa nyinyi bila kunung'unika.[#4:9 4:9 Ukarimu ulikuwa jambo muhimu nyakati hizo, hasa kutokana na hali yenyewe ngumu ambayo Wakristo walikumbana nayo. Taz Rom 12:13 maelezo, na pia rejea 1Tim 3:2; Tito 1:8; Ebr 13:2; 3Yoh 5-6.]
10Kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine kama wakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu.[#4:10 Rejea 1Kor 4:1-2 na pia Luka 12:42-48. Taz Rom 12:6-8; 1Kor 12:4-31.]
11Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumikia anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina.
12Wapenzi wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na kitu kisicho cha kawaida.[#4:12 Taz 1Pet 1:6-7 maelezo.]
13Ila furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili muweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa.
14Heri yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristo; jambo hilo lamaanisha kwamba Roho mtukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa nanyi.[#4:14 Mat 5:11; rejea Mate 5:41; 9:16.]
15Asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu ambaye anapaswa kuteseka kwa sababu ni mwuaji, mwizi, mhalifu au mwovu.
16Lakini kama mtu akiteseka kwa sababu ni Mkristo, basi, asione aibu, bali amtukuze Mungu, kwa sababu mtu huyo anaitwa kwa jina la Kristo.[#4:16 Maadui wa Ukristo walitumia jina hilo kwa dharau; rejea Mate 11:26.]
17Wakati wa hukumu umefika, na hukumu hiyo inaanza na watu wake Mungu mwenyewe. Ikiwa hukumu hiyo inaanzia kwetu sisi, basi, mwisho wake utakuwa namna gani kwa wale wasioamini Habari Njema ya Mungu?
18Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
“Ni vigumu kwa watu waadilifu kuokolewa;
itakuwaje basi, kwa wasiomcha Mungu na wenye dhambi?”
19Kwa hiyo, wale wanaoteseka kufuatana na matakwa ya Mungu, wanapaswa, kwa matendo yao mema, kujiweka chini ya Muumba wao ambaye ni wa kuaminika kabisa.