The chat will start when you send the first message.
1Basi, Wafilisti walipigana vita dhidi ya Waisraeli; nao Waisraeli walikimbia mbele ya Wafilisti, na kuuawa katika mlima wa Gilboa.
2Lakini Wafilisti wakamzingira Shauli na wanawe, kisha wakawaua Yonathani, Abinadabu na Malki-shua, wana wa Shauli.[#31:2 Inavyoonekana Shauli alikuwa na watoto wanne wa kiume: Yonathani ambaye anajulikana sana kwa vitendo vyake vya kishujaa na urafiki wake na Daudi (1Sam 14:1-46; 18:3-4), Abinadabu ambaye anatajwa tu hapa, Malki-shua ambaye anatajwa pia katika 1Sam 14:49, na Ishboshethi (taz 1Sam 14:49 maelezo). Huyu wa mwisho hakuwako vitani na alitangazwa mfalme badala ya baba yake (2Sam 2:8-10). Uhusiano wake na Daudi ulikuwa mbaya (2Sam 2—4).]
3Vita vilikuwa vikali sana dhidi ya Shauli. Wapiga mishale walipomwona walimjeruhi vibaya.
4Ndipo Shauli alipomwambia mtu aliyembebea silaha, “Chomoa upanga wako unichome nife, ili watu hawa wasiotahiriwa wasije wakanichoma upanga na kunidhihaki.” Lakini huyo aliyembebea silaha hakuthubutu kwa sababu aliogopa sana. Hivyo, Shauli alichukua upanga wake mwenyewe, na kuuangukia.[#31:4 Shauli anapendelea kufa kabla ya kukamatwa na Wafilisti asije akanyenyekeshwa na kudhalilishwa kama Samsoni (Amu 16:23-25). Lakini huyo mtumishi hakuthubutu labda kwa kujua kwamba Mungu angemwadhibu mtu ambaye amemuua mteule wa Mungu (26:9).]
5Halafu yule aliyembebea silaha alipoona kuwa Shauli amekufa, naye pia aliuangukia upanga wake, akafa pamoja na Shauli.[#31:5 Ilikuwa kawaida kwa mtumishi kujiua mwenyewe wakati bwana wake alipokufa vitani. Jamb la kujiua hutajwa mara chache sana katika Biblia na karibu kila mara ni kwa sababu kubwa sana kama vile utovu wa utii kwa Mwenyezi-Mungu (2Sam 17:23; 1Fal 16:18 na Mat 27:5).]
6Hivyo ndivyo Shauli alivyokufa, na wanawe watatu, pia na mtu aliyembebea silaha pamoja na watu wake wote katika siku hiyohiyo moja.
7Nao Waisraeli waliokuwa upande wa pili wa bonde, na wengine waliokuwa upande wa mashariki wa mto Yordani walipoona kuwa Waisraeli wamekimbia, naye Shauli na wanawe wamekufa, waliihama miji yao, wakakimbia. Wafilisti wakaenda na kukaa katika miji hiyo.
8Kesho yake, Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa walizikuta maiti za Shauli na wanawe mlimani Gilboa.
9Walikata kichwa cha Shauli na kumvua silaha zake; halafu waliwatuma wajumbe katika nchi yao yote ya Filistia kutangaza habari njema nyumbani mwa sanamu zao na kwa watu.
10Zile silaha zake waliziweka nyumbani mwa Maashtarothi; kisha wakautundika mwili wake kwenye ukuta wa mji wa Beth-sheani.[#31:10 Kuhusu Maashtarothi taz 1Sam 7:3. Kufanya hivyo aghalabu kunaashiria ni ushindi wa miungu yao dhidi ya Mungu wa Israeli.]
11Lakini wakazi wa mji wa Yabesh-gileadi waliposikia Wafilisti walivyomtendea Shauli,[#31:11-13 Rejea 2Sam 2:4-7. Kwa kufanya hivyo wakazi wa Yabesh-gileadi walionesha shukrani zao kwa Shauli ambaye aliwaokoa katika hali ya kuaibishwa (rejea 1Sam 11).]
12mashujaa wote waliondoka, wakasafiri usiku kucha, wakaondoa mwili wa Shauli na miili ya wanawe kutoka ukuta wa Beth-sheani; wakaja nayo mpaka Yabeshi na kuiteketeza huko.
13Baadaye, wakaichukua mifupa yao na kuizika chini ya mkwaju huko Yabeshi; nao wakafunga kwa muda wa siku saba.[#31:13 Kuhusu muda wa maombolezo katika Israeli ya kale, rejea Mwa 50:10.]