1 Samueli 29

1 Samueli 29

Daudi akataliwa na Wafilisti

1Wafilisti walikusanya majeshi yao yote huko Afeka, na Waisraeli walipiga kambi kwenye chemchemi ya bonde la Yezreeli.[#29:1 Mji huu labda ni uleule unaotajwa katika 4:1. Ulikuwa katika mwambao wa pwani ya Mediteranea, kaskazini mwa eneo lilokaliwa na Wafilisti na ulikuwa kituo cha kijeshi cha Wafilisti (1Sam 4:1).]

2Wakuu watano wa Wafilisti walipokuwa wakipita na vikosi vyao vya mamia na maelfu, Daudi naye akiwa na watu wake pamoja na Akishi walikuwa wanafuata upande wa nyuma wa jeshi hilo.

3Makamanda wa Wafilisti waliuliza, “Waebrania hawa wanafanya nini hapa?” Akishi akawajibu hao makamanda Wafilisti, “Huyu ni Daudi, mtumishi wa Shauli mfalme wa Israeli; naye amekuwa nami kwa muda mrefu: miaka kadhaa. Na tangu alipokimbilia kwangu, sijampata na kosa lolote.”[#29:3 Taz 1Sam 14:11 maelezo.; #29:3 Ni dhahiri kwamba mpaka hapa Akishi hakuwa amegundua mbinu za Daudi tangu wakati alipojiweka katika utumishi wake (rejea 1Sam 27:7-12).]

4Lakini makamanda wa Wafilisti walimkasirikia sana Akishi, wakamwambia, “Mrudishe aende mahali ulikompa akae. Kamwe asiende pamoja nasi vitani, la sivyo wakati wa vita atageuka na kuwa adui yetu. Huoni kuwa mtu huyu atapata njia nzuri ya kupatana na bwana wake halafu kuwa adui yetu vitani?

5Je, huyu si Daudi yuleyule ambaye wanawake waliimba habari zake walipokuwa wakicheza,

‘Shauli ameua maelfu,

lakini Daudi ameua maelfu kumi.’”

6Akishi akamwita Daudi na kumwambia, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba umekuwa mwaminifu kwangu. Lingekuwa jambo jema kwangu twende wote vitani, kwa maana sijaona lolote baya kwako tangu siku ile ulipokuja kwangu hadi leo hii. Hata hivyo, wakuu hawajaridhika nawe.[#29:6 Akishi anaapa kwa jina la Mungu wa Waisraeli labda kama njia ya kumhakikishia Daudi uaminifu wake.]

7Hivyo sasa, rudi nyumbani. Nenda kwa amani ili usiwachukize wakuu wa Wafilisti.”

8Daudi akamwambia Akishi, “Lakini nimefanya nini? Kama unavyosema kuwa, hujaniona na kosa lolote tangu siku ile nilipoanza kukutumikia hadi leo, kwa nini nisiende kupigana na maadui za bwana wangu, mfalme?”[#29:8 Kwanza sehemu ya kwanza ya jibu la Daudi ni lalamiko ambalo lengo lake ni kuonesha kwamba hana hatia. Na kuhusu sehemu ya pili ya jibu hili wengi wanafikiri Daudi aliliweka lieleweke makusudi kwa vile maneno “bwana wangu, mfalme” yanaweza kuwa na maana ya Akishi, au Shauli au hata Bwana, (adonay) yaani Mungu.]

9Akishi akamwambia, “Najua kuwa huna lawama mbele yangu kama malaika wa Mungu. Hata hivyo, makamanda wa Wafilisti wamesema, ‘Kamwe asiende pamoja nasi vitani’.[#29:9 Yamkini maneno haya yanatumika hapa kwa maana ya jumla, yaani: mtu mwema na mwaminifu. Katika 2Sam 14:17 na 19:27 maneno hayo yanahusu hasa uzoefu wa Daudi wa namna ya pekee wa kubainisha mema na mabaya.]

10Sasa, wewe pamoja na watumishi wa bwana wako Shauli waliokuja pamoja nawe, kesho asubuhi na mapema, amkeni na kuondoka mara kunapopambazuka.”

11Hivyo, kesho yake asubuhi, Daudi pamoja na watu wake waliondoka kurudi katika nchi ya Wafilisti. Lakini hao Wafilisti wakaenda Yezreeli.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania