1 Samueli 7

1 Samueli 7

1Kisha, watu wa Kiriath-yearimu wakaenda na kulichukua sanduku la Mwenyezi-Mungu, wakalipeleka nyumbani kwa Abinadabu, aliyeishi milimani. Wakamweka wakfu mtoto wake wa kiume aliyeitwa Eleazari ili alitunze sanduku hilo.

Samueli anatawala Israeli

2Tangu sanduku la Mwenyezi-Mungu lipelekwe mjini Kiriath-yearimu muda mrefu ulipita, miaka ishirini hivi. Wakati huo Waisraeli wote walimlilia Mwenyezi-Mungu.

3Samueli akawaambia Waisraeli, “Kama mnamrudia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wenu wote, ni lazima mwondoe kati yenu miungu ya kigeni na sanamu za Ashtarothi. Mwelekeeni Mwenyezi-Mungu kwa moyo wote, na kumtumikia yeye peke yake; naye atawaokoa kutoka mikononi mwa Wafilisti.”[#7:3-4 Mahali pengine anajulikana kama “Ashera”. Huyu alikuwa mungu wa kike wa rutuba. Wafuasi wake waliamini kwamba alisababisha ardhi kuwa na rutuba na kuwapatia watoto wengi. Jina “Baali” maana yake ni “Mwenye kuhodhi” au “Bwana”. Watu waliomwabudu waliamini kuwa yeye alisababisha dhoruba ya radi na mvua na kusababisha rutuba.]

4Hivyo, Waisraeli wakatupilia mbali sanamu za Mabaali na Maashtarothi, wakamtumikia Mwenyezi-Mungu peke yake.

5Kisha, Samueli akawaita Waisraeli wote wakutane huko Mizpa, akawaambia, “Huko nitamwomba Mwenyezi-Mungu kwa ajili yenu.”

6Hivyo, Waisraeli wote wakakusanyika huko Mizpa. Walichota maji na kuyamimina mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakafunga siku ile yote na kusema, “Tumetenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu.” (Samueli alikuwa mwamuzi wa Waisraeli huko Mizpa).[#7:6 Kiebrania maana yake ni “mnara wa ulinzi”. Katika Agano la Kale jina hili linatumiwa kutaja mahali mbalimbali (Mwa 31:44-52; Yos 11:3,8; Amu 11:34; 1 Sam 10:17). Mispa, mji unaohusika hapa ulikuwa yapata kilomita 8 kaskazini ya Yerusalemu.]

7Wafilisti waliposikia kuwa Waisraeli wamekusanyika huko Mizpa, wakuu watano wa Wafilisti wakaenda kuwashambulia. Waisraeli waliposikia juu ya jambo hilo waliwaogopa Wafilisti.

8Basi, wakamwambia Samueli, “Usiache kumlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwa ajili yetu. Endelea kumlilia atuokoe kutoka kwa Wafilisti.”

9Kwa hiyo Samueli alichukua mwanakondoo anayenyonya akamtolea Mwenyezi-Mungu kama sadaka ya kuteketezwa nzima. Kisha Samueli akamlilia Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya Israeli, naye akajibu kilio chake.

10Samueli alipokuwa anatoa ile sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti walikaribia kuwashambulia Waisraeli. Lakini Mwenyezi-Mungu akatoa sauti kubwa ya ngurumo dhidi ya Wafilisti, na kuwavuruga Wafilisti, nao wakatimuliwa mbele ya Waisraeli.

11Waisraeli walitoka Mizpa na kuwafuatilia Wafilisti mpaka karibu na mji wa Beth-kari, wakawaangamiza.

12Kisha, Samueli alichukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mizpa na Sheni, akaliita jiwe hilo Ebenezeri akisema, “Mwenyezi-Mungu ametusaidia mpaka sasa.”

13Siku hiyo Wafilisti walishindwa; na Mwenyezi-Mungu aliwazuia Wafilisti kuivamia nchi ya Israeli wakati wote Samueli alipokuwa hai.

14Miji yote ya Waisraeli ambayo Wafilisti waliiteka kati ya Ekroni na Gathi ilirudishiwa Waisraeli, nao walikomboa nchi yao kutoka kwa Wafilisti. Tena kulikuwa na amani kati ya Waisraeli na Waamori.

15Samueli alikuwa mwamuzi wa Israeli maisha yake yote.

16Kila mwaka Samueli alitembelea Betheli, Gilgali na Mizpa, na kuwaamua Waisraeli katika miji hiyo yote.[#7:16 Katika Mwa 28:19, jina la awali lilikuwa “Luzu”. Betheli ni maarufu sana katika historia ya Waisraeli: Abrahamu alijenga hapo mahali pa kutambikia (Mwa 12:8); Yakobo naye alijenga hapo mahali pa ukumbusho (Mwa 35:1-16) na wakati mmoja sanduku la agano liliwekwa huko (Amu 20:27).]

17Kisha, alikuwa akirudi Rama, maana huko kulikuwa nyumbani kwake; aliwaamulia Waisraeli haki zao huko, na kumjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu huko.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania