3 Yohane 1

3 Yohane 1

1Mimi mzee, nakuandikia wewe Gayo, rafiki yangu, ninayekupenda kweli.[#1 Taz 2Yoh 1 maelezo.; #1 Hatuna habari zaidi za huyu ila ni dhahiri alikuwa mtu maarufu katika kanisa fulani.; #1-2 Barua hii inaanza kwa mtindo wa kuandika barua za binafsi wa nyakati hizo. Gayo: Jina la kawaida la Kiroma; katika A.J. kuna watu wengine watatu wenye jina hilohilo: (Mate 19:29; 20:4; Rom 16:23; 1Kor 1:14).]

2Mpenzi wangu, nakutakia mafanikio mema ya kila aina; nakutakia afya njema ya mwili kama ulivyo nayo rohoni.

3Nimefurahi sana ndugu kadhaa walipofika hapa, wakashuhudia juu ya uaminifu wako kuhusu ukweli; naam, wewe unaishi daima katika ukweli.

4Hakuna kitu kinachonifurahisha zaidi kuliko kusikia kwamba watoto wangu wanaishi katika ukweli.[#4 Rejea 1Kor 4:15; Gal 4:19, File 10. Labda pia ni watu ambao huyo mwandishi alikuwa amewaongoza wakawa wafuasi wa Yesu.]

Uaminifu wa Gayo

5Mpenzi wangu, wewe ni mwaminifu kila mara unapowahudumia ndugu, hata kama ni wageni.[#5 Ukarimu kwa Wakristo waliokuwa safarini ulikuwa jambo la desturi na kawaida katika Kanisa (taz pia Rom 12:13 maelezo).]

6Ndugu hao wamelieleza kanisa hapa habari za upendo wako. Tafadhali uwasaidie waendelee na safari yao kwa namna itakayompendeza Mungu.

7Maana wanaanza safari yao katika utumishi wa Kristo bila kupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasioamini.

8Basi, sisi tunapaswa kuwasaidia watu hawa, ili nasi tupate kushiriki katika kazi yao kwa ajili ya ukweli.

Diotrefe na Demetrio

9Niliandika barua fupi kwa hilo kanisa; lakini Diotrefe, ambaye hupenda kuwa kiongozi wao, hataki kabisa kunisikiliza.[#9 Huyu alikuwa kiongozi wa kanisa ambalo (au jumuiya ya waumini) Gayo alikuwa mmoja wao. Jina hilo linatajwa hapa tu katika A.J.; #9 Barua hiyo inayotajwa hapa haikuhifadhiwa.]

10Basi, nitakapokuja nitayafichua mambo yote anayofanya, maneno mabaya anayotutolea na uongo anaosema juu yetu. Isitoshe, yeye hukataa kuwakaribisha hao ndugu walio safarini, na hata huwazuia watu wengine wanaotaka kuwakaribisha, na hujaribu kuwafukuza nje ya kanisa.

11Mpenzi wangu, usifuate mfano mbaya, bali mfano mwema. Kila atendaye mema ni wa Mungu; lakini anayetenda mabaya hajapata kumwona Mungu.

12Kila mtu anamsifu Demetrio; naam, ukweli wenyewe unamsifu. Nasi pia tunatoa ushahidi wetu juu yake, nawe wajua kwamba tunachosema ni kweli.[#12 Yamkini huyu alikuwa mmoja wa waumini wa jumuia hiyohiyo ambamo alikuwa Gayo; au mmoja wa Wakristo waliowaletea habari njema na ambao wengine wanatajwa katika aya 5-8; inawezekana kwamba Demetrio ndiye aliyeipeleka barua hiyo kwa jumuia hiyo.]

Salamu za mwisho

13Ninayo bado mengi ya kukuambia, lakini sipendi kuyaandika kwa kalamu na wino.

14Natumaini kukuona karibuni na hapo tutazungumza ana kwa ana.

15Nakutakia amani. Rafiki zako wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu wote kila mmoja binafsi.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania